Serikali yatoa ahadi ulinzi wa bahari IORA ikiadhimisha miaka 29

Dodoma. Tanzania imesema ulinzi wa bahari na rasilimali zake utaendelea kupewa kipaumbele, hasa katika kipindi hiki ambacho Dunia inapitia changamoto ya mabadiliko ya tabianchi.

Kauli hiyo imetolewa leo, Jumamosi, Machi 7, 2026, na Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira anayeshughulikia Mazingira, Balozi Baraka Luvanda, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Jumuiya ya Nchi za Mwambao wa Bahari ya Hindi, ijulikanayo kama IORA Day.

Balozi Luvanda amesema maadhimisho hayo yanawezesha kutathmini walipotoka, walipo sasa na wanapokwenda, kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia, kijamii na kiuchumi, mafanikio na changamoto zinazotokana na mabadiliko hayo, ikiwemo mabadiliko ya tabia nchi.

Naibu Katibu Mkuu amesema kwamba wakati wote wanazitambua changamoto zinazozunguka nchi zilizopo ukanda wa bahari, na kwamba zitaendelea kuwepo kutokana na sababu mbalimbali za kidunia, lakini wako tayari kukabiliana nazo.

Amesema jumuiya hiyo imeendelea kuwa jukwaa muhimu linaloleta pamoja nchi zinazozunguka Bahari ya Hindi ili kushirikiana katika masuala ya kipaumbele, hususan usalama na ulinzi wa bahari, uchumi wa buluu, biashara na uwekezaji, usimamizi wa uvuvi, utalii, usimamizi wa maafa, uwezeshaji wanawake kiuchumi, sayansi na teknolojia.

“Kwa zaidi ya miongo miwili, jumuiya hii imekuwa kichocheo muhimu cha kuhamasisha maendeleo baina ya nchi wanachama kupitia matumizi sahihi na endelevu ya rasilimali za bahari. Ni muhimu tukaendelea kutambua hilo na kupambana na mabadiliko ya tabia nchi,” amesema Balozi Luvanda.

Kwa mujibu wa mwanadiplomasia huyo, Tanzania ni mojawapo ya nchi wanachama 15 waanzilishi wa Jumuiya ya IORA kutoka bara la Afrika, Asia na Australia, na inatambua umuhimu wa Bahari ya Hindi kama chanzo kikubwa cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Hata hivyo, amesisitiza suala la upandaji miti kama njia ya kupambana na mabadiliko hayo, ili kulinda uoto wa asili na kupunguza joto.

Awali, Kaimu ya Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Mambo ya Nje, Lilian Mukasa, amesema maadhimisho hayo wameona yaendane na zoezi la kupanda miti, ili iwe kumbukumbu muhimu kwa ajili ya kutimiza miaka 29 ya jumuiya.

Mukasa amesema nchi zilizo mwambao wa Bahari ya Hindi zinaendelea kutambua umuhimu wa utunzaji wa mazingira na mkakati wa kuendeleza mapambano hayo, huku akibainisha kuwa Tanzania haitarudi nyuma.