Dar es Salaam. Zaidi ya nusu karne tangu kuanzishwa kwa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Tanzania imepiga hatua kadhaa katika kuinua nafasi ya wanawake katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi.
Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, changamoto kama mfumo dume, ukosefu wa fursa sawa na vitendo vya ukatili wa kijinsia bado vinaendelea kuwa kikwazo katika safari ya kufikia usawa wa kijinsia.
Leo Jumapili ya Machi 8, 2026, Tanzania inaungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani. Maadhimisho haya yalianzishwa rasmi mwaka 1975 na hivyo mwaka huu yanafikia mara ya 51 tangu kuanza kuadhimishwa kimataifa.
Maadhimisho ya mwaka huu pia yanakuja katika kipindi cha miaka 31 tangu mkutano mkubwa wa kimataifa kuhusu wanawake uliofanyika mwaka 1995 mjini Beijing, China. Katika mkutano huo, mataifa ya dunia yalipitisha azimio muhimu lililosisitiza kuwa haki za wanawake ni haki za binadamu, hatua iliyoweka msingi wa juhudi za kimataifa za kuimarisha usawa wa kijinsia.
Kwa Tanzania, katika miongo iliyopita kumeshuhudiwa maendeleo yanayoonekana katika elimu ya wanawake, ushiriki wao katika nafasi za uongozi na upatikanaji wa huduma za afya.
Wanawake wengi zaidi sasa wanapata elimu ya juu, kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi katika sekta za umma na binafsi, na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya jamii.
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya jinsia wanasema bado kuna kazi kubwa ya kufanyika. Mfumo dume unaoendelea kushikilia baadhi ya mila na mitazamo ya kijamii, pamoja na ukosefu wa fursa sawa katika maeneo kadhaa ya kiuchumi na kijamii, unaendelea kuwa changamoto kwa wanawake wengi.
Aidha, vitendo vya ukatili wa kijinsia bado vinaripotiwa katika jamii mbalimbali, hali inayodhoofisha juhudi za kuimarisha usawa na haki za wanawake.
Kwa maneno machache, taswira ya mwanamke wa Tanzania leo inaonyesha mchanganyiko wa mafanikio na changamoto. Ni picha ya mwanamke anayepiga hatua mbele katika nyanja nyingi, lakini wakati huo huo akiendelea kukabiliana na vikwazo vya kijamii vinavyohitaji juhudi za pamoja kuvikabili na kuviondoa.
Kwa mantiki hiyo, maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yanabaki kuwa fursa muhimu ya kutafakari mafanikio yaliyopatikana, huku yakichochea mjadala na hatua zaidi za kuhakikisha wanawake wanapata haki, fursa na heshima stahiki katika jamii.
Taarifa za Umoja wa Mataifa (UN) kuhusu kumbukumbu ya miaka 30 ya Beijing, zinaeleza kuwa Tanzania imepiga hatua katika maeneo ya elimu, afya na ushiriki wa wanawake katika ngazi ya uamuzi.
Kwa mfano, miaka mitano iliyopita, UN ilisema wasichana wanaomaliza elimu ya msingi walikuwa wameongezeka kutoka asilimia 68 mwaka 2000 hadi asilimia 89 mwaka 2022, suala ambalo kwa sasa linatarajiwa kuwa na mafanikio zaidi.
Kwa upande wa wanaomaliza elimu ya sekondari, ilieleza wameongezeka kutoka asilimia 45 mwaka 2000 hadi kufikia asilimia 72 mwaka 2022, huku vyuo vikuu ushiriki wa wanawake ukipanda kutoka asilimia 35 mwaka 2000 hadi asilimia 48 kwa kipindi hicho.
Kwa msingi huo, Mshauri wa masuala ya jinsia, Profesa Asha Makundi anasema elimu imekuwa msingi wa mabadiliko ya kijinsia nchini na ndio iliyofungua milango ya wanawake wengi kuingia katika uongozi, uchumi na taaluma mbalimbali ambazo hapo zamani zilikuwa zikionekana ni za wanaume pekee.
Sio hayo tu, mafanikio mengine ni kutengwa kwa asilimia 10 ya mapato ya halmashauri kwa ajili ya mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu huku Serikali ikiwa tayari imetoa Sh200 bilioni kuwezesha biashara za wanawake na vijana.
Katika uwiano wa nafasi za uongozi, Tanzania imeweka rekodi ya kihistoria kwa kuwa na Rais wa kwanza mwanamke tangu ipate uhuru.
Naye ni Rais Samia Suluhu Hassan aliyeingia madarakani mwaka 2021 na sasa anatajwa kama ishara ya maendeleo ya usawa wa kijinsia katika uongozi kwa nchi yake.
Kwa sasa yuko katika muhula wa pili baada ya ule wa kwanza alioupokea kutoka kwa mtangulizi wake, Rais John Magufuri, aliyefariki dunia na Katiba ikampa mamlaka ya kukalia kiti hicho.
