Dar es Salaam. Katika ulimwengu wa leo, wazazi wengi wanajikuta wakiwa katika mbio zisizokwisha za kutafuta maisha bora. Gharama za elimu, matibabu, makazi na mahitaji mengine ya msingi zimeongezeka.
Hivyo, hali hiyo huwalazimu wazazi wengi kutumia muda mwingi kazini au katika shughuli za kujiongezea kipato.
Hata hivyo, swali la msingi linalopaswa kujiuliza ni hili: Je, mipaka ya kutafuta maisha iko wapi linapokuja suala la malezi ya watoto?
Ni ukweli usiopingika kuwa jukumu la mzazi si tu kuzaa tu, bali pia kulea. Malezi yanahitaji uwepo wa mzazi kimwili na kihisia.
Mtoto hahitaji tu ada ya shule na sare nadhifu; anahitaji pia mazungumzo, ushauri, uangalizi na upendo.
Wataalamu wa saikolojia ya watoto wanaeleza kuwa uwepo wa mzazi katika makuzi ya mtoto hujenga hisia ya usalama na kujiamini.
Kukosekana kwa uwepo huo kwa muda mrefu kunaweza kuathiri mwenendo, tabia na hata mafanikio ya mtoto shuleni.
Katika harakati za kutafuta maisha, baadhi ya wazazi hulazimika kufanya kazi mbali na familia zao, wengine husafiri mara kwa mara na wapo wanaotumia muda mwingi nje ya nyumbani kuanzia asubuhi hadi usiku.
Ingawa nia yao ni njema, lakini inapaswa kuhakikisha familia inaishi vizuri, hali hiyo inaweza kuacha pengo katika malezi. Mtoto anapokosa mwongozo wa karibu kutoka kwa wazazi, anaweza kuathiriwa kirahisi na marafiki, mitandao ya kijamii au mazingira yasiyo salama.
Hii haimaanishi kuwa mzazi asitafute maisha. La hasha. Kazi ni sehemu ya wajibu wa mzazi. Lakini ni muhimu kuweka mizania. Mipaka ya kutafuta maisha inapaswa kuzingatia maslahi mapana ya mtoto.
Na mzzi unapaswa kujiuliza; Je, muda unaotumika kazini unaruhusu angalau mazungumzo ya kila siku na mtoto?
Je, mzazi anafahamu marafiki wa mtoto wake, maendeleo yake shuleni na changamoto anazokutana nazo?
Haya ni maswali yanayopaswa kuongoza uamuzi wa kila siku wa mzazi.
Kwa upande mwingine, kuna wazazi wanaoamini kuwa kutoa kila kitu cha kimwili ndiko kunakokamilisha jukumu lao. Mtoto anapopewa simu ya kisasa, nguo za gharama na matumizi ya kutosha, huonekana kama ametimizwa mahitaji yake.
Lakini tafiti zinaonyesha kuwa mahitaji ya kihisia yana uzito mkubwa zaidi katika ustawi wa mtoto.
Kukaa pamoja mezani wakati wa chakula, kusikiliza simulizi zake na kushiriki katika shughuli zake za shule ni sehemu ya malezi bora yasiyonunulika kwa fedha.
Jamii nayo ina nafasi yake katika mjadala huu. Katika utamaduni wa Kiafrika, malezi yalikuwa jukumu la familia pana.
Leo hii, mabadiliko ya kijamii na kiuchumi yamepunguza mtandao huo wa msaada. Hivyo, mzazi analazimika kubeba mzigo mkubwa peke yake.
Hata hivyo, hili halipaswi kuwa kisingizio cha kupuuza wajibu wa karibu kwa mtoto. Badala yake, linapaswa kuwa kichocheo cha kupanga ratiba na vipaumbele kwa busara zaidi.
Ni vyema pia kutambua kuwa ubora wa muda ni muhimu kuliko wingi wake. Mzazi anaweza kuwa na ratiba yenye msongamano, lakini akatenga muda maalumu wa kuzungumza na mtoto bila bughudha za simu au kazi.
Dakika chache za mazungumzo ya dhati zinaweza kuwa na athari kubwa kuliko saa nyingi za kuwepo kimwili bila mawasiliano ya karibu.
Katika zama hizi za ushindani wa kiuchumi, tunahitaji kizazi chenye maadili, nidhamu na ujasiri wa kukabiliana na changamoto.
Haya hayawezi kujengwa na shule pekee wala na fedha peke yake, bali yanajengwa nyumbani kupitia mfano wa mzazi na maelekezo yake ya kila siku. Mipaka ya kutafuta maisha inapaswa kuwekwa pale harakati hizo zinapoanza kuathiri uhusiano wa mzazi na mtoto.
Kwa hiyo, mzazi anapaswa kujitathmini mara kwa mara kwamba je; ninatafuta maisha kwa ajili ya mtoto au ninapoteza maisha ya mtoto wangu kwa sababu ya kuyatafuta maisha? Mizania kati ya kazi na malezi si jambo la anasa; ni hitaji la msingi.
Mtoto anayelelewa kwa upendo na uangalizi wa karibu huwa na misingi imara ya maisha, hata kama mazingira ya kiuchumi si ya juu sana.
Mwisho wa yote, mafanikio ya mzazi hayapimwi kwa ukubwa wa kipato pekee, bali pia kwa ubora wa watoto anaowaacha katika jamii.
Kutafuta maisha ni wajibu, lakini kulea ni dhamana. Mipaka hiyo ikizingatiwa tutakuwa tumetimiza jukumu letu kwa kizazi cha leo na cha kesho.