Tabora. Wanafunzi zaidi ya 15 wa Chuo cha Ardhi kilichopo Kata ya Cheyo, Manispaa ya Tabora mkoani Tabora, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Tabora kwa tuhuma za kumfanyia vurugu mlinzi, kwa kumpiga na kumng’oa meno manne, wakimtuhumu kuwazuia kutoka na kuingia chuo kwa muda wanaotaka.
Akizungumza chuoni hapo leo, Machi 7, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, ameagiza chuo hicho kuwafukuza wanafunzi hao mara moja.
“Mkuu wa chuo nikupongeze kwa hatua mlizochukua, lakini pia hakikisha kwa kufuata sheria na taratibu za chuo, fukuza hawa watu maana hatuwezi kufuga wahalifu hapa,” amesema Chacha.
Amesema wanafunzi hao wamekuwa wakishiriki matukio tofauti ya kihalifu chuoni hapo, ikiwemo ulevi, kurudi chuoni usiku wa manane, na kutishia wenzao kwa visu ili wawafungulie mlango, vitendo ambavyo havikubaliki kwa mwanafunzi yeyote.
Amesisitiza kwamba wanafunzi hao watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili, hivyo watahudhuria kesi yao wakiwa wanatokea majumbani mwao, na si chuoni.
Mkuu wa Chuo cha Ardhi Tabora, Jeremiah Minja, ameeleza namna vurugu zilivyoibuka, kwamba Machi 2, wanafunzi hao walienda kuwafanyia mahojiano walinzi wakidai wanaibiwa nguo zao, lakini walinzi wakakanusha tuhuma hizo na kusema jukumu lao ni kulinda chuo na vilivyomo, ikiwemo wanafunzi, lakini sio kuchukua mavazi.
Saa mbili usiku, baadhi ya wanafunzi hao wakaenda kupita sehemu ambayo hairuhusiwi, ili watoke nje ya chuo na baada ya kukamatwa na kuhojiwa na mlinzi, hawakutaka kuonesha ushirikiano na badala yake, wakaanza kupiga kelele huku wakimshambulia mlinzi na kumng’oa jino moja.
Hapo ndipo viongozi wa chuo pamoja na baadhi ya watumishi wanaoishi chuoni walidhibiti ugomvi na kurudisha hali ya usalama chuoni.
Mkuu huyo amesema usiku huo huo, wakajiunga tena, wanafunzi hao wakaenda getini kwa mlinzi na kusababisha vurugu, wakimshambulia kwa kumpiga sehemu mbalimbali mwilini na wakamng’oa tena meno matatu, hivyo jumla ya meno manne kumeng’olewa.
Baada ya hapo, viongozi walidhibiti tena ugomvi, na kwa sababu mlinzi alikua amejeruhiwa, akakimbizwa hospitali kwa ajili ya matibabu.
“Wanafunzi hawa, kutokana na vurugu, nilimpigia simu mkuu wa wilaya, na nashukuru polisi wakaja kwa haraka, na tayari tulikua tumeshajua wanafunzi walioshiriki vurugu, wakakamatwa na kupelekwa kituoni,” amesema Minja.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, amewahimiza wanachuo hao kuhakikisha wanazingatia lengo la wao kuwepo chuoni, badala ya kujiunga na makundi yasiyofaa ya mitaani na hatimaye kufanya matendo yasiyofaa.
“Wadogo zangu, someni, wazazi na walezi wenu nyumbani wakijua nyie mpo kwenye masomo, matokeo yake nyie mnafanya vurugu na kuharibu ndoto zetu,” anasema Wella.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa Chuo cha Ardhi, Jackson Mchele, amesema haungi mkono uvunjifu wa sheria za chuo na kwamba wanafunzi hao wawajibishwe, ili iwe fundisho kwa wengine.
“Hata wakati nagombea nafasi hii, niliwaambia kwamba miongoni mwa mambo nitakayosimamia ni pamoja na nidhamu chuoni,” anasema Mchele.