WAKATI kesho Machi 8 ni Siku ya Wanawake Duniani, waasisi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), wamekutana na kukumbushia safari ya mafanikio ya chama hicho na kuhamasisha kizazi kipya cha wanahabari wanawake kuendelea kupambana.
Waasisi hao walikutana katika tukio maalum la futari lililofanyika jana Ijumaa Machi 6, 2026 kwenye ukumbi wa TAMWA uliopo Sinza Mori jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo ulifanyika sambamba na maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani huku ukiambatana na kaulimbiu ya mwaka huu ‘Give to Gain’, ambapo waasisi wa TAMWA walipata nafasi ya kusimulia historia ya chama hicho na mafanikio yake katika kuibua masuala mbalimbali ya kijamii kupitia vyombo vya habari.
Mmoja wa waasisi wa TAMWA, Dk Gladness Munuo, amesema chama hicho kilianza kama jukwaa la wanahabari wanawake kuunganisha nguvu ili kuzungumzia changamoto zinazowakabili wanawake na watoto katika jamii.
“Mara nyingi tulikuwa tunakutana na migogoro au changamoto mbalimbali kwenye jamii, lakini tuliamini katika usuluhishi na majadiliano mezani. Kituo cha usuluhishi kilikuwepo, ingawa mara nyingi tulimaliza matatizo kwa mazungumzo,” amesema Dk Munuo.
Kwa upande wake Judica Losai, amesema kujiunga na TAMWA kulimfungulia milango mingi ya mafanikio, ikiwemo kupata nafasi ya kwenda kusoma nchini Sweden kupitia fursa alizozipata ndani ya chama hicho.
“Safari yangu ya kwenda Sweden ilitokana na TAMWA. Nimejifunza mengi hapa na hata sasa nimekuwa mstaafu, lakini bado TAMWA inatubeba sisi sote, waasisi na wanachama wa zamani,” amesema Losai.
Kwa upande wake Fatma Aloo, alikumbuka namna TAMWA ilivyokuwa mstari wa mbele kuibua masuala nyeti ya kijamii, ikiwemo kupaza sauti dhidi ya ukatili wa kijinsia na dhuluma kwa wanawake.
“Kulikuwa na masuala mengi ambayo hayazungumzwi hadharani, ikiwemo kupigwa kwa wanawake. TAMWA ilisimama imara kuhakikisha sauti za wanawake zinasikika,” amesema Fatma na kuongeza.
“Wakati tumeanza pia waume zetu walikuwa wakitusapoti na hiyo ilitutia nguvu zaidi kwani wanaume wa kitanzania ni wastaarabu sana.”
Naye Rose Rueben, amewahimiza wanawake kutokata tamaa katika safari yao ya taaluma, akieleza kuwa TAMWA imeendelea kutoa fursa mbalimbali ikiwemo mfuko wa kusaidia elimu kwa wanachama wake.
“Msikate tamaa wanawake, msitosheke na hapo mlipo. TAMWA ina mifuko ya kusaidia kusomesha wanachama wake na tunafurahi kuona hadithi zetu zinaendelea kusomwa na vizazi vingine,” amesema na kuongeza.
“Mbegu za TAMWA zilianza kupandwa 1986 ili kuinua hali zetu kama waandishi wa habari, TAMWA ilikuwa ndio asasi ya kwanza ya habari kufanyiwa usajili. Tulipata changamoto nyingi ikiwemo kuonekana waasi lakini hatukukata tamaa na tuliendea kutoka waandishi 13 mpaka sasa tupo zaidi ya 410.”
Kwa mujibu wa takwimu za TAMWA, chama hicho kilichoanzishwa mwaka 1987, kimekuwa na mchango mkubwa katika kampeni za kupinga ukatili wa kijinsia, ndoa za utotoni na ubaguzi dhidi ya wanawake kupitia mafunzo ya wanahabari, tafiti na programu za kijamii kwa zaidi ya miongo mitatu sasa.