Mecktilder kielelezo cha mwanamke anayeipambania sekta ya madini

Dar es Salaam. Katika simulizi nyingi za sekta ya madini, taswira inayojitokeza mara nyingi ni ya migodi mikubwa, mashine nzito na wafanyakazi ambao ni wanaume waliovalia mavazi ya kazi wakiwa katikati ya vumbi na mawe.

Lakini hali haiko hivyo katika siku za hivi karibuni, kwa sababu ndani ya mnyororo huo mrefu wa thamani, kuna sura nyingine inayozidi kung’ara ambayo ni ya mwanamke anayeongeza thamani ya madini kabla hayajafika sokoni.

Hapo ndipo anasimama mwana mama Mecktilder Mchomvu. Jina lake limekuwa kama taa ya matumaini kwa wanawake wanaotazama sekta ya madini kwa hofu au shaka.

Yeye ameichagua sekta hiyo si kama mtazamaji, bali kama mshiriki hai, muongezaji thamani wa madini na mtetezi wa ushiriki mpana wa wanawake na vijana.

Mchomvu anasema hamu yake ni kutaka kuona wanawake wengi zaidi wakikimbilia fursa zilizopo kwenye sekta ya madini nchini.

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, Mchomvu anasema madini si kuchimba pekee. “Lakini ndani yake kuna biashara, ubunifu, teknolojia, masoko na taaluma zinazoweza kubadili maisha ya mwanamke bila kushika koleo,” anasema.

Akiwa Mkurugenzi Mtendaji na Mwanachama Mwanzilishi wa Tanzania Women in Mining and Mineral Industry (TWiMMI), taasisi inayowawezesha wanawake na vijana kushiriki kikamilifu katika sekta ya madini na rasilimali zake nchini, Mecktilder anaizungumza sekta hiyo kwa uzoefu wa zaidi ya miaka 15.

Anasema anakumbuka alipoianza kazi hiyo wakati ambao taarifa zilikuwa haba, mwongozo haukuwa wazi na milango ya fursa haikuonekana kwa urahisi katika sekta hiyo ya madini.

“Nilikuwa sijui nianzie wapi, nifanye nini na leseni ipi ninayohitaji,” ameiambia Mwananchi ilipofanya naye mahojiano maalumu hivi karibuni kuelekea Machi 8, Siku ya Wanawake Duniani.

Lakini anasema jambo lingine lilikuwa ukosefu wa taarifa na uelewa wa sheria za madini ilikuwa changamoto ya kwanza kwake.

Ametaja nyingine ilikuwa mtaji, kwa mujibu wake, mikopo iliyokuwepo haikuwa ikizingatia uhalisia wa sekta hiyo.

“Riba za juu zilizofikia asilimia 33, ilitukatisha  tamaa vijana na wanawake wengi tuliokuwa tunataka kuingia kwenye mnyororo wa thamani wa madini. Hivyo ilikuwa vigumu kusonga mbele,” anasema Mchomvu.

Hivyo, anasema kutokana na hali hiyo, ndipo akapata  wazo la kuunda umoja wa kuwaunganisha wanawake na vijana huku akisema lengo lilikuwa kuondoa giza la taarifa, kujenga uelewa wa sheria na kufungua milango ya mitaji na masoko.

Mnyororo wa thamani fursa iliyojificha

Kwa mtazamo wa kiuchambuzi, sekta ya madini si eneo la wachimbaji pekee. Ni mnyororo mrefu unaojumuisha wachimbaji, wauzaji, waongezaji thamani, wasafirishaji, watumiaji na watoa huduma. Mchomvu anasema ndani ya kila kiungo, kuna nafasi ya ubunifu na ajira.

Hata hivyo, anasema amejikita zaidi kwenye eneo la uongezaji thamani, hatua inayobadilisha jiwe ghafi kuwa bidhaa yenye thamani kubwa sokoni.

“Hapa ndipo elimu, ubunifu na ujuzi wa mikono hukutana. Kukata, kung’arisha na kusanifu madini ni taaluma inayohitaji ustadi, si nguvu za mwili pekee,” anafafanua mwana mama huyo.

Anasema kwa kufanya hivyo, amejikuta akivunja dhana kwamba mwanamke katika madini lazima awe mgodini tu.

 “Lakini ukweli ni kwamba, mwanamke anaweza kufanya kazi kwenye maabara ya madini, karakana au ofisini, huku anatengeneza thamani inayoongeza kipato mara dufu au zaidi kama nifanyavyo mimi,” anasema.

Hata hivyo, kupitia TWiMMI, Mchomvu anasema wameanzisha programu mbalimbali za kuwawezesha wanawake na vijana na mojawapo ni ya “Pamoja Initiative,” inayotoa mafunzo ya siku tatu kuanzia darasani.

Anasema siku ya kwanza darasani huwa wanajifunza aina za madini, namna yanavyoongezwa thamani na masoko yaliyopo duniani.

