Polisi ilivyoweka kizuizi kongamano la siku ya wanawake Bawacha

Dar/mikoani. Vikwazo vimeendelea kuutawala mpango wa mkutano wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) wa kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, baada ya makundi ya makada wao kuzuiwa na Jeshi la Polisi kwa nyakati tofauti wakiwa safarini kuelekea kwenye mkutano huo uliopangwa kufanyika Musoma, mkoani Mara, kesho Jumapili, Machi 8, 2026.

Machi mosi, 2026, baraza hilo lilitangaza kwamba litaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani katika Kanda ya Serengeti, mkoani Mara, utakao wakutanisha wanawake wa chama hicho cha upinzani nchini.

Hata hivyo, leo Jumamosi, Machi 7, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo, ametangaza marufuku ya kufanyika kwa tukio hilo.

Katika tangazo lake, Kamanda Lutumo amesema Bawacha haitaruhusiwa kufanya tukio hilo kwa kuwa linakwenda kinyume na amri ya Mahakama iliyokitaka chama hicho kisimamishe kufanya shughuli za kisiasa hadi kesi yao ya msingi itakapomalizika mahakamani.

Hata hiyo, Bawacha kupitia Katibu Mkuu wake, Pamela Massay, imeeleza kuendelea na maandalizi, huku wanachama wake wakisafiri kutoka mikoa mbalimbali nchini kuelekea Musoma.

Alipozungumza na Mwananchi kwa simu leo, Massay amesema Jeshi la Polisi halina mamlaka ya kutoa tafsiri ya kimahakama na kujichukulia hatua zozote bila kupewa maelekezo na mhimili huo.

Wakati hali ikiwa hivyo, taarifa nyingine zilizoifikia Mwananchi zimedai Bawacha imezuiwa kutumia viwanja vya ‘Matumaini kwa Vijana’, vinavyomilikiwa na Kanisa Katoliki, kwa ajili ya maadhimisho hayo.

Inadaiwa kuwa uamuzi huo umefikiwa kutokana na sintofahamu iliyopo kati ya Bawacha na Polisi.

Mwananchi limezungumza na Mkurugenzi wa Kituo cha Matumaini kwa Vijana, Padri Michael Nyamhanga, ambaye amekiri kuandika barua ya kusitisha matumizi ya uwanja huo kwa shughuli hiyo kesho.

Padri Nyamhanga amesema awali walipokea barua kutoka Bawacha wakiomba kutumia viwanja hivyo kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa Machi 8 ya kila mwaka, ombi ambalo walilikubali.

Kwa mujibu wa Padri Nyamhanga, baadaye walipokea taarifa kutoka polisi ikiwataka kusitisha makubaliano hayo kutokana na sababu ambazo hakutaka kuziweka wazi.

“Ni kweli tumesitisha makubaliano ya awali kwa sababu tulipokea maelekezo kutoka polisi yakitutaka tusitishe. Hivyo, nimewaandikia barua (Bawacha), na wameipokea. Sasa mambo mengine mimi sijui, hayo yatakuwa ni baina ya Bawacha na polisi,” amesema.

Taarifa nyingine kutoka ndani ya Chadema, ambayo Mwananchi imeipata, inadai makundi ya makada wa chama hicho wamekamatwa na kuzuiwa wakiwa njiani kuelekea mkoani Mara ulikopangwa kufanyika mkutano huo.

Chanzo cha habari kinadai gari saba aina ya Toyota Coaster, zilizokodiwa na Bawacha Kanda ya Pwani, zimezuiwa maeneo ya Mlandizi na Gairo, mkoani Morogoro, zikiwa safarini kuelekea mkoani Mara.

Kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), John Heche, kila kona ya Tanzania wanawake wa Bawacha waliokuwa safarini wamekamatwa na kuzuiliwa na polisi.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi, Machi 7, 2026, Heche amesema: “Taarifa tulizonazo zinaonesha wanawake wa Bawacha karibu nchi nzima wamezuiliwa maeneo mbalimbali kuendelea na safari, ikiwamo hao wa Mlandizi, mkoani Pwani.

“Mlandizi kuna zaidi ya kinamama 100. Dakawa (Morogoro), kuna kinamama 100 wamezuiliwa. Geita, kinamama waliokuwa wakitoka Kagera wamezuiwa,” amesema Heche.

Wakati hayo yakiendelea, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama, amesema jeshi hilo limeyakamata magari madogo aina ya Toyota Coaster yaliyokuwa yakisafirisha abiria kwa masafa marefu kinyume cha taratibu.

Katika taarifa yake kwa umma, Kamanda Mkama amedai uchunguzi wa awali umebaini magari hayo yalikuwa yakiendeshwa bila kuzingatia sheria na taratibu za usalama barabarani.

“Uchunguzi zaidi unaendelea ili hatua stahiki za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika,” amesema Kamanda Mkama.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chadema Jimbo la Geita, Pasquina Lucas, amesema jumla ya viongozi na makada 60 wa Bawacha wanashikiliwa baada ya kukamatwa na polisi Machi 6, mkoani humo.

Mwananchi limemtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo, ambaye amesema kwa sasa hawezi kuzungumzia suala hilo, huku akiahidi kutoa taarifa kwa umma.

Mwananchi pia limemtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime, ambaye simu yake ilipoita alikata, akielekeza atumiwe ujumbe mfupi na hata alipotumiwa mpaka Mwananchi linaenda mtamboni, alikuwa hajajibu.