Camara atega kengele kokote! | Mwanaspoti

MITAA ya Kariakoo baada ya dabi kumalizika kwa Yanga na Simba kushindwa kufungana, kuna jambo lingine linaendelea chini kwa chini likiwahusu makipa wa timu hizo. Unaweza kusema ni suala la muda tu ndio jambo litaamuliwa iwe au isiwe.

Makipa hao wote ni wa kimataifa ambao ndio wanacheza vikosi vya kwanza wakiendelea kufanya vizuri kuhakikisha timu zinafikia malengo msimu huu kwa kubeba mataji ya ndani baada ya kimataifa wote kuishia makundi.

Djigui Diarra raia wa Mali anayecheza Yanga na Djibrilla Kassali wa Simba anayetokea Niger ndio makipa namba moja katika vikosi vya timu hizo waliobeba dhamana ya kulinda nyavu zisiguswe, hata hivyo, kuna taarifa kwamba msimu ujao wanaweza wasiwepo mitaa ya Kariakoo kwa sababu mbalimbali.

Sababu ya Diarra ni kwamba kuna ofa zipo mezani zinaangaliwa kama zinafaa, biashara ifanyike mwisho wa msimu huu, lakini upande wa Kassali, ishu yake ya kufanyiwa tathmini aendelee kuwepo Msimbazi au kupewa mkono wa kwaheri.

Ipo hivi; Kassali wakati anatua Simba alipewa mkataba wa miezi sita hadi mwisho wa msimu, kuna uwezekano akaongezewa muda au ndio basi tena.

Wakati makipa hao wakiendelea kukichafua hivi sasa, kinara wa clean sheet msimu uliopita, Moussa Camara yupo anasikilizia mchongo kwamba ataendelea kusalia Kariakoo au kusaka chaka jipya msimu ujao 2026-2027 ukianza baada ya huu 2025-2026 kwake kufungwa mapema kutokana na majeraha ya goti yaliyomkumba.

MAKI 01


Baada ya kumalizika kwa michuano ya AFCON 2025 na timu ya taifa ya Mali kuishia hatua ya robo fainali ilipofungwa 1-0 na bingwa Senegal, huku Diarra akadaka mechi zote, taarifa zinasema kipa huyo ana ofa mezani.

Diarra aliyetua Yanga Agosti 2021 akitokea Stade Malien ya kwao Mali, amekuwa na kiwango bora muda wote kiasi cha kushika namba moja kikosini hapo.

Mbali na hilo, pia amefanikiwa kuwa kipa bora wa Ligi Kuu Bara kwa misimu miwili mfululizo 2021-2022 na 2022-2023, kabla ya 2023-2024 kumaliza nyuma ya Ley Matampi kwa clean sheet nyingi kama ilivyotokea 2024-2025 nyuma ya Mousa Camara.

Agosti 2024, Klabu ya Yanga ilitangaza kumuongezea mkataba Diarra wa miaka mitatu ambao atakuwa hapo hadi mwaka 2027, hivyo ukimalizika msimu huu, atabakiwa na mwaka mmoja wa kuitumikia Yanga.

Taarifa zinabainisha, klabu mbalimbali za Afrika na Uarabuni zinaiwania saini ya Diarra ambapo kuna uwezekano mwisho wa msimu huu biashara ikafanyika.

“Ofa zipo na haikuanza leo, hii imetokana na kiwango bora cha Diarra kila msimu anachokionesha na ukizingatia kwamba anacheza timu ya taifa ya Mali na ndiye kipa namba moja.

“Unajua sio rahisi kikosi cha Mali kilichojaa wachezaji wengi wanaocheza soka nje ya Afrika halafu kipa wake namba moja atokee Ligi ya Tanzania, ukiona hivyo ujue anachofanya Diarra sio kitu cha kawaida, ni kipa wa viwango.

“Klabu nyingi zinamuangalia kama mtu sahihi wa kukaa langoni mwao na ndio maana kuna ofa kibao zinakuja, kinachoangalia ni makubaliano ya Yanga, mchezaji na hao wanaomtaka, ofa ikiwa nzuri biashara itafanyika kwani bado ana mkataba,” kimesema chanzo.

Miongoni mwa klabu zinazomtaka Diarra ni Zamalek ya Misri na CR Belouizdad kutoka Algeria ambazo ziliwasilisha ofa Januari 2026 baada ya kumalizika kwa AFCON 2025.

MAKI 03


Ufiti wa makipa ndani ya kikosi cha Simba ndiyo utaamua kama nafasi hiyo itahitaji mtu mwingine zaidi ama kuendelea na waliopo kwa sasa, hilo linatokana na uwepo wa taarifa ya ndani kuhusu Kassali kwamba ana rekodi za majeraha. 

