Maajabu ya Prince Dube Yanga

MSHAMBULIAJI wa Yanga, Prince Dube anaendelea kuonyesha ubora uwanjani kwenye kufunga mabao lakini kuna sura nyingine bora anaendelea kuisambaza nje ya uwanja ikiakisi mafanikio yake ndani ya klabu hiyo.

Dube moto wake uko juu mpaka sasa ndani ya Yanga akiwa ndiye kinara wa ufungaji kikosini hapo ndani ya Ligi Kuu Bara akifunga mabao sita kwenye mechi 12 za timu hiyo akiwa ameshafunga karibu ya nusu ya mabao aliyoyafunga msimu uliopita alipomaliza na 13.

Ndani ya kikosi cha Yanga, Dube amekuwa akikumbana na ukame wa mabao lakini pia unaotokana na kutotumia nafasi vizuri lakini bado umuhimu wake kwenye kikosi hicho umekuwa mkubwa.

Dube akiwa ndani ya kikosi cha Yanga, amekuwa akitoa wakati mgumu kwenye ukuta wa timu pinzani kwa namna alivyo na kasi lakini hatulii sehemu moja, na kuifanya Yanga kuwa hatari zaidi eneo la mbele.

Yanga ikiwa bila Dube muda mwingi inakuwa inazuilika kirahisi kuliko anavyokuwa uwanjani hatua inayoendelea kumpa umuhimu raia huyo wa Zimbabwe anayeitumikia timu hiyo kwa msimu wa pili tangu atokee Azam FC.

Kiungo wa JS Kabylie, Babacar Sarr akimuelezea Dube, amesema mshambuliaji ni mtu muhimu kwenye safu ya ushambuliaji ya Yanga ambapo mabeki wamekuwa wakipata kazi namna ya kumdhibiti kutokana na mikimbio yake.

DUB 01


“Tulipokutana na Yanga kama kuna mchezaji alitupa wakati mgumu alikuwa yule jezi namba 29 (Dube), wakati wote anakimbia uwanjani utamuona kulia, atakwenda kushoto na katikati, wakati wote hatulii,” amesema Sarr ambaye ni staa wa zamani wa Simba.

“Tulipokutana nao (Yanga) nakumbuka wakati wa mapumziko kule nyumbani kocha wetu aliwaita mabeki na sisi viungo kuhakikisha tunasaidiana kila tunapomuona anahama kwa kuwa huwezi kujua anakwenda wapi na kufanya hesabu gani ni mshambuliaji mzuri sana,” amesema kiungo huyo baada ya Yanga kushinda 3-0 dhidi ya JS Kabylie mechi ya mwisho kundi B katika Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Mbali na hilo, inaelezwa kwamba Dube ana moyo wa uungwana ambapo kuna matukio mawili yamempa heshima ndani ya Yanga akiyafanya kwenye mechi tofauti za timu hiyo msimu huu.

Pale Zanzibar, Dube akiwa na ukame mkubwa wa kufunga mabao, alifikia hatua ya kuomba wenzake asianze kwenye mechi dhidi ya AS FAR Rabat huku akiwataka makocha kumuanzisha Andy Boyeli ambaye alikuwa ametoka kufunga mabao mawili kwenye mchezo uliopita.

DUB 02


“Kuna siku tulikuwa tunaongea kama wachezaji kabla ya kikao cha kwenda kutaja timu, Dube akatuita na kuomba tuwaambie makocha wamuanzishe Boyeli ambaye alitoka kufunga mabao mawili kwenye mechi ya ligi dhidi ya KMC,” alifichua beki mmoja wa Yanga.

“Aliposema hivyo tulimkatalia tukasema hapana na tunashukuru makocha wakamuanzisha yeye badala ya Boyeli na timu ikapata ushindi tena mfungaji wa bao hilo akiwa yeye dhidi ya AS FAR Rabat.”

Tukio lingine la Dube ilikuwa majuzi wakati Yanga ikicheza na Singida Black Stars ambapo mshambuliaji huyo akiwa ndiye kinara wa ufungaji kikosini, huku akiwa tayari amefunga bao la kwanza katika ushindi wa 3-0 kwenye dakika ya 44 Yanga ilipata penalti ambayo Mzimbabwe huyo aliangushwa na Morice Chukwu.

DUB 03


Baada ya mwamuzi Raphael Ikambi kutoka Morogoro kutoa pigo la penalti, Dube alikuwa tayari na mpira akitaka kupiga, lakini akageuka na kumpa mpira kiungo Allan Okello akimtaka apige tuta hilo.

Kumbuka Okello alitua Yanga kwenye dirisha dogo la usajili Januari mwaka huu ambapo tangu afike hakufanikiwa kufunga bao lolote lakini Dube akaona atoe nafasi kwa raia huyo wa Uganda afunge bao lake la kwanza na ikawa hivyo.

Akisimulia tukio hilo, Dube amesema: “Unajua sisi wote ni timu moja, kama ukiona mtu mmoja kwenu hayupo vizuri unatoa nafasi kwake afanye vizuri ili apunguze presha, nashukuru amefunga na sasa anaweza kuendelea kufunga zaidi.”

DUB 04


Mshambuliaji huyo ambaye huu ni msimu wake wa pili anaitumikia Yanga, alianza kucheza Ligi Kuu Bara 2020-2021 akiwa Azam aliyojiunga nayo akitokea Highlanders ya kwao Zimbabwe.

Msimu wa kwanza ndani ya kikosi cha Azam wa 2020-2021, Dube alifunga mabao 14, lakini hadi anaondoka akihudumu hapo kwa misimu minne alifunga mara 34 katika mechi 54.

Msimu wa 2020-2021 alifunga mabao 14, kisha 2021-21 aliingia kambani mara moja kutokana na kusumbuliwa na majeraha yaliyomuweka nje muda mrefu. Msimu wa 2022-23 alifunga mabao 12 na msimu wa mwisho kuitumikia Azam FC 2023-24 alicheza miezi sita na kufanikiwa kufunga mabao saba.

Ndani ya Yanga, msimu wa kwanza alifunga mabao 13, akishika nafasi ya tatu kwa waliofunga mabao mengi Ligi Kuu Bara 2024-2025 nyuma ya kinara Jean Charles Ahoua aliyekuwa Simba akifunga 16, akifuatiwa na Clement Mzize wa Yanga (14). Katika mabao hayo 13, Dube alikuwa sawa na Leonel Ateba (Simba) na Jonathan Sowah aliyekuwa Singida Black Stars kabla ya msimu huu kutua Simba.

Huu ukiwa ni msimu wake wa pili ndani ya Yanga, tayari Dube amefunga mabao 19 katika Ligi Kuu Bara, ukiwa ni mwanzo mzuri zaidi kulinganisha na misimu miwili aliyokuwa Azam alipofunga mabao 15.