Shinyanga. Ziara ya Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi mkoani Shinyanga imefufua tumaini la kurudi darasani kwa binti aliyekwama kujiunga na Chuo kutokana na familia yake kukosa ada ya kumsomesha.
Kihongosi ambaye leo Machi 7, 2026 anahitimisha ziara ya siku nne mkoani Shinyanga, amejitolea kumsomesha binti huyo baada ya mama yake kuomba asaidiwe ili mwanaye aendelee na masomo baada ya kukwama kwa mwaka mmoja kwa kile alichodai familia yake imeshindwa kumsomesha.
Mama huyo aliyejitambulisha kwa jina la Rosemary Pastory, alikuwa miongoni mwa mamia ya waliohudhuria mkutano wa hadhara wa CCM uliofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Town, Shinyanga mjini.
Rosemary alikuwa miongoni mwa wananchi 18 waliopata nafasi ya changamoto zao kusikilizwa na Kihongosi.
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi akisikiliza changamoto za wananchi katika mkutano wa hadhara Shinyanga mjini.
Mama huyo alisema binti yake alimaliza kidato cha sita na alitakiwa kujiunga na chuo kikuu cha Dodoma tangu mwaka jana, lakini imeshindikana kwa kuwa wazazi wake hawana uwezo wa kumsomesha.
“Hadi kufika kidato cha sita tumehangaika, baba yake ni mlemavu na mimi mama yake sina uwezo wa kumsomesha tena,” amesema mama huyo kabla ya Kihongosi kumuuliza alipo huyo mtoto na kama nafasi yake chuoni bado ipo.
Rosemary amesema binti yupo nyumbani na Kihongosi kuahidi kumsomesha binti huyo akitaka taratibu zifanyike, tukio ambalo lilimtoa machozi ya furaha mama huyo.
Rosemary ni miongoni mwa wananchi 18 wa Shinyanga mjini waliopata fursa ya kueleza changamoto zinazowakabiri katika masuala mbalimbali ikiwamo ya kijamii na kiutawala.
Changamoto nyingine ilikuwa ya watu 65 wanaosotea malipo yao katika kibarua cha kufanya usafi, eneo la Shinyanga mjini.
Mmoja wao akizungumza kwa niaba ya wengine, alidai tangu Oktoba mwaka jana hadi Machi 6, 2026 jioni saa 10 walipokuwa kwenye mkutano wa hadhara wa Kihongosi, hawakuwa wamelipwa ujira wao wa Sh400,000 ambayo ni malimbikizo ya kuanzia Oktoba, 2025.
Kihongosi alimuuliza mkurugenzi endapo anafahamu kuhusu malalamiko hayo na kukiri kuwa ni kero ambayo anaifahamu.
Amesema walikuwa hawana fedha lakini hadi kufikia Jumatano ijayo (Machi11, 2026), watu hao 65 watakuwa wamelipwa.
Wananchi wakiwa kwenye mkutano wa hadhara wa Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenani Kihongosi uliofanyika kwenye uwanja wa shule ya Msingi Town ulipo Shinyanga mjini.
Kihongosi amebeba dhamana kwenye hilo na kutoa namba yake ya simu akibainisha kwamba katika kipindi walichoahidiwa kulipwa, atakuwa Simiyu, kama hawatawalipa, atatafuta fedha za kuwalipa watumishi hao.
Changamoto nyingine ambayo iliibua hisia tofauti ni ya Queen Emmanuel, mama wa mtoto mmoja aliyedai kutelekezwa na mume wake waliyeishi pamoja tangu 2014.
Alidai mumewe anafanya kibarua stendi ya soko kuu, lakini hahudumii familia na amekuwa akimpiga, kabla ya Kihongosi kumshauri kutoa taarifa polisi siku atakayompiga tena, huku akisisitiza umuhimu wa nidhamu kwa wanawake ndani ya nyumba.
“Wanaume wanamapungufu yao, lakini huwa hawapati nafasi ya kusikilizwa,” amesema Kihongosi na kumtaka mama huyo kurudi nyumbani na kukaa na mumewe waombane radhi huku akimtaka mkuu wa wilaya ya Shinyanga, afisa ustawi wa jamii na mwenezi wa mkoa kuwa kwenye timu ya maridhiano kwa lengo la kurejesha amani kwenye ndoa ya Queen.
Amempatia mtaji wa Sh1 milioni kabla ya kuwaita wabunge wa mkoa wa Shinyanga ambao nao wamemchangia mama huyo papo hyapo jumla ya Sh410,000.
Changamoto nyingine ilikuwa ya Teddy Kilangi aliyedai kuna mmoja wa watendaji amegushi saini yake na kumbambikia mkopo wa Sh5 milioni na kisha kapelekwa mahakamani ambako aliamliwa ameamriwa alipe deni hilo.
Kihongosi aliamuru mtendaji huyo aitwe kwenye mkutano huo, lakini hadi unakwisha hakuwa ametokea na Kihongosi kumtaka afike hotelini alipofikia Kihongosi aliyeambatana na mlalamikaji ili kujua mbivu na mbichi za malalamiko hayo kabla ya siku kuisha.
Changamoto nyingine ilikuwa ya mwenyekiti wa kijiji cha Shilagela, Ndulungudu Njagi ambaye aliomba afikishiwe salamu kwa waziri wa Tamisemi akieleza wao kulipwa posho ya Sh 10,000 ambayo ni ndogo na wakati mwingine malipo yanasuasua.
Akijibu hilo, mmoja wa wahusika alisema Halmashauri inapokea kila mwezi Sh 1milioni ambayo ni posho inayotolewa baada ya mishahara.
“Wenyeviti wengi hawana akaunti, wanapewa cash au wanaingiziwa kwenye simu, hivyo kuanzia kesho (Machi 7) watapewa pesa zao, kuhusu kiwango cha Sh 10,000 kwa mwezi Halmashauri yetu bado ipo chini,” amesema.
Katika mkutano huo Kihongosi alisikiliza na kutatua changamoto nyingine 20 ikiwamo za migogoro ya ardhi ambazo alizielekeza mwa kwa mkuu wa wilaya na zile za kijamii ambazo baadhi alizitatua palepale na nyingine alizielekeza kwenye mamlaka husika ikiwamo za kisheria, sambamba na kumkatia bima ya afya mzazi ambaye kijana wake anasumbuliwa na sikoseli na hana uwezo wa kumhudumia.