LEO ni Siku ya Wanawake Duniani inayoadhimishwa kila ifikapo Machi 8 ya kila mwaka, tangu ilipoadhimishwa 1975 baada ya Umoja wa Mataifa (UN), kuridhia ili kuhamasisha usawa wa kijinsia, haki za wanawake na mchango wao katika jamii.
Kwa mashabiki wa Simba na Yanga, ni ngumu kuisahau siku hii ya Wanawake, kwa sababu ni mara mbili tu timu hizo zimewahi kukutana siku kama ya leo katika mechi za Ligi Kuu Bara, huku kila upande ukitoka na ushindi.
Jambo la kushangaza mechi hizo zote mbili zina maajabu yanayofanana kiasi cha kuifanya Siku ya Wanawake iwe ya kipekee kwa miamba hiyo, hata kama baadhi ya mashabiki kindakindaki wanaozifuatilia na kuzipenda kuzishabikiwa wao wameshasahau.
Timu hizo zilikutana kwa mara ya kwanza Machi 8, 2015 na Simba kushinda bao 1-0 ikiwa ni baada ya kusota kwa takribani mechi tano mfululizo bila ya kuibuka na ushindi, tangu ilipoifunga Yanga kwa mabao 5-0, mechi iliyopigwa, Mei 6, 2012.
Mechi hiyo iliyopigwa Jumapili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini, Dar es Salaam, shujaa wa Simba aliyepeleka kilio kwa Yanga alikuwa ni nyota aliyezichezea timu hizo zote mbili, Mganda, Emmanuel Okwi, aliyepiga shuti kali dakika ya 52.
Baada ya hapo, ilipita tena miaka mitano kabla ya Yanga kujibu mapigo kwa kulipa kisasi katika siku kama ya leo ya Machi 8, 2020, ilipoifunga Simba bao 1-0, mechi iliyochezwa siku ya Jumapili, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Shujaa wa Yanga katika mechi hiyo alikuwa ni Mghana, Bernard Morrison, aliyezichezea pia timu zote mbili, ambapo alifunga kwa frii-kiki kali dakika ya 44, baada ya aliyekuwa kiungo wa Simba, Jonas Mkude, kumfanyia madhambi nje ya eneo la 18.
Mechi hiyo, itabakia katika kumbukumbu ya wadau wa soka nchini, kwa sababu ilihudhuriwa na aliyekuwa Hayati Rais John Magufuli na aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Ahmad Ahmad.
Ushindi huo kwa Yanga uliamsha morali kwa kikosi hicho baada ya kuvunja unyonge wa kucheza mechi saba mfululizo za Ligi Kuu bila ya kushinda dhidi ya Simba, tangu mara ya mwisho iliposhinda mabao 2-0, pambano lililopigwa, Februari 20, 2016.
Mechi iliyochezwa siku ya Wanawake na Simba kushinda bao 1-0, mwaka 2015, ilikuwa ya marudiano baada ya raundi ya kwanza kutoka suluhu ya (0-0), ikiwa ni ya msimu wa 2014-2015, Kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Oktoba 18, 2014.
Hata mechi ambayo Yanga ililipa kisasi cha bao 1-0, mwaka 2020, ilikuwa pia ni ya marudiano msimu wa 2019-2020, baada ya raundi ya kwanza miamba hiyo kufungana mabao 2-2, pambano lililopigwa Januari 4, 2020, Kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Jambo la kushangaza zaidi ni kwamba, Simba ilishinda mechi ya Machi 8, ikiwa ni pambano la 94 la ‘Kariakoo Derby’, huku kwa upande wa Yanga ikishinda mechi ya Siku ya Wanawake ikiwa ni ya 104, kwao kukutana katika Ligi Kuu Bara tangu 1965.
Katika misimu yote, Simba licha ya kuifunga Yanga ila haikubeba ubingwa msimu wa 2014-2015, kwani taji lilienda Jangwani sawa na ilivyotokea kwa Yanga iliyoshinda mwaka 2020 na kutoka kapa msimu wa 2019-2020, kufuatia ubingwa kutua Msimbazi.
Kwa rekodi hizo kabambe na mfanano wa matukio ya mechi hizo mbili za watani wa jadi kwa hapa nchini zilizopigwa ndani ya Machi 8, inatosha kusema kwamba, Siku ya Wanawake inashangaza kwa vigogo hao ingawa, matokeo yao ni Simba 1-1 Yanga.