Vijana 308 wapewa Sh7 bilioni kutekeleza miradi ya uvuvi

Mwanza. Vijana 308 waliohitimu mafunzo ya programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT-Uvuvi) wamekabidhiwa Sh7 bilioni kwa ajili ya kuwawezesha kutekeleza miradi ya ufugaji wa samaki kwa vizimba, ufugaji wa jongoo bahari, kilimo cha mwani pamoja na unenepeshaji wa kaa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kukabiliana na changamoto ya ajira.

Akikabidhi hundi ya fedha hiyo leo Machi 7, 2026, kwenye hafla iliyofanyika Chuo cha Wakala wa Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (Feta), Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amesema fedha hizo ni sehemu ya Sh200 bilioni iliyoahidiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ili kuwezesha makundi mbalimbali kupata mitaji ya shuguli za kiuchumi.

Nanauka amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imepokea Sh30 bilioni kati ya Sh200 bilioni zilizoahidiwa na Rais, huku sehemu ya fedha hizo ikitumika kuwezesha utekelezaji wa programu mbalimbali za kuwawezesha vijana kiuchumi, ikiwemo programu ya BBT katika sekta ya uvuvi.

Amesema uwezeshaji huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuwasaidia vijana kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa, huku akibainisha kuwa idadi kubwa ya vijana nchini inaendelea kuhitimu mafunzo kila mwaka, lakini fursa za ajira rasmi ni chache.

Kwa mujibu wa Nanauka, vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 nchini wanakadiriwa kufikia milioni 20.6, sawa na asilimia 34.4 ya idadi ya watu wote, huku takribani vijana milioni moja wakihitimu mafunzo mbalimbali kila mwaka, lakini ni vijana 40,000 pekee wanaopata ajira katika sekta ya umma na wengine 350,000 sekta binafsi.

Kutokana na hali hiyo, amesema Serikali imeamua kuimarisha programu mbalimbali za kuwawezesha vijana kiuchumi ili waweze kujiajiri na pia kutengeneza ajira kwa wengine.

“Fedha hizi tunazozikabidhi leo ni mikopo yenye masharti nafuu, ambayo inalenga kuwawezesha vijana waliopata mafunzo kwa vitendo kuanza kutekeleza miradi waliyoibuni wenyewe. Hii ni sehemu ya utekelezaji wa ahadi ya Rais ya kuwezesha vijana kiuchumi,” amesema Nanauka.

Ameongeza kuwa vijana watakaonufaika na mpango huo wanapaswa kutumia fursa hiyo vizuri, kwa kuwa fedha hizo ni mikopo inayotakiwa kurejeshwa ili kutoa nafasi kwa vijana wengine kunufaika na mpango huo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Meena, amesema programu ya BBT Uvuvi ilianzishwa mwaka 2022/23 kufuatia maelekezo ya Rais Samia ya kuanzishwa kwa programu maalum za kuwawezesha vijana kiuchumi.

Meena amesema utekelezaji wa programu hiyo unahusisha hatua tatu: mafunzo ya kubadili mtazamo wa vijana kuhusu ajira, mafunzo kwa vitendo kupitia mfumo wa atamizi, pamoja na uwezeshaji wa mitaji ili vijana waweze kuanzisha miradi waliyoibuni.

Amesema katika awamu za mafunzo zilizotekelezwa, jumla ya vijana 500 walidahiliwa, ambapo kati yao vijana 486 walifanikiwa kuhitimu mafunzo ya vitendo yaliyofanyika katika vituo 15 vya ukuzaji viumbe maji vya Serikali na watu binafsi kwa kipindi cha miezi mitatu.

“Katika mwaka wa fedha 2025/26, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetoa Sh7 bilioni kwa ajili ya kuwawezesha vijana wa BBT waliopata mafunzo kwa vitendo kupata mitaji ya kutekeleza miradi waliyoibuni,” amesema Meena.

Amefafanua kuwa kati ya vijana 308 watakaonufaika na fedha hizo, vijana 160 wataendesha miradi ya ufugaji wa samaki kwa vizimba katika mikoa ya Mwanza, Mara na Kagera, huku vijana 148 wakitekeleza miradi ya ufugaji wa jongoo bahari, kilimo cha mwani na unenepeshaji wa kaa katika ukanda wa pwani, hususan mikoa ya Pwani na Mtwara.

Aidha, amesema wizara inapanga kutumia sehemu ya Sh23 bilioni zilizosalia kati ya fedha ilizopokea ili kuendelea kuwawezesha vijana wengine waliobaki kati ya waliopata mafunzo ya BBT, hatua inayolenga kuhakikisha vijana wengi zaidi wanapata mitaji ya kuanzisha miradi yao na kuchangia kukuza uchumi wa sekta ya uvuvi nchini.

Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Ng’wasi Kamani, amewataka vijana wachangamkie fursa za mikopo nafuu, ikiwemo kuomba na kuwasilisha mawazo ya miradi serikalini matangazo yanapotolewa.

Awali, akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, amewataka vijana waliokabidhiwa fedha hizo kuwa waaminifu na kuzirejesha, akieleza kuwa zaidi ya Sh3 bilioni hazijarejeshwa wilayani humo na vijana waliokopa.

Katika mradi huo, Feta itasimamia shughuli zote kwa vijana hao, ikiwa ni pamoja na kusambaza pembejeo kama vile vifaranga vya samaki, vya jongoo bahari, mbegu za mwani, uwekaji wa miundombinu vikiwemo vizimba, pamoja na kufanya ufuatiliaji, tathmini na uwajibikaji wa vikundi vya vijana hao.