Global Publishers
March 8, 2026
0 Comments
MKUU wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, amethibitisha kukamatwa kwa wanachuo 17 wa Chuo cha Ardhi tawi la Tabora kwa tuhuma za kumpiga mlinzi wa chuo hicho na kumng’oa meno manne.
Kwa mujibu wa Chacha, wanachuo hao kwa sasa wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Tanzania mkoani Tabora kufuatia tukio hilo, huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo na wahusika wote wa tukio hilo.
Aidha, imeelezwa kuwa wanafunzi wawili kati yao walikutwa na silaha aina ya kisu katika eneo la bweni lao, jambo ambalo ni kinyume cha sheria pamoja na kanuni za chuo.
Chacha amesema kwa sasa jina la mlinzi aliyejeruhiwa limehifadhiwa wakati uchunguzi unaendelea, huku akiuagiza uongozi wa chuo hicho kuwasimamisha masomo wanachuo hao mara moja na kuhakikisha wanachukuliwa hatua za kisheria kwa kufunguliwa mashitaka.
Vilevile, Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wanafunzi wa vyuo mbalimbali kuepuka kujihusisha na vitendo vya uhalifu na badala yake kujikita katika masomo yao.
“Vyuo ni maeneo ya kujifunza na kujenga mustakabali wa maisha, siyo kufanya vitendo vya uhalifu,” alisisitiza.