Wanaodaiwa kumteka Mtanzania Kenya wasota mahabusu siku 16

Dar/Nairobi. Mahakama nchini Kenya, kesho itatoa uamuzi wa iwapo raia wawili wa Kenya na Mtanzania wanaotuhumiwa kufanya jaribio la kumteka mwanaharakati wa Tanzania, Mshabaha Hamza, waachiwe kwa dhamana ama la.

Katika jaribio hilo la utekaji ambalo lilishindikana, lililotokea Februari 22, 2026 huko Kaunti ya Machakos katika ardhi ya Kenya, watuhumiwa wanadaiwa kumchoma sindano mwanaharakati huyo kabla hajaokolewa na polisi wa nchi hiyo.

Washitakiwa katika shauri hilo la jinai ni Edward Mwangi ambaye ni raia wa Kenya anayeishi Afrika Kusini, Nelson Wanjohi, raia wa Kenya na aliyekuwa dereva wa gari lililombeba Mshabaha na raia wa Tanzania, Aziz Hamad.

Watuhumiwa hao walifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Mahakama ya Mavoko, Martha Nazushi Februari 23, 2026 upande wa mashitaka uliomba muda zaidi wa kuwashikilia ili kukamilisha upepelezi.

Hakimu Nazushi alikubali ombi hilo na kutoa muda wa siku 10 kwa washitakiwa kuendelea kushikiliwa na polisi lakini baada ya siku hizo kumalizika, upande wa mashitaka uliomba kuongezewa muda na kesi hiyo sasa itatajwa Machi 9, 2026.

Siku hiyo, Mahakama itaamua iwapo waachiwe kwa dhamana ama la na mpaka sasa haijawekwa wazi dhamira ya watuhumiwa hao ilikuwa ni nini na walikuwa wanampeleka wapi na kwa malengo gani.

Tukio la utekaji lilivyokuwa

Kulingana na taarifa zilizowasilishwa mahakamani, Mshabaha alitekwa na watu watatu Februari 22,2026 waliomshambulia kwa kumpiga na kumchoma sindano yenye kemikali ambazo bado hazijathibitishwa ni aina gani.

Hata hivyo, akiwa ndani ya gari hilo, aliendelea kupambana kujaribu kuokoa maisha yake na ndipo watekaji wake walipomtupa eneo la Lukenya na taarifa za tukio hilo zikiwa tayari zimewafikia polisi wa vituo vya Lukenya na Kyumbi.

Kwa kushirikiana na maofisa wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) nchini Kenya na polisi wa vituo hivyo viwili, walifanikiwa kulisimamisha gari hilo na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao watatu.

Tukio hilo la utekaji kwa Mtanzania katika ardhi ya Kenya ni la pili, baada ya jaribio lingine kama hilo kufanywa kwa mwanaharakati Maria Sarungi Januari 12,2026 kabla ya watekaji kumwachia kutokana na kupambana nao ndani ya gari.

Maria Sarungi ambaye mbali ya kuwa ni mwanaharakati, pia ni mwandishi wa habari ambaye yeye pamoja na Mshabaha, wamekuwa wakiendesha mijadala ya kisiasa katika jukwaa la Maria Space katika mtandao wa X zamani Twitter.