Tanga. Wataalamu wa ardhi mkoani Tanga wamefanikiwa kusikiliza jumla ya migogoro 49 ya ardhi ndani ya siku sita tangu kuanza kwa programu ya Samia Ardhi Kliniki, iliyofanyika kwa siku sita kama sehemu ya kuadhimisha wiki ya mwanamke duniani inayoadhimishwa kila mwaka.
Katika kipindi hicho, kuanzia Machi 2 hadi 7, 2026, migogoro 37 imepatiwa ufumbuzi, huku wananchi 97 wakikabidhiwa hati 97 za kumiliki ardhi.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Machi 7, 2026, Msajili Msaidizi wa Hati katika Mkoa wa Tanga, Mwajuma Kihiyo, amesema kliniki hiyo imeandaliwa na Wizara ya Ardhi kupitia Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya wanawake duniani.
Kihiyo amesema lengo la kliniki hiyo lilikuwa kusikiliza na kutatua kero za wananchi, hasa wanawake, zinazohusiana na migogoro ya ardhi, pamoja na kutoa elimu ya masuala ya ardhi, kukabidhi hati za umiliki na kukusanya mapato ya Serikali kupitia malipo ya kodi mbalimbali.
Amesema zoezi hilo limekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi na watumishi wa umma.
“Kliniki hii imetusaidia sisi kama watumishi wa umma kuwahudumia wananchi wengi kwa wakati mmoja. Hadi siku ya mwisho tumewahudumia wananchi 607, ambapo kati yao 343 ni wanawake ambao wamepata huduma walizokusudia,” amesema Kihiyo.
Amefafanua kuwa kati ya migogoro 49 iliyopokelewa, migogoro 37 ilitatuliwa kiutawala kwa kuwasuluhisha pande zote husika, huku migogoro iliyoshindikana kufikiwa muafaka wamiliki wake wakishauriwa kufuata taratibu za kisheria katika vyombo husika.
Aidha, amesema baadhi ya wananchi waliofika walikuwa wakileta malalamiko kuhusu migogoro ambayo ilikuwa imeshatolewa maamuzi ama kiutawala au kisheria.
Kuhusu utoaji wa hati, Kihiyo amesema jumla ya hati 97 zimetolewa kwa wananchi waliokuwa wameanza taratibu za umilikishaji wa ardhi.
Ameeleza kuwa katika baadhi ya kesi wananchi walipelekwa hadi katika maeneo yao kwa ajili ya ukaguzi wa viwanja, kuanzisha hati za miamala na kukamilisha hatua za mwisho za umilikishaji.
“Kwa wale waliokuwa wameanza taratibu na kulipia gharama husika, tuliwasaidia kukamilisha mchakato kwa haraka. Hadi sasa wananchi 97 wamepatiwa hati zao,” amesema.
Kihiyo ameongeza kuwa baada ya kumalizika kwa kliniki hiyo, wananchi wanaendelea kushauriwa kufuata utaratibu wa kawaida wa kupata huduma za ardhi katika ofisi za ardhi za halmashauri na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa, muda wa kazi.
Amesema mfumo wa kliniki umeleta urahisi mkubwa kwa wananchi kwa kuwa wataalamu wote wa sekta ya ardhi walikusanyika eneo moja, jambo lililowezesha wananchi kupata huduma zote kwa wakati mmoja badala ya kuzunguka katika ofisi mbalimbali.
“Katika kliniki hii wananchi walipata huduma zote sehemu moja. Kulikuwa na wapima ardhi, maafisa mipango miji na wataalamu wengine wote wa ardhi, hivyo mchakato wa kupata huduma ulikuwa rahisi zaidi,” amesema.
Changamoto zilizojitokeza
Kihiyo amesema changamoto kubwa waliyokutana nayo ni baadhi ya wananchi kutoridhika na maamuzi yaliyotolewa na vyombo vya kisheria na hivyo kuendelea kutafuta ushauri kuhusu migogoro ambayo tayari imeamuliwa.
Amesema mara nyingi hatua inayopaswa kuchukuliwa baada ya kutoridhika na uamuzi ni kukata rufaa katika ngazi zinazotambuliwa kisheria.
Aidha, amesema migogoro mingi iliyowasilishwa ilihusiana na masuala ya mirathi, na baadhi ya wananchi hutaka kumiliki ardhi iliyorithiwa bila kukamilisha taratibu za kisheria za mirathi.
“Pia tumekutana na migogoro ya kifamilia inayotokana na kugombea maeneo yaliyoachwa na marehemu,” amesema.
Changamoto nyingine ni baadhi ya wananchi kukaa na nyaraka za upimaji wa ardhi bila kukamilisha mchakato wa kupata hati za umiliki.
Amesema katika maeneo mengi ya Tanga ardhi tayari imepangwa na kupimwa kupitia upimaji shirikishi au urasimishaji, lakini baadhi ya wananchi hawajitokezi kukamilisha taratibu za umilikishaji.
“Ninatoa wito kwa wananchi ambao maeneo yao tayari yamepimwa kuhakikisha wanakamilisha taratibu zote za umilikishaji ili kupata hati za ardhi,” amesema.
Baadhi ya wanawake waliohudumiwa katika kliniki hiyo wamesema huduma hiyo imewasaidia kupata haki zao za umiliki wa ardhi kwa haraka.
Mkazi wa Donge jijini Tanga, Sophia Shundi, amesema amefanikiwa kupata hati ya umiliki wa kiwanja chake kupitia kliniki hiyo, mali ambayo ameipata kupitia shughuli zake za ujasiriamali.
“Hati hii itanisaidia kuhakikisha watoto wangu wanaendelea kumiliki eneo hili hata nitakapokuwa sina uwezo au nitakapofariki. Huduma hii imetupunguzia usumbufu wa kuzunguka ofisi mbalimbali,” amesema.
Naye Amina Juma, mkazi wa Donge, amesema alikuwa ameshaanza mchakato wa kupata hati ya kiwanja chake kwa muda mrefu bila mafanikio, lakini kupitia kliniki hiyo ameona mwanga wa kukamilisha taratibu zake.
“Nina viwanja viwili na natamani kupata hati zake. Mchakato wa kimoja unaendelea vizuri hapa kliniki na ninatarajia kukamilisha taratibu zote za umilikishaji,” amesema.
Kwa upande wake, Majabu Mohamed amependekeza zoezi hilo liendelee kufanyika kila mwaka wakati wa maadhimisho ya wiki ya wanawake duniani ili kuwapa wanawake wengi zaidi fursa ya kupata hati za umiliki na msaada wa kisheria katika migogoro ya ardhi.
“Ubunifu huu uendelee kila mwaka ili wanawake wengi wapate nafasi ya kupata haki zao za ardhi na ushauri wa kisheria,” amesema.