Unguja. Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar (ZFDA) umeteketeza kilo 2,447 za nyama mchanganyiko baada ya kubainika kuwa hazifai kwa matumizi ya binadamu.
Akizungumza baada ya kuteketeza nyama hizo leo Jumapili Machi 8, 2026 katika jaa kuu la Serikali Kibele, Daktari wa Mifugo wa ZFDA, Thamra Khamis Salum amesema bidhaa hizo ziliingizwa nchini na Kampuni ya Next Level Millenium Supply.
Amesema baada ya mzigo huo kuwasili, mamlaka hiyo ilichukua sampuli za bidhaa hizo na kuzifanyia vipimo katika maabara yake, matokeo yalionesha hazifai kwa matumizi.
“Bidhaa zilizoteketezwa ni nyama mchanganyiko ikiwamo ya ng’ombe, nguruwe na kondoo, mzigo huu uliingizwa nchini kupitia Bandari ya Malindi na sampuli 13 zilichukuliwa na kufanyiwa uchunguzi,” amesema.
Amefafanua kuwa, kati ya sampuli hizo, saba zilibainika kuwa hazifai kwa matumizi ya binadamu huku sita zikionekana kuwa bado zinaweza kutumika ingawaje Mamlaka haikutaka kuziwacha ziingizwe sokoni.
Daktari huyo, amewataka wafanyabiashara kuhakikisha kuwa wanahifadhi vyema bidhaa zao wakati wa kusafirisha kwa kuziweka katika mazingira yenye baridi ya kutosha, huku akibainisha kuwa bidhaa za nyama huharibika haraka zinapokosa hifadhi sahihi.
Pia, amesema ZFDA inaendelea kufanya ukaguzi katika maeneo ya forodha na madukani kwa lengo la kuhakikisha bidhaa zinazoingizwa na kuuzwa bado ziko ndani ya muda wa matumizi, hatua inayolenga kulinda afya za wananchi.
Dk Thamra amesisitiza kwamba, mamlaka hiyo itaendelea kukamata bidhaa zote zitakazobainika kufeli vipimo vya maabara au zilizomaliza muda wa matumizi na kuchukua hatua za kuziteketeza pamoja na kuwatoza faini wafanyabiashara husika.
Mtendaji wa Kampuni ya Next Level Millenium Supply, Steven Lucas amekiri kuwa bidhaa hizo hazikufaa kwa matumizi ya binadamu kutokana na kufika kwa tarehe ya mwisho ya matumizi.
Vilevile, ametoa wito kwa wafanyabiashara wenzake kuingiza bidhaa zinazokidhi viwango vinavyotakiwa ili kuepuka hasara kama ilivyowapata wao.