Kituo cha taarifa mwarobaini kero za wananchi Mbarali

Mbarali. Wananchi wa Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya wameeleza matumaini yao baada ya Serikali kufungua Kituo cha Taarifa (Call centre), wakisema kitawasaidia kupunguza gharama za kusafiri umbali mrefu kuwasilisha kero na kupata ufumbuzi.

Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti leo Jumamosi, Machi 7, 2026, katika Kata ya Igurusi, wamesema ujio wa mfumo huo utasaidia kuokoa muda na kujikita katika shughuli za kiuchumi, hususan sekta ya kilimo.

“Miaka yote Wilaya ya Mbarali kungekuwa na utaratibu wa uwasilishaji wa kero kupitia simu za mkononi, kusingekuwa na migogoro ya mara kwa mara. Tuna kila sababu ya kushukuru uongozi wa halmashauri kwa hatua hiyo kubwa,” amesema Isaya Maduhu.

Maduhu amesema awali, kabla ya uwepo wa kituo hicho, wananchi walikuwa wakilazimika kusafiri umbali wa kilometa zaidi ya 70 kufika makao makuu ya wilaya au halmashauri kuwasilisha na kutatuliwa kero zao.

“Kwa sasa changamoto zote ni kwenye simu tu. Unapiga bure na kutoa taarifa ya changamoto kwa wakuu wa idara husika, na baada ya muda unapata majibu kupitia simu ya mlengwa husika,” amesema.

Naye mkulima na mkazi wa Kata ya Kongoro, Mswisi, Tina Amos amesema kimsingi wana kila sababu ya kuishukuru Serikali kwa kuja na utaratibu huo ambao kwa sasa umewatoa gizani na kuwasaidia kuondokana na urasimu kwa baadhi ya watendaji wa halmashauri.

“Jiografia ya wilaya ya Mbarali asilimia kubwa ni maeneo ya uwekezaji, sasa ukiwa na changamoto inayokulazimu kufika ofisi za halmashauri kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa suala lolote, unajikuta ukitumia gharama kubwa za usafiri na wakati mwingine unafika suala lako likakosa ufumbuzi papo kwa papo,” amesema.

Amesema ujio wa kituo hicho kimerahisisha ufumbuzi wa changamoto za wananchi na kuongeza weledi wa utendaji kazi kwa watumishi wa Serikali.

Awali, akizungumzia uanzishwaji wa kituo cha kupokea taarifa za kero za wananchi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbarali, Raymond Mweli, amesema lengo ni kuokoa muda wa wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma, jambo ambalo linakwamisha shughuli za kiuchumi na matumizi mabaya ya rasilimali fedha.

Mweli ametaja sababu nyingine ni kuondoa ukiritimba na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi kwa watumishi wa Serikali kwa kupokea na kutatua changamoto za wananchi kwa wakati kupitia kituo hicho maarufu kama ‘Call centre’.

“Ni mikakati ya Serikali kuona namna bora ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi, ambapo kati ya halmashauri saba za mkoa wa Mbeya, Mbarali ndiyo ya kwanza kuanza utekelezaji wa uwepo wa kituo cha ‘Call Centre’. Lengo ni kupunguza adha kwa wananchi kutembea umbali mrefu kufuata huduma kwenye makao makuu ya wilaya na halmashauri husika,” amesema.

Amesema utaratibu huo umeleta matokeo makubwa kwa wananchi kupiga simu kuwasilisha kero kutoka maeneo yao, hususani vijijini, na hivyo kusaidia wakuu wa idara husika kuyafanyia kazi kupitia ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji.

Mweli amesema katika kutatua kero za wananchi, halmashauri imedhamiria kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora ili kuondoa urasimu, sambamba na kufanya ziara za kukagua miradi ya sekta zote na kufanya mikutano ya hadhara.

“Kupitia kituo cha taarifa tutakuwa na kitabu maalumu cha kuweka kumbukumbu za orodha za kero zilizowasilishwa na wananchi kwa kila wiki, siku hadi mwezi, ili kubaini zilizo tatuliwa na idara husika ngazi ya halmashauri,” amesema.

Mweli amesema ili kuhakikisha wanafikia malengo ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi, halmashauri imeweka utaratibu wa kituo hicho kusimamiwa na idara ya utawala kwa kuweka kumbukumbu za kero zilizowasilishwa na kutatuliwa kwa siku husika.

Katika hatua nyingine, Mweli amewataka wananchi wenye kero Mbarali kuwasiliana na watoa huduma katika kituo hicho kwa kupiga namba 0736600075 au 0799600075 bure ili kupata ufumbuzi na kupata mrejesho ndani ya muda mfupi.