Moshi. Wakati tafiti zikionesha asilimia 30 ya watu wanaougua matatizo ya moyo wanatoka Kanda ya Kaskazini, Hospitali ya KCMC, mkoani Kilimanjaro imepanga kutumia Sh25 bilioni kujenga kitengo cha matibabu ya moyo katika hospitali hiyo, kitachokuwa taasisi ya pili kwa ukubwa nchini.
Ujenzi wa kitengo hicho unalenga kuboresha huduma za matibabu ya magonjwa ya moyo katika ukanda huo na maeneo ya jirani.
Kesho, Machi 9, 2026, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Alex Malasusa ataongoza ibada maalumu ya maadhimisho ya miaka 55 tangu kuanzishwa kwa hospitali hiyo, huku Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa akitarajiwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo hilo.
Akizungumzia ujenzi huo leo Jumapili Machi 8, 2026 umefikia asilimia 35, ofisa uhusiano wa hospitali hiyo, Gabriel Chisseo amesema: “Moja ya kazi kubwa ambayo tunaifanya katika miaka 55 ni uanzishwaji wa huduma mpya, kwa upande wa Kanda ya Kaskazini kumekuwa hakuna matibabu ya moyo, yanaweza yakawepo lakini sio kwenye kiwango cha ubingwa bobevu na kwenda kwenye ngazi ambazo ni kubwa zaidi.”
“Takwimu mbalimbali ambazo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya mashirika ya afya na wenzetu wanaotoa huduma nje ya Kanda ya Kaskazini ni kwamba asilimia 30 mpaka 40 watu wenye magonjwa ya moyo wanatoka Kanda ya Kaskazini kwa hiyo hili ni tatizo na ni changamoto kubwa,”amesema Chisseo.
Jengo la kitengo maalumu cha matibabu ya moyo, KCMC ambalo linatarajia kugharimu zaidi ya Sh25 bilioni.
Amesema moja ya kazi kubwa na dhamana waliyopewa ya afya ni kuhakikisha wanajibu hoja ya changamoto za wananchi wanaowazunguka ambao wanategemea hospitali hiyo kwa kutoa matibabu stahiki kwa jamii.
“Hivyo, tumeanza ujenzi wa taasisi ya pili ya moyo Tanzania hapa KCMC.Tulishaanza na tunatarajia mwakani Januari ujenzi huu wa utakuwa umekamilika, kwa sasa ujenzi umeanza kwa asilimia 35 na unagharimu Sh25 bilioni,”amesema Chisseo.
Akizungumzia ujenzi wa kitengo hicho cha moyo, mmoja wa wananchi wa mkoa huo, Philipina Kimario amesema itawapunguzia gharama kubwa za kusafiri na kupata huduma kwa wakati.
“Mimi hapa nina mjukuu wangu ana shida ya moyo kusafiri kwenda Dar es Salaam kila mara inakuwa ni changamoto sana hasa kwenye suala la nauli, wakati mwingine huna fedha ya kwenda huko JKCI, ni mpaka uanze kuomba mchango, hiki kitengo kikiwepo hapa kitakuwa na manufaa makubwa sana,”amesema.
Mkazi mwingine wa mkoa huo, Agapith Tesha amesema uwepo wa kitengo hicho cha moyo mkoani hapo utasaidia wagonjwa wengi kupata huduma karibu bila kulazimika kusafiri umbali mrefu kwenda Dar es Salaam.