Global Publishers
March 7, 2026
0 Comments
Shambulio kubwa limeripotiwa kutokea katika moja ya viwanja vikuu vya ndege vya kibiashara mjini Tehran, ambapo milipuko na moto mkubwa umeonekana katika Uwanja wa Ndege wa Mehrabad.
Kwa mujibu wa video na picha zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii, ndege moja inaonekana ikiwa imewaka moto huku moshi mzito ukifuka juu ya eneo la uwanja huo wa ndege, ambao ni miongoni mwa viwanja vyenye shughuli nyingi zaidi nchini Iran na hutumika zaidi kwa safari za ndani.
Mashuhuda waliokuwepo karibu na eneo hilo wanasema walishuhudia milipuko mikubwa usiku, huku baadhi yao wakidai kuwa mashambulizi hayo yalikuwa makali zaidi kuliko yaliyowahi kushuhudiwa hapo awali.
Picha za satelaiti zilizopigwa Ijumaa zinaonyesha kuwa kulikuwa na ndege kadhaa zikiwa zimeegeshwa katika uwanja huo kabla ya tukio hilo. Vyombo vya habari vya serikali ya Iran pia vimeripoti kuwa baadhi ya maeneo ndani ya uwanja wa ndege huo yamelengwa katika shambulio hilo.
Tukio hilo linajiri muda mfupi baada ya jeshi la Israel kutangaza kuanza kwa kile walichokiita “wimbi jipya la mashambulizi makubwa” dhidi ya malengo ndani ya Iran.
Hapo awali, tarehe 4 Machi, Israel ilidai kufanya mashambulizi katika uwanja huo wa Mehrabad, ikisema kuwa ililenga mifumo ya ulinzi wa anga ambayo ilidai kuwa ilikuwa tishio kwa operesheni za Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF). Mashambulizi hayo pia yalidaiwa kuharibu sehemu inayotumika kwa utengenezaji na matengenezo ya helikopta ndani ya uwanja huo.
Hadi sasa, bado haijabainika ni sehemu zipi hasa za uwanja wa ndege zimeathirika katika shambulio jipya, huku mamlaka zikichunguza ukubwa wa uharibifu uliosababishwa na tukio hilo.