Mbeya. Kero ya miundombinu ya barabara iliyokuwa ikiwakabili wananchi wilayani Kyela mkoani Mbeya, huenda ikabaki historia baada ya Halmashauri hiyo kununua mitambo minne ya kisasa kwa ajili ya kukabiliana na changamoto hiyo kwa jamii.
Mara kadhaa wananchi wilayani humo walikuwa wakiripoti kukumbwa na mafuriko kufuatia mitaro na mifereji kutiririsha maji na kusababisha kero kwenye makazi haswa wakati wa mvua.
Hata hivyo, kupitia mapato ya ndani Halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha 2024/25 kwa asilimia 129 imefanikiwa kununua mitambo minne ikiwa ni greda, Scaveta, Lobed na Compacta zilizogharimu zaidi ya Sh 1.49 bilioni.
Akizungumza leo Jumamosi Machi 7, 2026 wakati wa uzinduzi wa mitambo hiyo, Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo, Florah Luhala amesema matarajio yao ni kuona kero ya barabara zikiwamo za mtaani kufikiwa kwa ujenzi.
Amesema mbali na mitambo hiyo kuwa makusudi kwa ujenzi wa barabara, lakini itatumika pia chanzo cha mapato kwenye Halmashauri pale itakapokuwa ikikodishwa kwa wadau mbalimbali.
“Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha mifumo rafiki ya ukusanyaji mapato, ambapo leo Kyela tunaona manufaa yake kwa kununua mitambo ili kurahisisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi”
“Kero ya barabara ni kubwa hapa Kyela hivyo mitambo hii itakuwa suluhisho kwakuwa inafika maeneo ya pembezoni, fedha hizi ni makusanyo ya ndani baada ya mwaka wa fedha 2024/25 kukusanya asilimia 129, hivyo ile baki tukanunua hii mitambo” amesema Florah.
Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Josephine Manase amempongeza mkurugenzi huyo kwa usimamizi na matumizi bora ya fedha, akieleza kuwa serikali inahitaji kuona wananchi wakinufaika na kodi zao kwa kupelekewa maendeleo.
“Tunatamani kuona barabara zetu hapa Kyela zinakuwa nzuri ili kurahisisha wananchi wanafanya shughuli zao za kiuchumi, tunaamini kwa bejeti za Tarura na Tanroad tutafikia malengo, tusimamie na kutunza vyema mitambo hii” amesema Josephine.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Mpinduzi Wilaya hiyo, Elias Mwanjala amesema mitambo hiyo ni historia kwa viongozi wote kwani haikuwahi kutokea, akiwashukuru baraza la madiwani kwa kupitisha bajeti hiyo.
“Rais amefanya makubwa kwa Wilaya yetu, leo tunaona mitambo hii lakini gari la kisasa la Zimamoto, lakini baadaye tutapokea tena gari nyingine, niwapongeze kwa kazi nzuri kwa kuiheshimisha Kyela” amesema Mwanjala.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Thobias Mwankona amesema ujio wa vifaa hivyo ni utekelezaji wa azma ya serikali ya Mkoa kushauri kila Wilaya kuwa na kifaa japo kimoja cha kazi, lakini Wilaya hiyo imeenda mbali zaidi kwa kununua vifaa vitatu.
“Kwa maana hiyo zile barabara korofi zitafanyiwa kazi kwa ufasaha, lakini hii mitambo itatumika kama chanzo cha mapato kwa kukodisha ili iweze kujiendesha na tutahakikisha tunailinda ibaki salama muda wote” amesema Mwankona.
Mmoja wa wananchi walioshuhudia uzinduzi wa mitambo hiyo, Zainab Yassin ameshauri vifaa hivyo kutumika kwa malengo husika, akiupongeza uongozi wa Halmashauri hiiyo kwa kusikia kilio cha wananchi.
“Tunamshukuru na kumpongeza Mkurugenzi kwa kazi nzuri, kilio chetu cha barabara huenda ikabaki historia kwakuwa tulipewa ahadi muda mrefu lakini leo tumeshuhudia mitambo imefika” amesema Zainab.