Mwalimu Lihepanyama, mkemia anayekuza sayansi Sekondari Pugu

Dar es Salaam. Katika mazingira ya kihistoria ya Shule ya Sekondari Pugu Boys, jina la Mwalimu Venancia Lihepanyama (57) limeendelea kutajwa kama sehemu ya hadithi ya mafanikio ya mamia ya wanafunzi waliopitia mikononi mwake katika masomo ya sayansi.

Wengi wa wanafunzi hao leo ni madaktari, watafiti, wahandisi, walimu na wataalamu wa kada mbalimbali waliopata msingi wao wa sayansi kupitia ufundishaji wake wa somo la kemia.

Katika mahojiano maalum na Mwananchi, uongozi wa shule hiyo unasema mchango wa mwalimu huyo hauishii darasani pekee.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Pugu, Patrick Sinyinza, anasema mwalimu huyo ni sehemu muhimu ya malezi ya wanafunzi.

“Ni mwalimu wa muda mrefu tangu mwaka 1996. Lakini hapa Pugu si mwalimu tu wa kemia ni mama wa wanafunzi wote kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita,” anasema.

Kwa zaidi ya miongo miwili shuleni hapo, Mwalimu Lihepanyama amekuwa akifundisha kemia kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita, huku wakati mwingine akisaidia madarasa ya chini panapokuwa na uhitaji. Darasani anajulikana kwa nidhamu, kujituma na msisitizo wa kujifunza kwa vitendo zaidi kuliko nadharia.

“Ni mchapakazi na role model (kiigizo) kwa walimu wa sayansi, hasa wanawake. Wanafunzi wetu wengi walioko leo ni madaktari, watafiti, wahandisi na viongozi wamepita mikononi mwake na wote wanaomaliza Pugu asilimia 100 wanaenda vyuo vikuu na wanaenda zaidi ya digrii ya kwanza ni matunda yake kwakuwa amewajenga vizuri,” anasema Sinyinza.

Mwalimu wa Chemistry shule ya sekondari Pugu Boys, Venancia Lihepanyama akiwafundisha wanafunzi wa kidato cha sita ndani ya chumba cha mahabara ya shule hiyo iliyopo jijini Dar es salam.



Kwa zaidi ya miaka 20, Mwalimu Lihepanyama amekuwa sehemu ya historia ya mafanikio ya masomo ya sayansi nchini.

Akiwa mwalimu wa kemia katika Shule ya Sekondari Pugu, amesema ameshuhudia na kushiriki moja kwa moja katika safari ya kuwajenga wanafunzi kitaaluma, kimaadili na kifikra.

Alianza kazi ya ualimu mwaka 1996 katika Shule ya Sekondari Imamba, wilayani Kilosa Mkoa wa Morogoro, akiwa na stashahada ya ualimu.

Anasema kiu ya kujiendeleza kitaaluma ilimsukuma kujiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) mwaka 2000 kusomea Shahada ya Sayansi (BSc) katika masomo ya biolojia na kemia, hadi alipohitimu mwaka 2004.

Baada ya hapo, alijiunga na Shule ya Sekondari Pugu Novemba 2005, ambako amekuwa akifundisha kwa muda mrefu kidato cha tano na sita huku akisaidia pia madarasa ya chini inapohitajika.

Alipoulizwa nini kinachompa fahari zaidi katika kazi yake, anasema ni kuona mafanikio ya wanafunzi aliowafundisha.

“Wanafunzi wengi wamepita mikononi mwangu. Leo nikitembea hospitalini au taasisi mbalimbali nakutana nao wakiwa madaktari, wahandisi na wataalamu wa sekta tofauti,” anasema.

Anakumbuka tukio la kukutana na aliyekuwa mwanafunzi wake, Dk Michael Mwakyusa, alipokwenda Hospitali ya Mloganzila, jijini Dar es Salaam.

“Aliwaambia wenzake, huyu ni mwalimu wangu wa kemia. Wakanishukuru. Niliona kweli kazi ya mikono yetu inaonekana,” anasimulia.

