Diwani wa Kata ya Makangarawe Fadhili Mboga akizungumza katika hafla ya utoaji wa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto wenye uhitaji kwenye shule ya msingi Yombo Dovya Manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam leo tar 6/3/2026
Diwani wa Viti Maalum, Farida Saumu Mkwanywe akizungumza katika hafla ya utoaji wa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto wenye uhitaji kwenye shule ya msingi Yombo Dovya Manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam leo tar 6/3/2026
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Yombo Dovya
Salum Gawaza akizungumza katika hafla ya utoaji wa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto wenye uhitaji kwenye shule ya msingi Yombo Dovya Manispaa ya Temeke jijini Dar es salaam leo tar 6/3/2026
Picha zote na Mussa Khalid
…………………..
Na Hawa Ismail- Dar es
Salaam
Diwani wa Viti Maalum,
Farida Saumu Mkwanywe, na Diwani wa Kata ya Makangarawe, Fadhili Mboga,
wameungana na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Makangarawe kutoa msaada kwa
watoto wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Yombo Dovya, iliyopo
wilayani Temeke, jijini Dar es Salaam.
Msaada huo umetolewa
Machi 6, 2026 ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake
Duniani, ambayo kilele chake hufanyika kila mwaka Machi 8. Madiwani hao
walisema tukio hilo linaonyesha upendo na mshikamano kwa watoto wenye mahitaji
maalum katika jamii.
Akizungumza katika
hafla hiyo, Diwani wa Viti Maalum Farida Saumu Mkwanywe aliipongeza UWT
Makangarawe kwa kuonesha moyo wa huruma kwa kuwasaidia watoto hao na kuwapa
furaha.
“Nawapongeza sana
Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Makangarawe kwa kuonesha moyo wa upendo kwa
kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum katika Shule ya Msingi Yombo Dovya.
Sisi kama viongozi tutaendelea kuwaunga mkono katika juhudi hizi za kijamii,”
alisema Mkwanywe.
Kwa upande wake,
Katibu wa UWT Makangarawe, Salma Lupinga, alisema kuwa katika kuadhimisha Siku
ya Wanawake Duniani mwaka huu waliamua kutembelea watoto wenye mahitaji maalum
ili kushirikiana nao na kuwapa msaada pamoja na walimu wanaowalea.
Alisema UWT
Makangarawe imekuwa ikifanya shughuli mbalimbali za kijamii kila mwaka, na
safari hii waliona ni vyema kusherehekea siku hiyo kwa kuonesha upendo kwa
watoto hao pamoja na walimu wao.
Naye Diwani wa Kata ya
Makangarawe, Fadhili Mboga, aliwapongeza wanawake wa UWT Makangarawe kwa maono
yao ya kusaidia jamii na kuwashukuru walimu wanaowalea watoto hao kwa kujitolea
kuwasaidia hadi kufikia hatua ya kuendelea na masomo ya sekondari na hata vyuo
vya ufundi.
Mboga alisisitiza kuwa
wanawake ni nguvu kubwa katika jamii, akitolea mfano kuwa katika sekta
mbalimbali za jamii, ikiwemo elimu na shughuli za kijamii, wanawake wamekuwa
mstari wa mbele katika kutoa huduma na mchango mkubwa kwa maendeleo ya jamii.
Aidha, Mwalimu Mkuu wa
Shule ya Msingi Yombo Dovya alisema kituo hicho kina watoto 100 wenye mahitaji
maalum, wakiwemo wavulana 67 na wasichana 33. Alifafanua kuwa watoto hao
wamegawanywa katika hatua tatu za kujifunza, huku wakifundishwa zaidi stadi za
maisha zinazowawezesha baadhi yao kuendelea na masomo katika vyuo vya ufundi
stadi (VETA).
Kwa upande wake, mwalimu
mlezi wa watoto wenye ulemavu, Bi. Naghenywa Mshighati, aliwashukuru madiwani
pamoja na wanawake wa Makangarawe kwa kuwatembelea na kuwapa zawadi watoto hao,
akisema kitendo hicho kinaonesha wazi jinsi wanawake walivyo jeshi kubwa katika
kuonesha upendo na kujali jamii.




