Naibu Waziri akabidhi viti mwendo 10 Manyara

Babati. Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege, amekabidhi viti mwendo kwa watu wenye mahitaji maalumu katika Wilaya ya Babati, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuwasaidia watu wenye ulemavu wa viungo kupata unafuu katika maisha yao ya kila siku.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi, Machi 7, 2026, Ndege amesema amekuwa na utamaduni wa kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu kila anapopata fursa, hususan watoto na watu wazima wenye changamoto za ulemavu wa viungo.

Ndege, ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu mkoa wa Manyara, amesema lengo ni kupunguza ugumu wa maisha yao na kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.

“Watu hawa ni ndugu zetu, ni jamaa zetu, ni Watanzania wenzetu. Tunapowaunga mkono kwa kuwapatia viti mwendo hivi, tunakuwa tumewasaidia kuwavusha mahali walipo na kuwasogeza mbali zaidi,” amesema Ndege.

Ametoa wito kwa watu wenye uwezo katika jamii kuendelea kuwakumbuka na kuwasaidia watu wenye mahitaji maalumu, kwani hawatapungukiwa na kitu pindi wakisaidia jamii yenye uhitaji.

Hata hivyo, amewataka walionufaika na viti mwendo hivyo kuvitunza ipasavyo ili viwasaidie kwa muda mrefu zaidi katika shughuli zao wanazozifanya kila siku.

“Hatua hii pia ni sehemu ya kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuwatetea na kuwasaidia watu wenye mahitaji maalum nchini,” amesema Ndege.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake (UWT) Wilaya ya Babati Mjini, Eva Luoga, amemshukuru naibu waziri huyo kwa moyo wake wa kujitoa na kuwasaidia wananchi wenye mahitaji maalumu.

Luoga amesema, kutoa ni moyo na siyo utajiri, pia Naibu Waziri Ndege amekuwa akiwajali na kuwashika mkono wananchi wa Babati kwa muda mrefu bila kuwatelekeza.

“Wanawake wa mkoa wa Manyara, hususan wa Babati Mjini, bado wanaendelea kuona matunda ya uongozi wako, na hawakufanya kosa kumchagua kwa kuwa mchango wake kwa jamii unaonekana wazi wazi,” amesema Luoga.

Mmoja wa walionufaika na msaada huo wa viti mwendo, Seleman Ally, amemshukuru Naibu Waziri Ndege na Rais Samia kwa kuendelea kuwajali na kuwathamini watu wenye mahitaji maalumu katika jamii.

Ally amesema Naibu Waziri amefanya jambo jema kwa wenye mahitaji maalumu, hasa kipindi hiki cha mwezi wa Ramadhan kwa Waislamu na Kwaresma kwa Wakristo.