Katika nafasi ya ubunge ingawa idadi yao inaongezeka, hali si shwari sana. Uchaguzi mkuu uliopita, ulikuwa na wagombea 558 wanawake, ambao waliteuliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kugombea ubunge wa majimbo kupitia vyama vya siasa 18 vilivyoshiriki uchaguzi mkuu huo.
Idadi hiyo ni sawa na asilimia 32.17 ya wagombea wote 1,735 wa ubunge walioteuliwa na INEC katika uchaguzi huo. Kwa maneno mengine, katika kila wagombea 10 wa nafasi hiyo, watatu walikuwa wanawake.
Hata hivyo, kati ya wanawake hao 558 walioteuliwa kugombea majimboni, zaidi ya robo tatu walishindwa kufurukuta kwa wingi wa kura, 37 pekee ndiyo walioshinda ubunge, sawa na asilimia 6.63.
Ukiacha kwenye nafasi za ubunge, serikalini nako hali si shwari. Kati ya mawaziri 28 walioteuliwa na Rais Samia kuunda Baraza la Mawaziri, wanawake ni wanne pekee, sawa na asilimia 14.3.
Kwa upande wa unaibu mawaziri, kati ya 28 walioteuliwa, 10 ni wanawake.
Mchambuzi wa maendeleo ya kijinsia, Rehema Mosha anasema bado wanawake wanakabiliwa na changamoto kubwa katika kupata nafasi za uongozi.
Ingawa baadhi yao wamekuwa na mwamko wa kushiriki chaguzi, anasema wanakosa msuli wa kushindana kwa sababu bado wanakabiliwa na changamoto za kiuchumi na lugha chafu dhidi yao.
“Ukikuta mwanamke anashindana kwenye nafasi fulani, ujue amepitia mengi. Wengi kwa sababu ya hayo wanaogopa hata kwenda kugombea. Ndio maana unakuta nafasi za wabunge wa viti maalumu, wagombea huwa ni wale wale, wengi hawatamani kuwania majimbo,” anasema.
Mtaalamu wa Sheria, Nancy Aloyce anasema ingawa idadi ya wanawake bungeni imeongezeka, bado wanaochaguliwa moja kwa moja majimboni ni wachache ikilinganishwa na wanaume.
Anasema licha ya mfumo wa viti maalumu kuchangia kuongeza uwakilishi wa wanawake bungeni, lakini bado kuna haja ya kuweka mazingira yatakayowawezesha wanawake wengi zaidi kugombea na kushinda nafasi za uongozi kupitia majimbo.
“Hivi viti maalumu vinatufanya tuonekane kama sisi ni wahitaji maalumu, pia vinalemaza, nafikiri wanawake tunapaswa kuwa na uwezo wa kupambana majimboni sio kutegemea viti maalumu,” anasema.
Katika vyama vya siasa, imeshuhudiwa sekretarieti zikiwa na wanaume wengi zaidi ya wanawake. Angalau Chama cha Mapinduzi (CCM), kina wajumbe wawili wanawake kwenye sekretarieti yake.
Wajumbe hao ni, Katibu Mkuu, Dk Asha-Rose Migiro na Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Abdallah Hamid.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kina mwanamke mmoja katika kurugenzi zake, ambaye ni Brenda Rupia, mkurugenzi wa mawasiliano na uhusiano.
ACT – Wazalendo nao, sekretarieti yake ina wajumbe wawili wanawake, ambao ni Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu na Naibu Katibu Mkuu Bara, Esther Thomas.
Kwa upande wa umiliki wa rasilimali nako kunasuasua. Kwa mujibu wa taarifa ya Taasisi ya Generation Equality ya mwaka 2023, asilimia 25 ya wanaume wanamiliki ardhi pekee yao, ukilinganisha na asilimia nane kwa wanawake.
Katika umiliki wa nyumba, asilimia 26 ya wanaume wanamiliki nyumba, ikilinganishwa na asilimia saba ya wanawake.
“Umiliki wa rasilimali ndio msingi wa nguvu ya kiuchumi. Bila ardhi au mitaji, wanawake wengi wanabaki katika uchumi usio rasmi,” anasema Rehema.
Ukatili bado ni changamoto katika safari ya usawa wa kijinsia nchini. Miongoni mwa sababu zinazoathiri wanawake ni ndoa za utotoni, mimba katika umri mdogo na unyanyasaji wa majumbani.
Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) asilimia 12 ya wasichana vijijini huacha shule kutokana na ndoa za utotoni na mimba za mapema.
Profesa Asha anasema Tanzania iko katika hatua muhimu ya safari ya usawa wa kijinsia.
“Serikali imeanza kutekeleza sera na mikakati mbalimbali ikiwemo sera ya maendeleo ya jinsia ya mwaka 2023, inayolenga kuongeza ushiriki wa wanawake katika uongozi, elimu na uchumi,” anasema.