Rais Samia atoa ujumbe wa siku ya wanawake duniani

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amehimiza kuendeleza juhudi za kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata haki na usawa ili kuchochea maendeleo jumuishi ya Taifa.

Rais Samia ametoa wito huo leo Machi 8, 2026 katika ujumbe wake kwa Taifa wa  maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, akieleza  siku hii ni muhimu kwa kutambua mchango mkubwa wa wanawake katika maendeleo ya familia, jamii na Taifa kwa ujumla.

Akitaja msingi wa maadhimisho hayo amesema mwaka huu Kitaifa yanaongozwa na kaulimbiu isemayo; “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana, Msingi Jumuishi wa Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” huku kaulimbiu ya kimataifa ikiwa “Give to Gain,” kutoa ndio kupata.”

Kwa mujibu wa Rais Samia, kaulimbiu hizo zinakumbusha maendeleo ya kweli ya jamii na Taifa yanajengwa katika misingi ya haki, usawa na ushirikishwaji.

“Kaulimbiu hizi zinatukumbusha kwamba maendeleo ya kweli ya jamii na Taifa letu yanajengwa katika msingi wa haki, usawa na ushirikishwaji, pamoja na moyo wa kujitoa, kushirikiana na kuwainua wengine,” amesema.

Rais Samia amesema katika maisha ya kila siku, mwanamke ana nafasi kubwa katika ustawi wa jamii na Taifa.

“Kwa asili, mwanamke ni mama, ni mlezi, ni kiongozi na ni mfariji wa familia, jamii na Taifa. Katika maisha ya kila siku, wanawake wanahimili kwa vitendo falsafa ya ‘Kutoa ndio Kupata’. Wanajitoa kwa familia zao, wanalea kizazi, wanahudumia jamii na wanachangia kwa namna mbalimbali maendeleo ya Taifa letu,” amesema.

Amesema hata wanapokumbana na changamoto, wanawake hubaki kuwa imara na hutumia hekima na uvumilivu kukabiliana nazo kwa manufaa ya jamii.

“Hata katika nyakati za changamoto, mwanamke hakimbii majukumu. Badala yake, hubeba changamoto hizo kwa ujasiri na hekima, kuzielekeza kuwa nguvu ya kuimarisha familia, jamii na Taifa. Mwanamke hulea familia, hulea jamii yake, hulea Taifa, hulea bara na hata hulea dunia,” amesema.

Katika ujumbe wake huo, Rais Samia pia ametaja mifano ya wanawake waliotoa mchango mkubwa duniani akiwemo Mother Teresa, Wangari Maathai na Graça Machel, pamoja na wanawake wengine barani Afrika waliopigania ustawi wa jamii.

Akitaja heshima aliyopewa yeye kama kinara wa masuala ya afya barani Afrika, Rais Samia amesema anaendelea kushirikiana na wanawake katika juhudi za kuimarisha afya ya uzazi na ustawi wa mama na mtoto barani Afrika, akitaja jukumu lake kama kinara wa  Afrika katika masuala ya afya ya mama, mtoto na afya ya uzazi.

“Jukumu hili linahusisha kuhamasisha juhudi za pamoja ili kupunguza vifo vya mama na watoto vinavyoweza kuzuilika barani Afrika, kuimarisha huduma za afya ya uzazi, na kuhakikisha kila mama na mtoto wanapata haki yao ya msingi ya huduma bora za afya,” amesema.

Rais Samia amesema mafanikio ya juhudi hizo yanategemea mshikamano wa wanawake na jamii kwa ujumla, akitoa wito kwa wanawake kote nchini kuendelea kushiriki kikamilifu katika maendeleo.

“Ninawaalika wanawake wote wa Tanzania kuendelea kuwa sehemu ya juhudi hizi kujitolea kwa maendeleo na kushika nafasi mbalimbali za uongozi katika jamii,” amesema.

Pia, ametoa wito kwa wanawake wa makundi mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara, wakulima, wafanyakazi wa sekta binafsi na umma, walimu, wahudumu wa afya, viongozi wa taasisi, wanahabari, wanasharia, wabunifu na wanafunzi kushirikiana katika kulinda afya ya mama na mtoto pamoja na kuimarisha usawa wa kijinsia.

Amesisitiza kuwa kupitia mshikamano na vitendo vya kujitoa kwa ajili ya maendeleo ya wanawake na watoto, jamii itaweza kuishi kwa vitendo kaulimbiu ya mwaka huu ya “Give to Gain.”

Aidha, Rais Samia amewatakia wanawake wote nchini na duniani maadhimisho mema ya Siku ya Wanawake Duniani yanayoadhimishwa duniani kote leo.