Serengeti kujengwa madaraja makubwa matano kudhibiti mafuriko

Serengeti. Serikali imepanga kujenga madaraja makubwa matano katika maeneo korofi ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, ikiwa ni hatua ya kudhibiti athari za mvua kubwa zinazoendelea kunyesha na kuharibu miundombinu ya barabara na vivuko.

Mbali na madaraja hayo makubwa, pia yanatarajiwa kujengwa madaraja madogo matano katika maeneo mengine yenye changamoto, hatua inayolenga kupunguza usumbufu kwa watalii na watumiaji wengine wa barabara hasa katika kipindi cha mvua za masika.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa, Machi 6, 2026 na Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayesimamia Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara katika Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Massana Mwishawa, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la Bwawa la Viboko la Nabi, Serengeti.

Mwonekano wa baadhi ya magari ya utalii, yakivuka eneo la Bwawa la Viboko vya Nabi,katika Hifadhi ya Taifa Serengeti leo Ijumaa Machi 6,2026 eneo ambalo ni miongoni mwa maeneo korofi yaliyoathiriwa na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha ambapo kivuko chake kimeharibiwa na mvua hizo.



Mwishawa amesema eneo hilo ni miongoni mwa yaliyoathirika zaidi kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha, ambazo zimesababisha maji kufurika na kukata kivuko hicho.

Amesema mwaka huu mvua zimekuwa nyingi zaidi kuliko ilivyokuwa katika miaka ya nyuma, hali iliyosababisha uharibifu wa baadhi ya miundombinu ya barabara na vivuko ndani ya hifadhi hiyo.

“Maeneo mengi yameathirika, lakini hapa changamoto ni kubwa zaidi. Hata hivyo hadi sasa hakuna majeruhi wala vifo vilivyoripotiwa. Wote waliotumia barabara hizi wako salama. Serengeti bado ni salama licha ya changamoto hizi,” amesema.

Amesema suluhisho la kudumu ni kujenga madaraja makubwa matano yenye matundu makubwa yatakayowezesha maji kupita kwa urahisi, ili kupunguza athari za mafuriko kwa watalii, watumishi wa hifadhi na watumiaji wengine wa barabara.

“Tunahitaji madaraja makubwa matano ya juu yenye matundu makubwa yatakayopitisha maji kwa haraka. Pia kutakuwa na madaraja madogo matano katika maeneo mengine yenye changamoto,” amesema.

Ameongeza kuwa tayari maandalizi ya bajeti kwa ajili ya utekelezaji wa mpango huo yameanza, huku lengo likiwa kuhakikisha watalii wanaotembelea hifadhi hiyo wanaingia, kufanya shughuli za utalii na kuondoka wakiwa salama.

“Changamoto hii imesababishwa na mvua kubwa ambazo hazijawahi kushuhudiwa kwa kiwango hiki kwa miaka mingi. Ndiyo maana tunapanga kuweka miundombinu imara zaidi,” amesema.

Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi,Ismail Omary, akitoa maelekezo kwa mmoja wa askari katika eneo la Bwawa la Viboko vya Nabi,hifadhini humo leo Ijumaa Machi 6,2026.



Aidha, Mwishawa amewataka watumiaji wa barabara ndani ya hifadhi hiyo, hususan madereva na waongoza watalii, kufuata maelekezo ya askari wanapokutana na maeneo yenye maji mengi.

“Ni afadhali mgeni achelewe kufika anakoenda lakini awe salama,” amesema.

Awali, Mkuu wa Hifadhi ya Serengeti, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Ismail Omar, ametaja maeneo matatu yaliyoathirika zaidi kuwa ni Bwawa la Viboko la Nabi, Mto Mokasi na Bwawa la Bona.

Amesema mvua zinazoendelea kunyesha zimesababisha uharibifu wa miundombinu ya barabara na maji kutuama katika maeneo mengi ya hifadhi hiyo, hali inayosababisha usumbufu kwa shughuli za utalii na ulinzi.

“Hifadhi hii ina misimu miwili ya mvua. Bahati mbaya msimu wa mvua ndogo wa Novemba na Desemba haukuwepo, hivyo masika yameanza kwa mvua nyingi zilizojaza maji barabarani na kuharibu miundombinu ikiwemo vivuko,” amesema.

Amesema hali hiyo ilisababisha msongamano wa zaidi ya magari 200 ya watalii yaliyokuwa yakisubiri maji yapungue ili yaweze kuvuka katika baadhi ya maeneo yaliyoathirika.

Kwa sasa, amesema Tanapa imeanzisha operesheni ya uokoaji katika maeneo hayo kwa kupeleka vikosi maalumu vilivyo na vifaa mbalimbali ikiwemo greda na trekta ili kusaidia magari yaliyokwama.

Pia amesema wanatumia ndege kubaini magari yaliyokwama ndani ya hifadhi hiyo, ambapo baada ya kubainika hutumwa taarifa za GPS kwa timu za uokoaji ili ziweze kufika kwa haraka.

“Kulikuwa na tukio moja ambapo dereva alikaidi maelekezo ya askari waliokuwa wakiongoza magari kuvuka kivuko na kujaribu kupita mwenyewe, jambo lililosababisha gari lake kukwama majini. Ndani ya gari hilo kulikuwa na watalii watatu ambao wote waliokolewa salama,” amesema.

Amesema askari wamewekwa katika vivuko vyenye changamoto kuanzia asubuhi hadi jioni ili kuongoza magari yanayopita na kuhakikisha usalama wa watumiaji wa barabara.

Aidha, Tanapa inaendelea kufanya ukarabati wa dharura kwa baadhi ya vivuko vilivyochimbika kutokana na maji, huku malori yakipeleka mawe katika maeneo hayo ili kurejesha hali ya barabara.

“Hakuna madhara makubwa yaliyowapata wageni zaidi ya kuchelewa kwa safari. Wageni wote waliochelewa kutokana na changamoto hii hawakutozwa malipo ya ziada hata kama walitakiwa kuondoka siku iliyotangulia,” amesema.

Mmoja wa waongoza watalii, Bryson Msuya mwenye uzoefu wa miaka 25 katika kazi hiyo, amesema ni muhimu Serikali kujenga daraja la kudumu katika eneo hilo ili kuondoa tatizo hilo.

“Hali imekuwa ngumu kwa wageni na wengi wamekuwa na hofu. Tatizo la kivuko hiki ni la muda mrefu, hivyo ni vyema kujengwa daraja imara litakaloruhusu maji kupita chini kama ilivyo kwenye Daraja la Ruvu,” amesema Msuya.

Naye mwongoza watalii mwingine, Israel Nnko amesema barabara nyingi ndani ya hifadhi hiyo huwa na changamoto kubwa wakati wa mvua, hivyo ujenzi wa daraja utasaidia kurahisisha usafiri.

Kwa upande wake, mtalii kutoka Denmark, Nichlas Lerche amesema wamefurahia kuona mandhari na wanyama mbalimbali ndani ya hifadhi hiyo, ingawa miundombinu ya barabara imekuwa changamoto katika kipindi hiki cha mvua.