Mbali na mafanikio ya wanafunzi wake, anasema anajivunia pia mchango wake katika kuimarisha ufundishaji wa majaribio ya maabara katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Kati ya mwaka 2010 na 2016, wakati kulipokuwa na uhaba wa wataalamu wa maabara shuleni, Serikali ilianzisha mpango wa kuwawezesha walimu wa sayansi kuandaa na kusimamia majaribio ya maabara.

Katika kipindi hicho, mwalimu Lihepanyama alikuwa miongoni mwa wawezeshaji waliotoa mafunzo kwa walimu wa kemia katika shule mbalimbali za mkoa huo.

“Leo hii si rahisi kukuta mwalimu wa kemia anashindwa kuandaa practical. Zamani kulikuwa na kuazimana (walimu) wakati wa mitihani, lakini sasa walimu wengi wana uwezo wa kusimamia majaribio kwa ufasaha,” anasema.

Mwalimu wa Chemistry shule ya sekondari Pugu Boys, Venancia Lihepanyama akiwafundisha wanafunzi wa kidato cha sita ndani ya chumba cha mahabara ya shule hiyo iliyopo jijini Dar es salam.



Kwa mtazamo wake, mafanikio ya Shule ya Sekondari Pugu, hasa katika masomo ya sayansi, yanatokana na mambo manne makuu; nidhamu, ushirikiano, kujituma na upendo.

“Masomo ya sayansi yana utaratibu wake na yanahitaji nidhamu. Lakini pia mwalimu anapaswa kumpenda mwanafunzi na mwanafunzi ampende mwalimu. Upendo ukitawala, kila kitu kinaenda sawa,” anaeleza.

Anasema wanafunzi wengi wanapoanza kidato cha kwanza huingia na dhana kwamba sayansi ni ngumu, hivyo jukumu kubwa la mwalimu ni kubadili mtazamo huo.

“Akifundishwa vizuri anaona kumbe ni kitu cha kawaida. Ndiyo maana wanafunzi wengi wanaobadilika kifikra huanza kujitengenezea ndoto zao mapema kuwa daktari, mhandisi au mtafiti,” anasema.

Hata hivyo, anabainisha changamoto katika ngazi ya A-Level, ambapo baadhi ya wanafunzi huingia wakiwa na alama nzuri za O-Level lakini bila kuongeza bidii.

“Mwanafunzi anakuja na A yake, anadhani itaendelea tu. Lakini A-Level inahitaji umakini mkubwa zaidi. Tunawahamasisha wasome kwa bidii na kuwajengea ujasiri kupitia maabara na mijadala ya makundi,” anasema.

Shule ya Sekondari Pugu imezalisha viongozi na wataalamu wengi waliolitumikia na wanaoendelea kulitumikia taifa.

Miongoni mwa waliowahi kusoma hapo ni hayati Benjamin Mkapa, Rais wa awamu ya tatu wa Tanzania, ambaye alifundishwa na hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Wengine ni pamoja na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda na Jaji Mkuu mstaafu, Augustino Lubuva.

Kwa kizazi cha sasa, Mwalimu Lihepanyama anawataja pia Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda; Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo; aliyekuwa Waziri wa Habari na Teknolojia, Jerry Silaa na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso.

“Aweso wakati anaingia hapa alikuwa mwanafunzi wangu, nimemfundisha na baadaye akaondoka,” anasema.

Hata hivyo, anasisitiza mafanikio makubwa kwake si tu kwa wanafunzi wenye majina makubwa, bali pia kwa wale wanaotumikia jamii kwa uadilifu.

“Wapo wengi ambao si maarufu, lakini ni waadilifu, wanyenyekevu na wanaitumikia nchi na wananchi kwa ufanisi. Huo ndiyo ushindi wetu.”

 Teknolojia fursa na tahadhari

Katika zama hizi za matumizi ya akili unde (AI), Mwalimu Lihepanyama anasema teknolojia inaweza kusaidia kurahisisha maandalizi ya vipindi na upatikanaji wa taarifa.

Hata hivyo, anasisitiza umuhimu wa mwalimu kufanya uchambuzi kabla ya kutumia taarifa hizo darasani.

“AI inaweza kusaidia, lakini mwalimu lazima achuje kwanza kabla ya kumpelekea mwanafunzi. Pia tusisahau kusoma vitabu.”

Anasema licha ya faida za teknolojia katika sayansi, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yamechangia kupungua kwa umakini wa wanafunzi na kushuka kwa maadili.

