Serengeti. Wakati Serikali ikiendelea kuchukua hatua za kukabiliana na athari za mvua zinazoendelea kunyesha, waongoza watalii wametakiwa kuchukua tahadhari wanazopewa na vikosi vya uokozi katika maeneo korofi katika Hifadhi ya Taifa Serengeti.
Mamkala ya hifadhi hiyo imesema itaendelea kuhakikisha shughuli za utalii zinaendelea kama kawaida huku usalama wa watumiaji wa barabara, wakiwemo watalii, wanaowaongoza na watumiaji wengine ukiwa wa kutosha.
Hayo yamesemwa leo Jumamosi Machi 7, 2026 na Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Kitengo cha Mawasiliano, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (Tanapa), Catherine Mbena akizungumza na baadhi ya waongoza watalii katika eneo la Kivuko cha Viboko vya Nabi, baada ya kufanya ukaguzi na kuangalia hatua zinazoendelea kuchukuliwa.
Amesema wanaendelea kuhakikisha shughuli za utalii zinaendelea kama kawaida, kwani watalii wametoka mbali kuja kufurahia maeneo haya ya utalii.
Mbena amesema wamefika katika eneo hilo si tu kuangalia hali ilivyo bali pia kuwasikiliza na kuchukua hatua, ambapo kwa sasa timu za waokozi zilizopo katika maeneo korofi mbali na kuelekeza magari, zinachukua hatua nyingine kama kuweka mawe kwenye mashimo ili magari yaweze kupita bila kukwama.
“Tambueni mnabeba wageni ambao wakiondoka wanaondoka na neno zuri au baya kuhusu nchi yetu. Tumeona video mnazosambaza wenyewe; watu wanavuka, kuna madereva ambao ni wazoefu na kuna madereva wageni. Niwaombe tutumie hizi barabara kwa busara. Najua ni wazoefu sana wa barabara hizi, tusikilizie timu za uokozi ziko hapa,” amesema.
“Kivuko hiki cha Viboko vya Nabi kinaendelea kurekebishwa na kuna maeneo yamechimbwa na mvua nyingi. Kinachofanyika ni kuweka mawe kuhakikisha safari zinaendelea. Tumekuwepo hapa leo siku ya nne kuhakikisha hakuna anayeshindwa kuendelea na ratiba zake, ziwe za utalii, uhifadhi au binafsi,” amesema.
“Shughuli za utalii zinaendelea kama kawaida, ila panapokuwa na maji mengi tunachofanya ni kuwaelekeza wapi wapite, kwani haijulikani barabara ni ipi. Lakini watu wetu wenye uzoefu wanawaelekeza na safari zimeendelea kama kawaida,” amesema.
Hata hivyo, ameonya maji yasipimwe kwa macho.
“Usipime maji kwa macho, sikiliza timu ya uokozi iliyopo hapa ikuongoze namna gani unaweza kupita hapa na kuendelea na safari. Na kama maji yamejaa usiwe na haraka kuliko usalama wako,” amesema.
Kwa upande wao baadhi ya madereva hao waliomba Serikali iharakishe ukarabati wa miundombinu hiyo.
“Kivuko tumepigia kelele miaka yote wanasema watarekebisha, hatuoni kinachoendelea. Kila mwaka maji yanapita; tulipendekeza pajengwe daraja la juu ili watu wavuke. Tunaomba kivuko hiki na vingine vinavyofuata vitengenezwe,” amesema Wilfred Laizer.
Naye Joseph Wilson ameomba Tanapa itafute njia mbadala zitakazotumika pindi kunapokuwa na changamoto.
Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waongoza Watalii Tanzania (Tato), Elirehema Maturo, ameomba Serikali ihakikishe inaboresha miundombinu ya barabara ambayo imekuwa kilio cha muda mrefu.
Amesema wao kama chama wanaendelea kupeana mrejesho ili waongoza watalii wachukue tahadhari.
“Sisi malalamiko yetu kama chama ni kwamba maeneo hayo korofi miaka nenda rudi yana changamoto hiyo. Tanapa waweke madaraja; hata ukiamua kujenga daraja moja kwa mwaka kwa miaka 10 tungemaliza. Maeneo korofi yakirekebishwa itaondoa adha hii,” amesema.
Awali Mkuu wa Hifadhi ya Serengeti, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Ismail Omar, ametaja maeneo matatu korofi kuwa ni Bwawa la Viboko vya Nabi, Mto Mokasi na Bwawa la Bona.