WATAALAMU WALIOSOMA JAPAN WACHOCHEA MIRADI YA MAENDELEO NCHINI


 ::::::::

Wataalamu wa Kitanzania waliopata mafunzo nchini Japan wameelezwa kuwa rasilimali muhimu katika kuharakisha maendeleo ya sekta mbalimbali kwa kutumia ujuzi na teknolojia walizojifunza nje ya nchi.

Akizungumza katika mkutano uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Msaidizi wa Ofisi ya Rais – Utumishi, Fadhili Mitimingi, amesema ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Japan International Cooperation Agency (JICA) umewezesha Watanzania wengi kupata mafunzo ya kitaalamu nje ya nchi.

Mtimingi ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Utumishi katika Mkutano Mkuu wa Japan Alumni of Tanzania Association (JATA), amesema wahitimu wa mafunzo hayo wamekuwa wakirejea nchini na kuanzisha miradi mbalimbali ya maendeleo.

Amesema kupitia miradi hiyo, wataalamu hao wamekuwa wakisambaza maarifa waliyopata kwa wananchi wengine ili kusaidia matumizi ya mbinu bora na za kisasa katika uzalishaji.

“Hatua hiyo imechangia kuboresha maisha ya wananchi kwa kuwahamasisha kutumia teknolojia na mbinu mpya katika sekta muhimu za uchumi,” amesema Mitimingi.

Kwa upande wake, Balozi wa Japan nchini Tanzania, Mikami Yoichi, amesema mkutano huo ulihusisha mawasilisho ya miradi kutoka kwa washiriki watatu waliowasilisha kazi walizozitekeleza baada ya kurejea nchini.

Naye Mwenyekiti wa JATA, Gregory Mlay, amesema umoja huo unawakutanisha wataalamu kutoka sekta mbalimbali zikiwemo kilimo, mifugo, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), biashara na afya ili kushirikiana katika miradi ya maendeleo.

Katika hatua Nyingine, Mwakilishi Mkazi wa JICA Tanzania, Ara Hitoshi, amesema  lengo kuu la mafunzo hayo  ni kuchangia maendeleo ya Tanzania ili kufanikisha hilo, washiriki wanaporudi kutoka kwenye mafunzo wanapaswa kuchukua hatua za kuwasaidia wengine kwa kutumia maarifa na uzoefu walioupata.

Mmoja wa wanufaika wa mafunzo hayo, Godfrey Christopher, amesema wamejifunza mbinu za kuongeza thamani ya mazao ya uvuvi kupitia usindikaji na uhifadhi bora, hatua inayosaidia kupunguza upotevu wa mazao na kuongeza kipato cha wananchi.