Mtwara. Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema Serikali imewekeza Sh704 milioni za kufunga transfoma ya ziada katika Kituo cha Kupooza Umeme cha Mahumbika mkoani Lindi ili kupunguza changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara Lindi na Mtwara.
Aidha, waziri huyo amempa siku 14 mkandarasi anayetekeleza mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Songea hadi Mahumbika kupitia Tunduru na Masasi kurejea eneo la mradi na kuendelea na kazi mara moja.
Ndejembi ametoa maagizo hayo jana Jumamosi, Machi 7, 2026 kwa nyakati tofauti kwenye ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Ndejembi amesema kufungwa kwa transfoma hiyo ni jitihada za muda mfupi za Serikali katika kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi wa mikoa hiyo.
Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi akikagua maendeleo ya kituo cha kupooza umeme cha Mahumbika mkoani Lindi.
“Pamoja na jitihada hizi za muda mfupi, bado kuna mradi mkubwa wa kusafirisha umeme kutoka Songea kupitia Tunduru hadi Masasi na hatimaye kufika Mahumbika, ambao utaongeza nguvu ya upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara,” amesema.
Amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya kuimarisha miundombinu ya umeme katika ukanda huo, ikiwamo mradi wa kusafirisha umeme kutoka Mkuranga kupitia Somanga, Kilwa hadi Lindi, ambao utaunganishwa na miundombinu ya kusambaza umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Aidha, Ndejembi amelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa kuhakikisha makandarasi waliotekeleza ujenzi wa kituo hicho ni wazawa kutoka ndani ya taasisi hiyo.
Amesema pia Serikali ina mpango wa kuhakikisha kila wilaya inakuwa na kituo chake cha kupooza umeme ili kupunguza changamoto za kukatika kwa umeme zinazosababishwa na hitilafu katika maeneo mengine.
“Hatutaki tena hali ya umeme kukatika Mtama kwa sababu ya hitilafu iliyotokea Lindi Mjini au Nachingwea. Lengo ni kuhakikisha kila wilaya inapata substation yake na haya ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.
Miundombinu ya mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Songea hadi Mahumbika kupitia Tunduru na Masasi ambayo Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amemtaka mkandarasi kurejea eneo la mradi kuuendeleza.
Meneja wa mradi wa kuongeza transfoma katika Kituo cha Mahumbika, Joseph Efrem amesema kufungwa kwa transfoma mpya yenye uwezo wa 15 MVA kumeongeza uwezo wa kituo hicho kufikia takribani MVA 35.
Amesema hatua hiyo itaongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme na kusaidia kuimarisha shughuli za kiuchumi kwa wananchi wa mikoa ya Lindi na Mtwara.
Katika hatua nyingine, Waziri Ndejembi akiwa wilayani Tunduru, Mkoa wa Ruvuma, ametoa siku 14 kwa mkandarasi anayetekeleza mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Songea hadi Mahumbika kupitia Tunduru na Masasi kurejea eneo la mradi na kuendelea na kazi mara moja.
Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia kutoridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya Kalpataru Projects International Limited, ambayo ina jukumu la kujenga vituo vya kupoza umeme katika wilaya za Tunduru, Masasi na Mahumbika.
Miundombinu ya mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Songea hadi Mahumbika kupitia Tunduru na Masasi ambayo Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amemtaka mkandarasi kurejea eneo la mradi kuuendeleza.
Amesema mkandarasi huyo hapaswi kupewa kazi nyingine yoyote ya Serikali hadi atakapokamilisha mradi huo ambao utekelezaji wake umechelewa kinyume na masharti ya mkataba.
Pia, amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati kumuandikia barua ya onyo mkandarasi huyo, akieleza tayari walikutana na uongozi wa kampuni hiyo jijini Dodoma na kukubaliana kuwa wangeanza kazi ndani ya siku 25 baada ya kulipwa fedha walizokuwa wanadai tangu Desemba 2025.
Hata hivyo, amesema hadi sasa mkandarasi huyo hajarejea katika eneo la mradi wala kuanza kazi.
“Huyu mkandarasi anafanya kazi kwa kusuasua sana. Walilipwa fedha mwezi Desemba na tukakubaliana ndani ya siku 25 wawe wamerudi site na kazi ianze, lakini muda wote umeisha na hakuna kinachoendelea,” amesema Ndejembi.
Ameserma mradi huo ulipaswa kukamilika ndani ya kipindi cha miaka miwili na kukabidhiwa mwishoni mwa mwaka huu, lakini hadi sasa utekelezaji umefikia takribani asilimia 50 pekee.
Amesema mradi huo ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kuunganisha mikoa ya kanda ya kusini ambayo ni Ruvuma, Lindi na Mtwara kwenye gridi ya Taifa ili kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika.
“Wananchi wa kusini wanahitaji umeme wa uhakika na Serikali imeweka kipaumbele katika kutatua changamoto hiyo kwa kutoa fedha za kutekeleza mradi huu. Haiwezekani mkandarasi akachelewesha kazi hii,” amesema.
“Baada ya onyo tutakalompa, endapo ataendelea kusuasua tutachukua hatua zaidi.”