Milipuko Mikubwa Yatikisa Tehran Baada ya Israel Kushambulia Vituo vya Mafuta

Tehran, Iran – Mlipuko mkubwa na moto uliotanda angani uliripotiwa katika mji mkuu wa Iran, Tehran, baada ya Israel kufanya mashambulizi kadhaa yaliyolenga vituo muhimu vya kuhifadhi mafuta.

Kwa mujibu wa jeshi la Israel (IDF), mashambulizi hayo yalilenga maeneo kadhaa ya kuhifadhi mafuta yanayodaiwa kutumiwa na vikosi vya kijeshi vya Iran kusambaza nishati kwa shughuli zao za kijeshi. Mashambulizi hayo yalisababisha milipuko mikubwa na moto mkubwa uliotuma moshi mzito wa rangi ya machungwa angani, huku video zilizorekodiwa na wakazi zikisambaa mitandaoni zikionyesha moto mkubwa ukiteketeza maeneo hayo.

Mashambulizi hayo ni sehemu ya mzozo unaoendelea kati ya Israel na Iran ambao sasa umeanza kuathiri nchi nyingine za Mashariki ya Kati.

Wakati huo huo, tukio lingine liliripotiwa katika mji wa Dubai, ambapo dereva mmoja raia wa Pakistan alifariki baada ya vipande vya chuma (shrapnel) kuangukia gari lake kufuatia shambulio la droni lililozuiwa katika eneo la Al Barsha. Droni hiyo ilidaiwa kulenga jengo la ghorofa 19 la Azayez Tower.

Katika tukio tofauti, moshi mkubwa ulionekana ukitoka katika jengo refu la ghorofa 88 la 23 Marina, baada ya shambulio jingine lililoripotiwa kuhusishwa na mashambulizi ya Iran. Maafisa wa Falme za Kiarabu (UAE) walielezea tukio hilo kama “incident ndogo” na kusema hakuna vifo vilivyoripotiwa katika tukio hilo.

Iran kupitia Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ilidai kuwa imefanikiwa kulenga vituo vya kijeshi vya Marekani katika eneo la Dubai Marina katika wimbi la 27 la operesheni yao waliyoipa jina la “True Promise 4”.

Katika eneo la Lebanon, angalau watu wanne waliripotiwa kuuawa na wengine 10 kujeruhiwa kufuatia shambulio lingine la Israel lililolenga hoteli moja katika mji wa Beirut.

Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ameomba radhi kwa nchi jirani kufuatia mashambulizi yaliyolenga mali za Marekani katika mataifa ya Ghuba. Alisema Iran haina nia ya kuvamia nchi jirani na kwamba mashambulizi yaliyogusa baadhi ya nchi huenda yalitokana na “kutokuelewana ndani ya vikosi vya jeshi”.

Hata hivyo, Pezeshkian alionya kuwa mashambulizi yanaweza kuendelea endapo Iran itaendelea kushambuliwa.

Kwa upande wake, Rais wa Marekani Donald Trump ameonya kuwa Iran “itapigwa kwa nguvu zaidi”, akisema taifa hilo linaendelea kudhoofishwa na mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya miundombinu ya kijeshi ya Iran.

Mzozo huo unaendelea kuongeza hofu ya kuzuka kwa vita vikubwa zaidi katika eneo la Mashariki ya Kati huku mashambulizi na mashambulizi ya kulipiza kisasi yakiripotiwa katika nchi kadhaa za eneo hilo.