Dar es Salaam. Wataalamu wa saikolojia duniani wametengeneza ‘Kanuni ya siku 90’ kama mhimili wa mabadiliko ya tabia ya mtu, endapo jambo litafanyika kwa siku hizo mfululizo, inakuwa tabia.
Limekuwa ni jambo gumu kwa mtu kubadili tabia, kwa mfano mtu anayetaka kuacha kunywa pombe, uasherati, au kutumia dawa za kulevya. Hata hivyo, wataalamu wanaeleza kwamba ukifanikiwa kusitisha mambo hayo kwa siku 90 mfululizo, unafanikiwa, inakuwa tabia yako.
Vilevile, wengine wamekuwa wakipata shida kufanya mazoezi ya viungo au kusoma vitabu. Ili kujenga tabia hizo, wanashauriwa kuanza na kufanya kwa miezi mitatu mfululizo, hapo itakuwa tabia yako halisi.
Kanuni ya 21/90 inaeleza kwamba inachukua siku 21 kuanzisha tabia mpya na siku 90 kuifanya kuwa mtindo wa maisha wa kudumu.
Kwa kufanya vitendo kwa uthabiti kila siku kwa muda wa miezi mitatu mfululizo, unaweza kubadilisha mienendo yako na kuigeuza kuwa utaratibu wa kudumu na wa moja kwa moja, na hatimaye kubadilisha mtazamo wako na utambulisho wako binafsi.
Wataalamu wa mapenzi na uhusiano pia wanatumia kanuni hiyo wanapoeleza kwamba wenza wawili wakiweza kuvuka salama kipindi cha siku 90, basi uhusiano wao utakuwa thabiti, kwani kipindi hicho kinatosha kuijua tabia ya mtu.
Baadhi ya uhusiano huvunjika katika kipindi hicho kutokana na baadhi yao kushindwa kuendana na tabia za watu wao wapendao. Hata hivyo, wengine hujenga ‘bond’ inayowasaidia kuishi vizuri kwa maelewano kila siku.
Mwanasaikolojia Clara Mwambungu anasema mara nyingi hukutana na migogoro inayotokana na watu kujitoa kwa kila kitu kwa wenzi wao, lakini baada ya muda hudhihirisha tabia zao halisi ndani ya uhusiano.
Anasema katika siku 90 za mwanzo, mwili unakuwa kwenye kilele cha homoni ambazo hupofusha uwezo wa kuona upungufu wa mtu unayeanzisha naye uhusiano.
“Mara nyingi tunawashauri watu kutumia miezi mitatu ya mwanzo kama kipindi cha uchunguzi. Baada ya siku 90, ile pazia la ugeni huondoka, na hapo ndipo mtu anaweza kujua kama anaweza kuvumilia tabia za mwenzake au la,” anasema.
Anasema hali hiyo hutumika hata katika kazi na biashara, ambapo mikataba ya ajira nchini huanza na kipindi cha majaribio cha miezi mitatu. Hii ni kwa sababu akili ya binadamu inahitaji takriban siku 60 mpaka 90 kuzoea mazingira mapya, kujua utamaduni wa ofisi, na kuelewa kama uwezo wake unaendana na majukumu.
“Huwa tunasema hutakiwi kukimbilia kuacha kazi au kusema ‘siwezi’ ndani ya mwezi wa kwanza, inatakiwa kuipa akili siku 90. Ukiona bado hufurahii baada ya kipindi hicho, basi hapo kuna tatizo la msingi, si shinikizo la ugeni tu,” anasema Mwambungu.
Anasema hiyo inaendana pia na mabadiliko ya tabia ambayo watu wamekuwa na nadharia kuwa inachukua siku 21 kujenga tabia, lakini tafiti za kisasa za kisaikolojia zinaonesha kuwa ili tabia iwe sehemu ya maisha bila kulazimisha, inahitaji wastani wa siku 66 mpaka 90.
Hali hiyo, anasema, inajengwa katika vitu vingi, iwe ni kuanza mazoezi, kuacha pombe, au kujifunza lugha mpya. Hivyo, haitakiwi kujihukumu ndani ya mwezi mmoja. Ukivuka mstari wa siku 90, akili yako inatengeneza mfumo mpya wa neva unaofanya jambo hilo kuwa sehemu ya maisha ya kawaida.
“Kanuni ya Siku 90 inatufundisha subira, inatukumbusha kuwa mhemko ni wa muda mfupi, lakini tabia na uhalisia ni wa kudumu. Kabla ya kuwekeza hisia, fedha, au muda wako mwingi kwenye jambo jipya, jipe karantini ya siku 90 ili uone kama msisimko utabaki au utatoweka,” anasema.
Mwanasaikolojia mwingine, Jamal Othman kutoka Zanzibar, anasema kumekuwa na changamoto ya subira, hususani kwa vijana wa sasa ambao wapo kwenye ulimwengu wa kuridhika papo kwa hapo, kama vile kupata chakula au taarifa kwa sekunde moja.
Amasema maswali yaliyopo ni kwanini siku 90? Wakati uamuzi unatakiwa kufanywa kwa haraka, lakini hawafikirii muda huo, huongozwa na mhemko wa muda mfupi badala ya mantiki.
“Siku 90 zinasaidia akili kutulia na kuona kama kinachotaka ni hitaji la kweli au ni msisimko tu wa mpito,” anasema Othman.
Anasema vijana wengi hukata tamaa haraka wanapoanza kazi mpya au biashara wakihisi mambo hayaendi, bila kujua kuwa miezi mitatu ya kwanza ni kipindi cha kujifunza kuhusu mifumo. Ni kipindi ambacho inaruhusiwa kukosea na kusahihisha.
Mwanasaikolojia huyo anasema kukimbia kabla ya siku 90, mtu anakuwa ameacha fursa kabla hata akili yake haijazoea. Serikali na mashirika mengi hutumia siku 100 za mwanzo kama kipindi cha kipimo cha dira na uelekeo.
“Kutumia siku 90 kunajenga misuli ya uvumilivu, kujifunza kusubiri matokeo ya biashara au kumjua mtu, kunajenga kinga dhidi ya msongo wa mawazo pindi mambo yanapokwama baadaye. Vijana wanaokimbilia mambo mara nyingi hupata anguko la kisaikolojia mapema zaidi,” anasema.
Pia, anasema kipindi hicho ni cha kuchuja marafiki wa fursa na wakweli, ambapo katika maisha ya kijamii siku 90 ni muda ambao watu huvua magamba yao na kuonesha uhalisia wao. Watu wengi wanaweza kuigiza wema kwa mwezi mmoja, lakini ni vigumu kuendelea kuigiza tabia wasiyo nayo kwa siku 90 mfululizo.
Anasema hiyo inaokoa dhidi ya kuingia kwenye mikataba mibaya ya kibiashara au urafiki wenye sumu, ambao ungegharimu miaka mingi ya maisha ya mbeleni.
“Nawaambia vijana wa sasa ambao wanajiachia kwa marafiki waliokutana nao siku moja, kukata tamaa wiki mbili za kazini, kufunga biashara kwa kukosa wateja kwa mwezi mmoja, siku 90 si kupoteza muda, ni kufanya utafiti. Ni bora kuchelewa kuanza kwa uhakika kuliko kuanza gizani na kuishia kupata hasara ya muda, fedha, na amani ya moyo,” anasema.