“Wengi hawafuati mazuri yaliyopo mtandaoni, wanafuata mabaya. Hilo linaathiri maadili na hata ari ya kujifunza.”

Kwa uzoefu wake wa muda mrefu, anasema kuna tofauti kubwa kati ya wanafunzi wa zamani na wa sasa.

“Zamani kulikuwa na nidhamu ya hali ya juu na ukaribu kati ya mwalimu na mwanafunzi ulikuwa wa mipaka. Leo mwalimu ana kazi kubwa ya kumfuatilia mwanafunzi mmoja mmoja.”

Anasisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya mzazi, mwalimu na mwanafunzi katika kuhakikisha mtoto anafaulu.

“Mabadiliko ni makubwa. Mtoto ana mambo mengi kichwani kutokana na utandawazi.”

Nini kifanyike kuboresha sayansi

Kwa mtazamo wake, Serikali inapaswa kuendelea kuwajengea uwezo walimu wa sayansi kwa mafunzo ya mara kwa mara kadri mbinu za ufundishaji zinavyobadilika.

Pia anasisitiza umuhimu wa kuajiri walimu zaidi ili kukabiliana na ongezeko la wanafunzi.

“Unaweza kukuta wanafunzi 700 wa kidato cha kwanza na mwalimu mmoja wa sayansi. Hiyo ni changamoto.”

Aidha, anashauri kuboreshwa kwa maslahi ya walimu wa sayansi ili kuongeza motisha.

“Zamani kulikuwa na allowance (posho) maalum kwa walimu wa sayansi na tulikuwa tunaona namna tulivyokuwa tunashindana kufundisha kwa ustadi mkubwa. Motisha ni muhimu,” anasema.

Kuhusu mabadiliko ya mtaala, anaona ni vyema utekelezaji wake ukaanza katika ngazi za chini na kuendelea hatua kwa hatua hadi juu.

Akiwa mwalimu wa kike aliyefundisha kwa muda mrefu wanafunzi wa kiume, anasema changamoto ya mitazamo ilijitokeza mwanzoni mwa kazi yake.

“Wakati naanza nilikuwa mdogo kiumri na kiumbo. Wanafunzi wengine walikuwa wakubwa kuliko mimi. Ilibidi nijenge heshima darasani kwa kuzungumza nao wazi kwamba mimi ni mwalimu na wao ni wanafunzi.”

Anasema walimu wa kike wana mchango mkubwa katika malezi ya wanafunzi kwa sababu mara nyingi wanakuwa karibu zaidi na changamoto za watoto.

“Mama anamfahamu mtoto kwa undani. Walimu wa kike wanajitoa sana wanakuwa walezi, washauri, wakati mwingine hata madaktari.”

Katika idara ya sayansi shuleni hapo, anasema walimu wa kike ni wengi kuliko wanaume, hali inayosaidia kuvunja mitazamo ya kijinsia kuhusu masomo ya sayansi.

“Hakuna somo la mwanamke au mwanaume. Wote tuna akili sawa.”

Anawahimiza wasichana kupenda sayansi na kujiamini.

“Hakuna kitu chepesi. Hata sheria ni ngumu kuliko sayansi. Waige mifano yetu. Wanawake tunaweza,”anasema.

Kwa walimu wanaoanza taaluma ya ualimu, Mwalimu Lihepanyama anatoa ujumbe mmoja: kufanya kazi kwa moyo na kujituma.

“Tunatengeneza madaktari, mainjinia, watafiti. Tusipofanya kazi kwa bidii, tutakuja kukutana na wataalamu wasiokuwa makini, na madhara yake yatafika hata kwetu,”anaeleza.

Anasisitiza kuwa masomo ya sayansi ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa.

“Kazi yetu ni ya kutengeneza jamii. Tufanye kwa moyo, kwa uadilifu na kwa upendo,”anasema.

Baada ya karibu miaka 30 ya ualimu, Mwalimu Lihepanyama bado anaendelea kusimama darasani kwa ari ile ile ya mwanzo, akiamini kuwa kila mwanafunzi anaweza kufanikiwa akipewa mwongozo sahihi, nidhamu na moyo wa kujituma.