Arusha. Zikiwa zimebaki dakika chache kuanza kwa mkutano wa 25 wa Kawaida wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Rais wa Rwanda, Paul Kagame, na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix Tshisekedi, hawajawasili jijini Arusha.
Katika mkutano huo, jumla ya Wakuu wa Nchi wanane wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) walitarajiwa kuhudhuria mkutano huo wenye lengo la kuimarisha zaidi ushirikiano wa kikanda.
Jambo hilo limezua sintofahamu huku likihusishwa na mgogoro wa kisiasa na kimaslahi uliopo baina ya nchi hizo mbili.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa EAC, Veronica Nduva, amethibitisha kwamba marais hao hawatahudhuria ana kwa ana kutokana na kuzidiwa na majukumu ya ndani ya nchi.
Amesema marais hao wamewasilisha taarifa rasmi wakieleza kuwa ratiba zao za kazi na majukumu mengine ya kitaifa yamewazuia kushiriki moja kwa moja katika mkutano huo unaofanyika katika ukumbi wa AICC.
Kwa upande wa Rais Kagame, Nduva amesema amewasilisha ujumbe wa kuomba radhi akieleza kuwa anakabiliwa na mgongano wa ratiba pamoja na majukumu mengine ya kikazi ya ndani ya nchi.
“Kutokana na dharura hiyo, amemteua Waziri Mkuu wa Rwanda kumwakilisha katika mkutano huu,” amesema.
Kwa upande wa DRC, Nduva amesema Rais Tshisekedi ameteua mawaziri wawili kuwakilisha nchi yake katika mkutano huo wa viongozi wa EAC.
“Hata hivyo, dharura hizi si ajabu kwani kanuni zetu za utaratibu zinaeleza wazi kwamba iwapo Rais hataweza kuhudhuria kwa sababu yoyote ile, anaweza kuteua mwakilishi wake rasmi kuhudhuria kwa niaba yake.”
Amesema hata katika mikutano mingine ya kimataifa, ratiba za viongozi wa nchi mara nyingi huwa na majukumu mengi ya kitaifa na kikanda.
Hata hivyo, mbali na Rwanda na DRC, Nduva amesema Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, pia hajahudhuria mkutano huo kutokana na changamoto za ndani ya nchi yake, na anawakilishwa na waziri.
Hata hivyo, katika mkutano huo viongozi wengine wa nchi wanachama wamewasili, akiwemo mwenyeji wao Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Mwenyekiti wa mkutano na Rais wa Kenya, William Ruto, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye, pamoja na Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud.
Mkutano huo wa 25 wa wakuu wa Nchi za EAC unatarajia kuzindua rasmi Mkakati wa Saba wa Maendeleo wa EAC (2026/27–2030/31), kufanya uteuzi wa viongozi mbalimbali wa jumuiya, akiwemo Katibu Mkuu na majaji, lakini pia watajadili changamoto za kifedha zinazoikabili EAC na kupitisha sera mpya ya uchangiaji.
Kwa mujibu wa Sekretarieti ya EAC, takribani wajumbe 700 wanatarajiwa kushiriki mkutano huo, wakiwemo wawakilishi wa nchi wanachama, washirika wa maendeleo, mabalozi wa kidiplomasia waliopo Tanzania pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo ya kikanda.
Katika mkutano huo pia wakuu wa nchi wanatarajiwa kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa maamuzi yaliyofikiwa katika mikutano iliyopita ya jumuiya hiyo pamoja na kuidhinisha miswada iliyopitishwa na Bunge la Afrika Mashariki (EALA).
Pia baadaye watafanya uchaguzi wa mwenyekiti mpya atakayemrithi Rais Ruto, huku nchi za Tanzania na Somalia zikitajwa katika nafasi hiyo.
Neema Swai, mkazi wa Arusha, amesema kuwa wanatarajia kusikia maazimio mbalimbali ya utatuzi wa vizuizi visivyo vya kiforodha, lakini pia jinsi utengamano unavyosaidia kupanua soko la ajira kwa vijana katika nchi zote bila ubaguzi.
“Pia tunataka kusikia fursa za kibiashara za bidhaa zitokanazo katika nchi zetu na jinsi tunaweza kuungana mkono sisi kwa sisi bila kuabudu bidhaa za nje ya kanda yetu,” amesema.