Anasema wataalamu hushirikishwa kuonesha ramani ya masoko ya kimataifa na jinsi mwanamke anavyoweza kushiriki.

Siku ya pili washiriki hujifunza madini kwa vitendo ikiwamo kuyakata, kuyaongeza thamani na baadaye kutembelea migodini kuona maeneo yakochimbwa na namna ya kuyatambua.

Mchomvu anasema hatua hiyo husaidia kumuondolea hofu mwanafunzi na kumjengea  uelewa zaidi.

“Programu nyingine inalenga kuwafundisha wachimbaji wanawake na vijana umuhimu wa kutumia vifaa vya kujikinga kazini, sambamba na mafunzo ya fedha, biashara na afya,” anasema Mecktilder.

Hata hivyo, Mchomvu anasema uchimbaji salama na usimamizi mzuri wa mapato ni nguzo mbili za mafanikio ya muda mrefu mtu anapotengeneza mnyororo wa thamani wa madini.

Anasema mpaka sasa wameshawafikia zaidi ya vijana na wanawake 3,500 katika mikoa ya Geita, Kahama, Shinyanga, Lindi na Dodoma, huku wakitarajia kupanua wigo zaidi.

Anasema kwa sasa, ushiriki wake hauishii ndani ya mipaka ya Tanzania, bali ni Mjumbe wa Bodi ya Investing in African Mining Indaba.

Amasema bodi hiyo huwa inaandaa mkutano mkubwa wa kila mwaka wa sekta ya madini barani Afrika unaofanyika Afrika Kusini, unaowaleta pamoja viongozi wa Serikali, wawekezaji na wadau wa sekta hiyo.

Anasema kupitia jukwaa hilo, amewahi kwenda na vijana ili wakutane na watoa uamuzi wa sekta ya madini.

Mchomvu anasema hilo linafungua mitazamo mipya na kuwapa ujasiri wa kuingia katika majadiliano ya kimataifa.

Kwa mujibu wake, baadhi ya wanawake wa Tanzania wametambuliwa katika mkutano huo kwa ubora wao katika ujasiriamali wa madini na uhamasishaji bora wa uchimbaji.

“Hii ni ishara kwamba juhudi za ndani zinaweza kuzaa matunda hata kimataifa,” anasema Mchomvu.

Anakiri kuwa Serikali imekuwa na mchango katika kuwawezesha wanawake kuinuka katika sekta hiyo.

Anasema maboresho ya sera na sheria, utoaji wa leseni maalumu kwa wanawake na vijana, pamoja na ushiriki wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico) katika kutoa vifaa vya uchimbaji, ni miongoni mwa hatua zinazotajwa.

Pia, utekelezaji wa sera za ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya uziduaji ikiwamo manunuzi ya ndani, ajira na uhawilishaji teknolojia, umeongeza fursa kwa wazawa.

Hata hivyo, anabainisha kuwa bado yapo maeneo yanayohitaji maboresho, hasa upatikanaji wa taarifa sahihi za madini na urahisishaji wa masoko ili kupunguza utegemezi kwa mabroka.

Kwa mtazamo wake, anasema Tanzania imepiga hatua kubwa ikilinganishwa na baadhi ya mataifa ya Afrika katika sheria na masoko, lakini utekelezaji bora na uwazi zaidi vitaharakisha mafanikio.

Mabadiliko ya mitazamo ya watu

Miaka ya nyuma, mwanamke akionekana mgodini alikumbana na maneno ya kubezwa na hata imani potofu.

Kulikuwa na dhana kwamba uwepo wa mwanamke ungeathiri upatikanaji wa madini.

Hata hivyo, Mchomvu anasema hivi sasa hali hiyo imebadilika. Wanawake wameanza kumiliki mitambo, kushiriki uchenjuaji na kuonekana kama wajasiriamali kamili katika sekta hiyo. Mchomvu anasema mabadiliko ya mtazamo yamekuja kupitia uthibitisho wa vitendo, wanawake wakionesha ufanisi na uadilifu katika kazi zao.

Kwa TWiMMI, hilo ni jambo la kujivunia kuona wanawake wakionekana si kama wageni, bali kama wadau halali wa sekta ya madini.

Wito kwa mwanamke wa leo;

Kwa mwanamke ambaye bado anaitazama sekta ya madini kwa mbali, Mchomvu ana ujumbe wa wazi akisema, “wakati ni sasa, fursa ni nyingi kuanzia uchimbaji, uongezaji thamani, biashara ya madini, hadi utoaji wa huduma.”

Anasisitiza kuwa kinachohitajika kwa wanawake na wasichana wa sasa ni ujasiri na utayari wa kujifunza.

“Kila mtu ana nafasi ya kunufaika, iwapo ataamua kuichukua,” anasema Mchomvu.