Serengeti. Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Mbeya imetupa rufaa iliyowekwa na Braison Sanga, aliyekuwa akipinga hukumu ya kifungo cha miaka 30 jela baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la unyang’ang’anyi wa kutumia silaha.
Braison Sanga na wenzake wawili, ambao si warufani, walidaiwa kuiba bunduki mali ya Gereza la Songwe.
Watuhumiwa hao walitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 287A cha Kanuni ya Adhabu.
Tukio hilo liliripotiwa kutokea mwaka 2013, mrufani na wenzake waliiba bunduki ya Gereza la Songwe yenye namba TZPS 39847164020 (SAR), ambayo ni mali ya Serikali ya Tanzania.
Baada ya wizi huo, walidaiwa kutumia panga kumshambulia askari B.5709 WDR Ambrose, aliyekuwa na bunduki hiyo na kumpora mali hiyo.
Mahakama ilibaini kuwa ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka ulikusanya vipengele vinavyomuhusisha mrufani na tukio, ikiwamo ushahidi wa mashahidi na vilelezo vilivyopatikana katika chumba cha mrufani.
Hukumu iliyotupilia mbali rufaa hiyo imepatikana kwenye mtandao wa Mahakama, imetolewa Machi 6, 2026 na Jaji Musa Pomo, aliyekuwa akisikiliza Rufaa hiyo ya jinai namba 10228/2025, ambapo mrufani huyo alikuwa akipinga hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Mbeya.
Katika hukumu yake, Jaji Pomo alieleza kuwa Mahakama Kuu, kama Mahakama ya kwanza ya rufaa, ina wajibu wa kupitia upya ushahidi wote uliowasilishwa katika Mahakama ya chini.
Baada ya kufanya tathmini hiyo, Mahakama ilibaini kuwa mwathirika wa tukio hakuwatambua washambuliaji wake kutokana na giza lililokuwepo eneo la tukio.
Jaji alieleza kuwa, upande wa mashtaka uliwasilisha ushahidi mwingine uliomhusisha mrufani na tukio hilo.
Miongoni mwa ushahidi huo ni pamoja na kukiri kwa mdomo kulikodaiwa kufanywa na mrufani mbele ya viongozi wa kijiji na mashahidi wengine.
Mahakama ilieleza kuwa kukiri kwa aina hiyo kunakubalika kisheria pale kunapofanywa mbele ya mashahidi wanaoaminika.
Aidha, ushahidi ulionesha kuwa panga lililotumika katika shambulio hilo lilipatikana katika chumba cha mrufani baada ya polisi kufanya upekuzi.
Mahakama ilibainisha kuwa mrufani hakupinga ushahidi huo wakati mashahidi walipotoa maelezo yao mahakamani.
Kwa mujibu wa sheria ya ushahidi, kushindwa kumhoji shahidi kuhusu jambo fulani kunachukuliwa kama kukubaliana na maelezo ya shahidi huyo.
Kuhusu utetezi wa mrufani, Jaji amesema kuwa Mahakama pia ilitathmini hoja yake kwamba hakutambuliwa katika eneo la tukio.
Hata hivyo, utambuzi huo haukuwa msingi pekee wa upande wa mashtaka kuthibitisha kosa, kwani kulikuwepo ushahidi mwingine unaomunganisha mrufani na tukio hilo.
Kwa sababu hiyo, Mahakama iliona kuwa utetezi wa mrufani haukuwa na uzito wa kuondoa ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka.
Baada ya kupitia hoja zote za pande zote, Mahakama Kuu ilihitimisha kuwa upande wa mashtaka ulikidhi ushahidi wa kutosha kuthibitisha kosa hilo bila shaka yoyote na hivyo kutupilia mbali rufaa hiyo.
“Kwa sababu hizo, rufaa ya mrufani haina msingi na inatupiliwa mbali,” amesema Jaji Pomo katika hukumu yake.