Kigoma. Mkazi wa jijini Mbeya Nickolaus Komba (30), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, akikabiliwa na makosa manne, likiwamo la kujifanya Ofisa wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) na kuwatapeli watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kakonko.
Mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Machi 6, 2026 mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma, Aristida Tarimo huku Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Flora Lucas akisaidiana na Nestory Kayula.
Imeelezwa mahakamani hapo kuwa, mshitakiwa aliwadanganya watumishi hao waliokuwa na mikopo ya HELSB.
Kosa la pili mtuhumiwa alighushi barua kwa mtumishi wa Halmashauri ya Kakonko kinyume cha kifungu cha sheria 333,335(a) 337 ya kanuni ya adhabu.
Kwa mujibu wa waendesha mashtaka, mtuhumiwa huyo anakabiliwa na kosa la tatu la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu chini ya kifungu cha 302 cha kanuni ya adhabu.
“Mshitakiwa anakabiliwa na makosa manne kwa jumla na kosa la nne ni la utakatishaji fedha chini ya kifungu cha 12(1)(d)(e) na 13(1)(a) cha sheria ya uthibiti wa utakatishaji fedha sura 423 marejeo 2023,”amesema mwendesha mashtaka Lucas.
Mtuhumiwa hakutakiwa kujibu lolote kwa kwasababu ya Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi hiyo na mtuhumiwa alirudishwa mahabusu hadi Machi 19, 2026 kwa hatua inayofata.