TRA YATOA VIFAA TIBA VYA SHILINGI MILIONI 40 DAR ES SALAAM

::::::::

Uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam umepokea msaada wa vifaa tiba na viti mwendo vyenye thamani ya shilingi milioni 40 kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kusaidia wagonjwa katika hospitali mbalimbali za mkoa huo.

Msaada huo ulipokelewa Februari 7, 2026 jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Mpogolo aliipongeza TRA kwa mafanikio makubwa ya ukusanyaji wa mapato pamoja na juhudi zake za kurejesha sehemu ya mapato hayo kwa jamii kupitia huduma mbalimbali.

Alisema katika mwaka wa fedha 2025/2026, TRA imefanikiwa kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 32 sawa na asilimia 103 ya lengo lililowekwa, jambo linaloonyesha ufanisi mkubwa wa taasisi hiyo.

Kwa upande wake, Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Mcha Hassan Mcha, alisema msaada huo umetolewa kama sehemu ya kurudisha kwa jamii na kusaidia kutatua changamoto katika sekta ya afya.

Aliongeza kuwa utoaji wa vifaa hivyo umezingatia pia kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ambayo huadhimishwa Machi 8 kila mwaka, kwa kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya jamii na uchumi.

Naye Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Dk. Frank Chiduo, aliishukuru TRA kwa msaada huo akisema utasaidia kuboresha huduma za afya na kupunguza vifo vya kina mama na watoto wachanga.

Mpogolo aliwahimiza wananchi kuendelea kulipa kodi kwa hiari, akisema ushirikiano wa walipa kodi unawezesha Serikali kutekeleza miradi ya maendeleo na kuboresha huduma kwa jamii.