Kassali raia wa Niger aliyezaliwa Julai 5, 1996 akiwa na umri wa miaka 29, alijiunga na Simba Januari 20, 2026 kuziba pengo la Camara aliyotolewa katika mfumo wa usajili ili ajiuguze majeraha, hilo linawapa alamu vigogo wa Simba skauti ya wachezaji wanayofanya wanatazama eneo hilo pia kuelekea msimu ujao.

Taarifa zinadai kurejea kwa Camara ndani ya kikosi cha Simba aliyemaliza na cleansheets 19 msimu uliopita itategemeana na ufiti pia na kiwango atakachokionyesha Kassali.

“Mechi za Ligi Kuu na za CAF Kassali kafanya vizuri, lakini tufahamu kwamba mpira wa miguu unatumia nguvu, anaweza akajitonesha na malengo ya Simba ni kurejesha ushindani wa kila nafasi, ili kufanya vizuri kila michuano,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;

“Malengo ya klabu ya Simba ni makubwa, ukiachana na msimu huu tumetolewa mapema michuano ya CAF, bado tuna nafasi ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho la FA.

“Tunapozungumzia suala la kuboresha kikosi ni mipango ya muda mrefu inafanyika, ndiyo maana watu wanaofanya skauti ya wachezaji wanaangalia wachezaji ndani na nje kwa nafasi tulizo na uhitaji nazo, likiwemo la kuangalia kipa.”

MAKI 02


Majeraha aliyopata Camara Septemba 28, 2026 katika mechi ya hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Gaborone United iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, yameufanya uongozi wa Simba kumtoa kwenye mfumo na kumsajili Kassali dirisha dogo.

Camara kabla ya kuumia, alicheza mechi tatu za mashindano msimu huu akiwa na jezi ya Simba akianza Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, Ligi ya Mabingwa dhidi ya Gaborone United (ugenini) na Ligi Kuu Bara dhidi ya Fountain Gate. Mechi ya nne marudiano dhidi ya Gaborone United akaumia, akashindwa kuendelea, nafasi yake ikachukuliwa na Yakoub Suleiman ambaye naye kwa sasa ni majeruhi.

Yakoub aliyetua Simba msimu huu akitokea JKT Tanzania, naye anauguza majeraha ya goti aliyopata akiwa na kikosi cha Taifa Stars wakati wa maandalizi ya kushiriki AFCON 2025, mashindano yaliyofanyika Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026 nchini Morocco ambayo kipa huyo hakushiriki baada ya kuumia.

Kuumia kwa Yakoub na majeraha ya awali aliyopata Camara, ndipo Simba ikatumia dirisha dogo la usajili lililofunguliwa Januari 1, 2026 na kufungwa Januari 30, 2026 kumsajili Kassali baada ya kubakiwa na kipa namba tatu pekee, Hussein Abel.

Kwa mujibu wa kanuni za Ligi Kuu toleo la 2025, klabu moja hairuhusiwi kuwa na makipa wawili wa kimataifa ndio maana Simba ikamtoa kwenye mfumo Camara, ikamuingiza Kassali, hata hivyo, Camara bado anasikilizia ishu kwani mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu, kuna uwezekano akarudishwa kama usajili mpya, au akahamia upande wa pili.

Kwa sasa taarifa zimepamba moto kwamba Yanga inampigia hesahu Camara ambaye yupo njiani kupona kabisa majeraha yake baada ya kuanza mazoezi mepesi.

Hesabu za Yanga ni kumsajili Camara endapo itamuuza Diarra.

Yanga inamuona Camara ni kipa wa daraja la juu ukimuweka kando Diarra kwani makipa hao msimu uliopita walichuana vikali kila mmoja akionyesha ubora wake.

Camara alimaliza kinara wa clean sheet akiwa nazo 19 katika Ligi Kuu Bara akicheza mechi 28 kati ya 30, wakati Diarra akimaliza na 17.

Mchuano huo ambao Camara alikuwa ndio msimu wake wa kwanza, unatoa picha ya ubora wake wa daraja la Diarra ambaye naye msimu wa kwanza 2021-2022 alimaliza kinara wa clean sheet akikusanya 15 katika mechi 25 kati ya 30.

Wakati hesabu za Yanga zikiwa hivyo, Simba nayo haijamuacha jumla Camara, inaangalia uwezekano wa kumpa mkataba mpya huu wa sasa ukimalizika lakini hiyo itategemea na Kassali kama atawaridhisha mabosi au kuona waachane naye.