Unguja. Huenda mwarobaini wa kata, washa ya umeme, ikapatikana baada ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuwekeza Sh800 bilioni katika miundombinu hiyo.
Zanzibar inapokea umeme kupitia waya za baharini kutoka Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco). Kwa upande wa Unguja, zipo waya mbili, moja ya megawati 45 iliyowekwa mwaka 1980 na imeshatumika hadi kufikia asilimia 98.8, na pili ya megawati 100 imeshatumika asilimia 97.3, ambapo waya zote zimeshafikia ukomo wa uwezo wa kusafirisha umeme.
Kwa sasa, Zanzibar ina kiasi cha umeme cha megawati 135 na upungufu wa megawati 65.
Akizungumza na Mwananchi, leo Machi 7, 2026, Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Nadir Abdullatif, amesema kwa sasa wizara hiyo kupitia Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco imeingia mikataba na kampuni mbalimbali kwa lengo la kuboresha miundombinu ya umeme.
Amefafanua kuwa wizara imefanikiwa kusaini mkataba na kampuni ya Elecmech Switchgears ya Dubai ya kubadilisha laini za umeme kilomita 1,000, yenye thamani ya dola za Marekani 159 milioni, sawa na Sh411 bilioni.
“Umeme wa uhakika uliopo Zanzibar ni megawati 135, na kilichoongezeka ni megawati 65. Miradi iliyopo imechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko hilo,” amesema.
Amesema wakati wakisubiri miradi hiyo kukamilika, Zanzibar imeshapokea transfoma nne zenye uzito wa tani 105, ambapo mbili zimewekwa Mkoa wa Kusini Unguja na mbili zimewekwa Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Ameeleza kuwa kukamilika kwa miradi hiyo mwaka 2028 kutakuwa na uhitaji wa megawati 100 ili nchi iwe salama.
Amefafanua kuwa Zanzibar inatumia umeme kutoka Tanzania Bara, ambapo kuna megawati 100 za waya chini ya bahari, waya wa megawati 45 kutoka Tanzania hadi Unguja, na waya wa megawati 20 kutoka Tanga hadi Pemba.
Amesema kutokana na waya hizo kutumika kwa muda mrefu, hazitakuwa na uwezo wa kusafirisha umeme megawati hizo kama ilivyokuwa awali.
“Kukatika kwa umeme hakusababishwi na miundombinu chakavu peke yake, bali wakati mwingine kutokana na kuzidiwa kwa matumizi katika miradi inayoendelea kujengwa.”
Waziri Nadir amesema Serikali imefanya jitihada mbalimbali katika kukabiliana na changamoto hiyo, ikiwemo kukarabati jenereta 30 zilizopo katika Kituo cha Umeme Mtoni, Unguja.
Pia, amesema wizara imeleta meli ya umeme wa muda, kwa lengo la kutoa umeme katika kipindi cha miezi nane hadi mwaka mmoja, huku wakisubiri vifaa vifungwe ili waindoshe, kwani ina gharama kubwa.
Amesema meli hiyo itatoa megawati 40, huku jenereta zikitoa umeme wa megawati 16, na zote zitakuwa salama kwa kipindi cha mpito.
Hivyo, amewaomba wananchi kuendelea kuwa na subira, kwani Serikali ina njia mbadala ya kutatua changamoto hiyo.
Ameeleza wizara inatambua changamoto zinazowakabili wananchi katika suala la umeme na Serikali imeingia makubaliano na mikataba mikubwa; tatizo hilo linatarajiwa kumalizika ifikapo mwaka 2028.
Mbali na hilo, Nadir amesema Serikali inatambua kuwa baadhi ya watendaji waliondoshwa au kufukuzwa Zeco wanafanya hujuma katika kukata umeme kwa baadhi ya maeneo. Waziri huyo ametoa onyo kwa wananchi hao kuacha mara moja tabia hiyo, na atakaebainika atachukuliwa hatua za kisheria na atakuwa mfano kwa wengine.
Amesema Serikali inafanya yote hayo kwa ajili ya kujitegemea katika suala la umeme na haitaki kuwa tegemezi kama ilivyo sasa.
Naye, Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Seif Kombo Pandu, amesema Serikali ina mpango wa kulaza waya wenye megawati 270 kupitia bahari.
Amesema miongoni mwa changamoto zinazouikuta Serikali ni usafirishaji kupitia msongo wa 133, na transfoma zilizoletwa zitaondosha changamoto hiyo.
Hivyo, Serikali imesema kata ya washa ya umeme inatarajiwa kumalizika ifikapo mwaka 2028, kabla ya Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, kumaliza awamu yake ya pili.
Asma Mbaraka Hashim amesema shirika la umeme linavyotoa umeme katika kipindi hiki, wanapaswa kuwaambia wananchi wanafanya mgao ili waandae mazingira ya kuandaa vitu vyao vizuri.