Jua tofauti za mitazamo kati ya wanawake na wanaume

Dar es Salaam. Kwa muda mrefu, wanaume na wanawake wamekuwa na mitazamo tofauti kuhusu namna wenzao wanavyofikiri, kuhisi na kutenda.

Mitazamo hii mara nyingi imejenga vichekesho, mshangao, migogoro na wakati mwingine kutoelewana katika uhusiano. Wanawake, kwa upande wao, wamekuwa wakieleza kuwa wanaume hawawezi kuzieleza hisia zao vya kutosha.

Kwao, mwanaume huonekana kufunga milango ya moyo na kuacha mambo mengi yakibaki kimya, jambo linalowafanya wanawake wajisikie kutengwa au kutoeleweka.

Wanawake pia huona kuwa wanaume hawawezi kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja. Kwa mfano, ni jambo gumu kwa mwanamke kuzungumza na mpenzi wake wa kiume huku akiwa anaangalia mpira wa soka, kwani akili ya mwanaume hujikita katika jambo moja.

Mara nyingi, mwanaume hulazimika kwanza kuacha analofanya ndipo aweze kusikiliza kwa umakini. Aidha, wanawake hudhani kuwa wanaume hujiona wanafanya mambo kwa ufanisi zaidi kuliko walivyo kwa uhalisia, na pia si wasikilizaji wazuri, kwa sababu badala ya kusikiliza hisia zao, hujitahidi haraka kutatua tatizo.

Kwa mtazamo wa wanawake, wanaume ni watu wa ajabu kwani hawapendezwi na ununuzi au kutembelea maduka. Wanawake hushangaa kwa nini jambo linalowapa furaha wao, kwa wanaume linaonekana kama adhabu.

Zaidi ya hayo, kuna mtazamo kuwa wanaume hufikiria sana kuhusu tendo la ndoa kiasi cha kuonekana kama hakuna jambo jingine muhimu akilini mwao.

Kwa upande mwingine, wanaume nao wana mitazamo yao juu ya wanawake. Wanaume hudai kuwa wanawake wana hisia laini sana na kwamba machozi yao yako karibu kiasi kwamba jambo dogo tu linaweza kuwafanya walie.

Pia huona wanawake wana maneno mengi, wakati wao hawana muda wala hamu ya kusikiliza maelezo marefu. Kwa wanaume, wanawake huongeza chumvi katika maelezo na kuwasilisha mambo kwa mtazamo wa hisia zaidi kuliko uhalisia.

Wanaume pia hudai kuwa wanawake huumizwa haraka hata kwa maneno au matendo madogo ambayo hayakuwa na nia mbaya. Katika ununuzi, wanawake huonekana kuchanganyikiwa, wakitumia muda mrefu kuangalia vitu hata kama hawana fedha ya kununua.

Kwa wanaume, hali hii huonekana kutokuwa na mantiki. Aidha, wanaume huona ni vigumu kuwaamini wanawake kwa sababu hubadilisha uamuzi mara kwa mara; leo wanasimamia jambo moja na kesho wanakuwa na msimamo tofauti kabisa.

Mtazamo mwingine wa wanaume ni kuwa wanawake hutoa hitimisho haraka bila kuwa na taarifa za kutosha. Badala ya kuangalia uwezekano zaidi ya mmoja, wanawake huweza kuamini tafsiri wanayojenga akilini mwao.

Mfano unaotajwa mara kwa mara ni pale mwanaume anaposhindwa kupokea simu; badala ya kufikiria sababu nyingi, mwanamke anaweza kuhitimisha kuwa mwanaume huyo yuko na mwanamke mwingine, hali inayoweza kusababisha ugomvi usio na msingi.

 Pia wanaume hudhani wanawake huamini kuwa wanaume wana uwezo wa kusoma mawazo yao, ilhali wao hutamani waelezwe waziwazi wanachohitaji na wanavyohisi.

Chanzo cha tofauti hizi nyingi kimeelezwa kuwa ni muundo wa ubongo. Ubongo wa mwanamke una muunganiko mkubwa zaidi kati ya pande zake mbili kupitia mishipa ya mawasiliano, jambo linalowezesha mawasiliano ya haraka ndani ya ubongo.

Hali hii humsaidia mwanamke kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja kwa ufanisi zaidi. Kwa mwanaume, muunganiko huo ni mdogo, hivyo humfanya ajikite katika jambo moja kwa wakati mmoja.

Tofauti hizi pia hujitokeza wazi katika masuala ya tendo la ndoa. Mara nyingi wanaume huonekana kuwa na hamu kubwa zaidi ya kufanya tendo la ndoa, hata katika mazingira ambayo hayawafurahishi wapenzi wao wa kike.

Hii inahusishwa na sababu za kibaiolojia na kimaumbile. Vilevile, wanaume hufika kileleni kwa haraka zaidi kuliko wanawake, jambo ambalo limesababisha migogoro mingi katika uhusiano.

Wanawake wengi hawako tayari kueleza kutoridhika kwao, hivyo hujifanya wamefika kileleni ili kumridhisha mwanaume au kumlinda kisaikolojia. Hali hii imechangia kuibuka kwa biashara ya dawa na bidhaa zinazodaiwa kusaidia mwanaume kuchelewesha kufikia kileleni.

Aidha, wanaume wanaweza kutamani kufanya mapenzi hata wakiwa na hasira au maumivu ya kihisia. Kwao, hisia za hasira na hamu ya tendo la ndoa huwekwa katika mifumo tofauti.

Kwa wanawake, hali ni tofauti kabisa; mfumo wao wa kihisia huathiri mwili mzima. Mwanamke akiumizwa au kukasirishwa, hamu ya tendo la ndoa hupotea hadi pale atakaposaidiwa kurejea katika hali ya utulivu.

Changamoto hujitokeza pale mwanaume anapodhani kuwa mwanamke anamnyima penzi kwa makusudi, badala ya kuelewa hitaji la kusawazisha kwanza hisia zake.

Katika mazingira haya, tafiti zimeonyesha kuwepo kwa vitendo vya ubakaji ndani ya uhusiano na ndoa.

Kwa ujumla, kuelewa tofauti hizi ni hatua muhimu katika kujenga uhusiano wenye afya. Tofauti si adui wa uhusiano, bali ni changamoto inayohitaji uelewa, uvumilivu na mawasiliano ya wazi.