Mbeya. Kufuatia kuwepo kwa changamoto ya baadhi ya wazee kuishi mazingira magumu kwa kukosa makazi bora, mbunge wa Uyole Dk Tulia Ackson ameeleza mpango wake wa kujenga nyumba 13 katika kila kata jimboni kwake ili kuwarejeshea tabasamu.
Dk Tulia amesema hatua hiyo ni kuikumbusha jamii kuwa na utaratibu wa kusaidia makundi hayo na wasione jambo la kawaida kufurahia tabu,mateso na shida kwa watu wengine.
Kauli hiyo ameitoa katika Mtaa wa Itongo Kata ya Mwakibete leo Jumamosi Machi 7, 2026, wakati akikabidhi nyumba kwa kikongwe Tuli Mwantindili (80), ambayo imejengwa kupitia Taasisi ya Tulia Trust kupitia kampeni ya “Tulia Trust mtaani kwetu.”
Awali Mwantindili, mkewe na mtoto wake mmoja mwenye tatizo la afya ya akili walikuwa wakiishi kwenye nyumba chakavu iliyoezekwa kwa karatasi laini kuzuia mvua kutokana na uchakavu wa bati.
“Sisi kama sehemu ya jamii tusione jambo la kawaida mtu akiwa na dhiki,tabu,kuteseka ni vyema kusaidia na sio kuongeza maumivu kwa kusema vibaya,”amesema.
Dk Tulia ameomba jamii kujitoa kusaidia wahitaji hususani kwenye familia hiyo ya watu watatu ambao licha ya kupata makazi wamekuwa na changamoto ya kiafya jambo ambalo linahitaji msaada wa hali na mali.
“Tunamuona Mzee wetu afya yake sio njema ,lakini pia binti yake naye ana changamoto ya mguu na afya ya akili sisi tumejenga nyumba, lakini bado wanahitaji misaada ya hali na mali kutoka kwenu ninyi ,”amesema.
Familia iliyojengewa nyumba baada ya kuishi kwenye makazi yasiyo salama kwa kuziba karatasi laini juu ya bati kuzuia maji ya mvua na jua. Picha na Hawa Mathias
Kuhusu mkakati ujenzi makazi
Dk Tulia amesema mikakati yake ni kujenga nyumba 13 katika kila kata kugusa wazee waishio mazingira magumu kwa lengo la kurejesha la kuwawezesha kuishi kama jamii nyingine kwa kuheshimika
“Ndugu zangu wana Mwakibete niombeeni Mwenyezi Mungu anipe uzima lengo langu ni kujenga nyumba 13 kila kata, lakini nashangazwa watu wanaosema kwanini wahitaji kupigwa picha na vyombo vya habari kutangaza,”amesema.
Dk Tulia amesema sababu ya kuwatangaza na kuwapiga picha ni kuikumbusha jamii kuguswa kusaidia kundi hilo na sio kufurahia kwa kuwasema vibaya.
“Nitafanya haya kuwakumbusha kutoa ushirikiano kwa watu wenye mazingira magumu na sio kugeuka sehemu ya kuongeza maumivu, lakini sitoishia kujenga nyumba moja ama mbili kwenye Jimbo la Uyole, “amesema
Mkazi Mtaa wa Itongo Imelda Kyando (45), amesema amepokewa na familia hiyo mwaka 2008, mazingira ya maisha yao yalikuwa magumu hususani katika nyumba waliyokuwa wakilala yeye, mumewe na binti yao mwenye shida ya afya ya akili.
“Kwa kweli nyumba yao haikuwa salama ilikuwa chakavu kiasi kwamba walikuwa wakilazimika kuweka makaratasi laini nje ya bati na kwenye vitanda kuzuia maji ya mvua kuingia ndani,”amesema.
Kikongwe Tunu Mwantindili (80), (kulia) akimtazama Mbunge wa Uyole, Dk Tulia Ackson kabla ya kukabidhiwa nyumba iliyojengwa kupitia Taasisi ya Tulia Trust katika kampeni ya “Tulia Trust mtaani kwetu “.Picha na Hawa Mathias
Amesema kimsingi wanamshukuru mbunge wao Dk Tulia kwa kuifuta machozi familia hiyo na jamii inayo wazunguka kwani haikuwa rahisi kurejeshewa matumizi kuishi sehemu salama.
Msimamizi wa Kata ya Mwakibete kupitia Taasisi ya Tulia Trust, Haruna Kasale amesema maisha ya familia hiyo yalikuwa yakitegemea biashara ya kukusanya na kuuza mikopo, kuni na vibarua mashambani.
“Tulipata taarifa ya familia hiyo ambapo tuliwasiliana na diwani wa kata husika kupata uhalisia wa maisha yao jambo ambalo lilibarikiwa kulingana na vigezo vyetu,”amesema.
Diwani wa Mwakibete, Lucas Mwampiki amesema: “Hatuna mengi ya kusema umegusa mioyo ya wananchi wengi wa Mbeya ambao walikata tamaa kutokana na hali ya maisha.”