PROF. KABUDI AWAHIMIZA DIASPORA KUWEKEZA NCHINI TANZANIA

:::::::

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalum), Prof. Palamagamba Kabudi, amewahimiza Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) kuendelea kuwekeza nchini na kushiriki kikamilifu katika juhudi za maendeleo ya taifa.

 Amesema Watanzania walioko ughaibuni wana nafasi kubwa ya kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi kupitia mitaji, utaalamu na uzoefu walioupata nje ya nchi. Prof. Kabudi ameyasema hayo wakati wa mkutano na Watanzania wanaoishi jijini London, Uingereza, ambapo aliwasilisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na ujumbe wa serikali kwa Watanzania waishio ughaibuni. 

Amesema serikali inaendelea na juhudi za kurekebisha, kujenga upya na kufanya maboresho katika sekta mbalimbali.

 Aidha, Profesa Kabudi amewataka Watanzania wanaoishi nje ya nchi kununua hisa katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa nchini, kushiriki katika uwekezaji wa pamoja na kutumia utaalamu wao kwa kushirikiana na wataalamu waliopo Tanzania kusaidia maendeleo ya sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu na teknolojia.

 Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Mhe. Mbelwa Kairuki, amesema serikali itaendelea kushirikiana kwa karibu na Watanzania wanaoishi nje ya nchi kupitia balozi zake. 

Ameongeza kuwa Ubalozi wa Tanzania jijini London utaendelea kuwa kiungo muhimu kati ya serikali na Diaspora katika kuimarisha ushirikiano wa uwekezaji na maendeleo ya taifa. Akizungumza kwa niaba ya Diaspora, Bw. Hassan Khamis amemshukuru Prof. Kabudi kwa ziara yake na kwa kukutana na Watanzania wanaoishi nje ya nchi. 

Amesema ziara hiyo inaonesha dhamira ya serikali ya kuimarisha mawasiliano na Diaspora, huku akiahidi kuwa Watanzania waliopo ughaibuni wataendelea kushirikiana na serikali katika kuchangia maendeleo ya nchi yao.

 Katika mkutano huo, Profesa Kabudi aliambatana na Mshauri wa Rais katika masuala ya Diplomasia, Balozi Lazaro Nyalandu.

 Viongozi hao wapo nchini Uingereza kuhudhuria mikutano ya Jumuiya ya Madola pamoja na kushiriki majadiliano mbalimbali yanayolenga kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na maendeleo ya nchi wanachama.