Kipa Singida BS atuma ujumbe baada ya kufutiwa tuhuma za upangaji matokeo

MUDA mfupi baada ya Singida Black Stars kutangaza kumuondolea adhabu ya kumsimamisha kwa kipindi cha miezi mitatu kutokana na tuhuma za upangaji matokeo kipa wa kikosi hicho, Amas Obasogie, mwenyewe ameibuka na kutoa shukrani zake kufuatia kutokutwa na hatia.

Mapema leo Machi 7, 2026, Singida Black Stars ilitangaza kumuondolea Obasogie adhabu ya kumsimamisha kwa kipindi cha miezi mitatu baada ya kubaini hakuna ushahidi wa upangaji matokeo wala mchezo wa bahati nasibu aliokuwa akituhumiwa nao.

Ikumbukwe kuwa, Februari 27, 2026, taarifa ya Singida Black Stars iliyotolewa na Ofisi ya Mtendaji Mkuu, Jonathan Kassano ilibainisha kuwachukulia hatua za kinidhamu wachezaji wao, Khalid Aucho kwa utovu wa nidhamu na utoro kazini, huku Obasogie akisimamishwa kazi kwa miezi mitatu pia kupisha uchunguzi wa tuhuma za upangaji wa matokeo.

Baada ya kuondolewa adhabu hiyo, Obasogie amesema: “Habari za mchana wapendwa wote. Jina langu ni Amas Obasogie. Nina furaha kubwa kuwajulisha kuwa suala la tuhuma zilizokuwa zikielekezwa kwangu sasa limetatuliwa kikamilifu.”

Kipa huyo raia wa Nigeria, ameendelea kwa kusema: “Napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa kila mtu aliyesimama nami katika kipindi hiki kigumu, wale walioniombea, walionitakia mema, walionipigia simu kupitia WhatsApp na Instagram wakitaka kujua kinachoendelea. Msaada na upendo wenu umenipa nguvu na matumaini makubwa.

“Kwanza kabisa, namshukuru Mungu Mwenyezi kwa rehema na wema wake. Pia ninatoa shukrani zangu kwa NFF (Shirikisho la Soka Nigeria) kwa kuniamini na kutambua uwezo wangu.

“Ninapenda pia kumshukuru sana Philip Shaibu (Naibu Gavana wa Jimbo la Edo kuanzia 2016 hadi 2024 ambaye ni mwanamichezo na mfanyabiashara mkubwa Nigeria), mtu mwenye mapenzi makubwa na mpira wa miguu ambaye daima amekuwa akiunga mkono mambo mazuri. Shukrani zangu pia ziende kwa SWAM, Benden Insurance na Austin Festers kwa msaada na sapoti yao.

“Pia ninawashukuru sana wanahabari wenye weledi ambao walichukua muda kutafuta ukweli na kuniuliza kabla ya kuchapisha habari.

Ninatoa shukrani za pekee kwa familia yangu na wapendwa wangu ambao waliendelea kuniamini na kunitia moyo wakati wote.

“Shukrani zangu za dhati pia ziende kwa klabu yangu, Sengida Black Stars, ambao walifanya uchunguzi wao na kubaini kuwa tuhuma hizo hazina ukweli, kisha wakaamua kunisafisha na kuruhusu amani itawale.

“Ninawashukuru pia nahodha wangu, wachezaji wenzangu wa ndani na wa kigeni pamoja na ndugu zangu kutoka Nigeria waliopo kwenye timu. Upendo wenu umekuwa mkubwa sana.

“Mwisho, nawapongeza mashabiki wangu wapendwa kwa maombi yenu na sapoti yenu. Mmenipa matumaini makubwa sana. Asanteni sana nyote. Mungu aendelee kuwabariki.”

Singida Black Stars ilianza kumrudisha kazini Aucho Machi 5, 2026 baada ya mchezaji huyo kuomba radhi, kisha leo Machi 7, 2026 ikawa zamu ya Obasogie aliyekutwa hana hatia baada ya uchunguzi wa awali kufanyika kwa mujibu wa klabu hiyo.