Moshi. Mbunge wa Moshi Mjini (CCM), Ibrahim Shayo amesema ajali aliyopata Februari 18, 2026 haikuhusisha mkono wa mtu kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakidai.
Shayo amesema chanzo cha ajali hiyo ni kupasuka kwa tairi la mbele la gari walilokuwa wakisafiria, hali iliyosababisha dereva kushindwa kulimudu kutokana na gari hilo kuwa katika mwendo mkali.
Ameyasema hayo leo, Machi 8, 2026 wakati akizungumza na wananchi wa jimbo hilo, katika viwanja vya stendi ya mabasi mjini Moshi ambapo amewashukuru kwa kumuombea dua. “Nimekuja kwenu leo kutoa neno la shukurani, asiyeweza kumshukuru Mwenyezi Mungu hata mwanadamu mwenzake hawezi kumshukuru. Nasema asante kwa ajili ya sala zenu na dua zenu, mmelia na mimi mmeomba na mimi na kama sio maombi yenu, dua zenu na sala zenu nisingetoka kwenye lile gari kwa namna lilivyoharibika.”
“Kwenye ile ajali iliyotokea tukiwa kwenye msafara wa Waziri Mkuu, maneno mengi yalisemwa lakini nataka niwaambie ukweli, tairi la mbele lilipasuka, hivyo lazima gari liende pembeni kwa sababu lilikuwa spidi 160 maana yake ni nini lazima gari lianguke,” amesema mbunge Shayo.
Mbunge wa Moshi mjini(CCM), Ibrahim Shayo akizungumza na wananchi wa Jimbo hilo (hawapo pichani) katika stendi ya mabasi Moshi mjini .
Amesema, “Mkono wa mtu unatoka wapi hapo, yaani wewe hujala siku mbili huna hela halafu unalalamika eti ninalogwa kwa sababu nina njaa, una njaa si hujala? Umelogwaje wakati una njaa hujala.
“Nataka niwaambie na huu ni mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni kwamba ile ajali ilikuwa ni mitihani ya Mwenyezi Mungu, naamini Mwenyezi Mungu ameninusuru na ile ajali, amenirudisha, amejua kabisa waliomchagua Ibra kuna kazi hazijaisha. Na mimi nimerudishwa nimalizie kazi zenu,” amesema mbunge Shayo.
Pamoja na mambo mengine, mbunge huyo amesema hivi karibuni mji wa Moshi, hususani maeneo ya stendi ya mabasi, kutawekwa taa ili wafanyabiashara wafanye kazi usiku na abiria wanaoshuka katika stendi hiyo wasikumbane na changamoto.
“Wakati naomba ridhaa ya kuwatumikia, niliongea kwa uchungu sana na nikasema lazima tuibadilishe Moshi iwe mpya, sasa habari njema ni kwamba stendi yetu inaenda kuwaka taa ndani, maeneo yote yanayozunguka Round About tunaenda kuweka taa ndani, Moshi itakuwa na mabadiliko makubwa sana,” amesema mbunge huyo.
Baadhi ya wananchi wakimsikiliza Mbunge wa Moshi mjini (CCM), Ibrahim Shayo wakati alipokuwa akiwashukuru katika mkutano wa hadhara ambao umefanyika katika stendi hiyo.
Akizungumza kuhusu uwekaji wa taa katika Manispaa ya Moshi, Meya wa Manispaa hiyo, Zuberi Kidumo, amesema kuwa kuanzia Jumatatu wiki ijayo, shughuli ya kuweka taa za barabarani inaanza rasmi.
“Mungu akijalia, wiki ijayo tutaweka taa katika mji wote wa Moshi. Tutaanza kwa kuweka taa kuanzia YMCA, mzunguko wa stendi ya Mboya, mpaka Nelson Mandela pamoja na baadhi ya mitaa mingine, kuhakikisha watu wanaweza kufanya kazi hadi usiku,” amesema Kidumo.
Amesema kwa sasa halmashauri hiyo imeweza kukusanya Sh12 bilioni kwa mwaka huu wa fedha unaoisha tofauti na Sh6 bilioni zilizokuwa zikikusanywa hapo awali katika baraza la madiwani lililopita.