Talaka yenu inawafunza nini watoto wenu?

Canada. Inakuwaje mtu anakuwa kiongozi mashuhuri, msomi aliyebobea au tajiri wa kutajwa, lakini anashindwa kuhimili ndoa yake? 

Je, ni suala la majaliwa, mipango mibovu au ukweli mchungu kwamba binadamu hawezi kuwa na kila kitu kwa wakati mmoja? 

Maswali haya yameendelea kuibuka kila tunaposikia habari za talaka katika familia zetu, hasa pale wahusika wanapokuwa watu wa hadhi na ushawishi mkubwa.

Katika tafakuri ya maisha ya ndoa na talaka, tulikumbana na tukio lililotuacha na maswali mengi kuliko majibu. Marafiki zetu, wanandoa wa ndoa ya mke mmoja, walipotutembelea kwa lengo la kulala nyumbani kwetu, tuliwaandalia vyumba vitatu—kimoja chao, na viwili vya watoto wao wa jinsi tofauti. 

Kwa mshangao wetu, walituomba tuwape vyumba viwili tu. Watoto wa kike wangelala na mama yao, na wa kiume na baba yao.

Hatukupinga, lakini tulibaki na mshangao. Baadaye, tulipowatembelea kwao, nao walitupangia vyumba viwili badala ya vitatu.

Walipotueleza kuwa kwa kawaida hawalali mume na mke chumba kimoja, tulibaki midomo wazi. Uchunguzi wetu wa kirafiki ulibaini kuwa walirithi utaratibu huo kutoka kwa wazazi wao waliokuwa katika ndoa za mitala, wakiishi kwenye boma moja lenye vijumba tofauti. Baba alikuwa na chumba chake; wake walimfuata kwa zamu.

Lakini je, kwa nini wanandoa hawa wa mke mmoja waliendeleza utaratibu huo bila kuhoji? Jibu lao lilikuwa rahisi: “Tulikuta hali hii.” Hapo ndipo swali kubwa linapozaliwa—watoto hujifunza nini kutoka kwa wazazi wao?

Funzo la kwanza ni kwamba watoto huathiriwa sana na matendo ya wazazi wao kuliko maneno yao. Wanaona, wanaiga na kuhalalisha. Pili, si kila mila au desturi inayorithiwa huhojiwa kwa kina. 

Wapo wanaofuata walivyokuta bila kuchunguza mantiki au madhara yake.

Tukirejea kwenye talaka, hali huwa nzito zaidi. 

Mtoto anayekulia kwenye familia iliyovunjika anaweza kuichukulia talaka kama jambo la kawaida, akiona si tatizo kubwa kuvunja ndoa pale mambo yanapokwenda kombo. 

Wengine, kinyume chake, huichukia talaka kiasi cha kuogopa hata kuingia kwenye ndoa.

Tunayo mifano hai. Rafiki yetu mmoja, tajiri wa kupigiwa mfano, alitalikiwa na mkewe. Wana watoto wanne, wote watu wazima. Kati yao, ni mmoja tu aliyeingia kwenye ndoa.

Wengine huepuka kabisa mjadala wa ndoa wanapokuwa na baba yao. Hawapendi hata kutaja majina ya wazazi wao kwa pamoja.

Baba huyo anaishi na hofu isiyoisha—kuwa talaka yao imewaathiri watoto kwa namna isiyoonekana kwa macho.

Kwa mujibu wa wataalamu wa uhusiano na saikolojia, madhara ya talaka hayaishii kwenye mgawanyiko wa mali au malezi. 

Huzaa msongo wa mawazo, chuki zilizofichika, hasira, hofu ya kujitoa kwenye uhusiano na hata upweke wa kudumu. Mtoto hujikuta katikati ya mvutano akae na nani? Ampende nani zaidi?

Hii haimaanishi kuwa kila ndoa lazima idumu kwa gharama yoyote. Zipo ndoa zenye mateso na ukatili ambako talaka huwa suluhisho la mwisho. 

Lakini swali la msingi hubaki: tunawafundisha nini watoto wetu tunapovunja ndoa? Je, tunawapa somo la ujasiri wa kuondoka kwenye mateso au la kukimbia changamoto?

Jamii inapaswa kutafakari. Maamuzi ya watu wazima huacha alama kwenye nafsi za watoto. Kama ilivyo kwa mila zinazorithiwa bila kuhojiwa, vivyo hivyo talaka inaweza kurithiwa kama mtazamo au hofu.

Ni muhimu kwa wazazi, kabla ya kufikia uamuzi wa talaka, kujiuliza si tu kuhusu wao, bali pia kuhusu kizazi wanachokilea. Maana mwishowe watoto hujifunza zaidi kutokana na tunavyoishi kuliko tunavyosema.

Talaka si tukio la watu wawili pekee. Ni somo linaloandikwa kwenye maisha ya watoto. Na somo hilo, huendelea kusomwa kwa vizazi.