Arusha. Vitendo vya unyanyapaa dhidi ya wanawake waliowahi kutumia dawa za kulevya vimeelezwa kuwa miongoni mwa vikwazo vinavyowazuia kupata tiba stahiki na kurejea katika maisha ya kawaida ndani ya jamii.
Hayo yameelezwa na Kamishna Msaidizi wa huduma za ustawi na mwitikio wa jamii kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Sara Ndaba wakati akitoa elimu kuhusu madhara ya matumizi ya dawa za kulevya kwa wanawake na wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani.
Ndaba amesema kuwa licha ya juhudi za Serikali na wadau mbalimbali katika kutoa huduma za matibabu na usaidizi wa kijamii kwa waraibu wa dawa za kulevya, bado wanawake wengi hushindwa kujitokeza kutafuta msaada kutokana na maneno makali wanayopewa, hofu ya kutengwa na kunyanyapaliwa na jamii.
Amesema jamii inapaswa kuacha vitendo vya kuwanyanyapaa, kuwatenga au kuwasema vibaya waathirika wa dawa za kulevya, kwani hali hiyo huwakatisha tamaa na kuwafanya kushindwa kurejea katika maisha ya kawaida.
“Mbaya zaidi, unyanyapaa huu hauishii tu katika jamii, wapo baadhi wanaodai hata katika vituo vya afya hukumbana na kauli za kuwatenga na kuwasimanga, jambo linalowapunguzia hamasa ya kwenda kupata tiba,” amesema Ndaba.
Aidha, ameitaka Serikali na wadau wa maendeleo kuhakikisha wanawake waliopona au wanaopambana na uraibu wanapewa nafasi katika fursa mbalimbali za kiuchumi, ili waweze kujitegemea na kuchangia katika maendeleo ya Taifa.
Kauli hiyo inakuja wakati takwimu za mwaka 2025 zikionyesha kuwa changamoto za unyanyapaa, ubaguzi na mitazamo hasi bado zinawazuia wanawake wengi kupata huduma za tiba pamoja na msaada wa kijamii na kiuchumi hata wanapokuwa tayari kuacha matumizi ya dawa za kulevya.
Kwa mujibu wa ripoti ya Mtandao wa Watanzania Wanaotumia Dawa za Kulevya (TANPUD), takribani asilimia 80 ya wanawake hukabiliwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia, kiwango ambacho ni kikubwa zaidi ikilinganishwa na wanawake wasiotumia dawa hizo.
Mmoja wa mashuhuda wa changamoto hizo, Flora Manongi, amesema waraibu wa dawa za kulevya hukutana na matatizo mengi, ikiwemo changamoto za kiafya, kutengwa na kunyanyapaliwa na jamii.
“Nitumie nafasi hii kuwaomba wenzangu ambao bado wanajaribu kufuata mkumbo wa matumizi ya dawa za kulevya waache mara moja, kwani ndani yake kuna mateso makubwa,” amesema.
Ameongeza kuwa uraibu wa dawa za kulevya huambatana na maumivu makali ya kimwili pale unapokosa dawa hizo, hali inayomtesa mtumiaji na kumfanya kushindwa kujinasua kirahisi.
“Ukishakuwa mraibu, ukikosa dawa hizo unapitia maumivu makali ya mwili, Lakini pia jamii haikuoni tena kama yule mwanamke wa awali, hapo ndipo mwanzo wa mateso yako unapoanzia,” amesema.
Akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha katika maadhimisho hayo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Arusha, Jacob Rombo, amesema Serikali inaendelea kutekeleza mipango mbalimbali ya kuwasaidia vijana kuepuka mazingira yanayoweza kuwapelekea kutumia dawa za kulevya. Amesema miongoni mwa hatua hizo ni kuwawezesha vijana kiuchumi kupitia mikopo ya ujasiriamali, pamoja na kuboresha miundombinu ya uwekezaji ili kufungua fursa zaidi za ajira na biashara.
Pia amesema Serikali imeanzisha vituo maalumu vya malezi na tiba kwa waathirika wa dawa za kulevya, maarufu kama Sober Houses, pamoja na kutoa dawa zinazosaidia kupunguza makali ya uraibu ili kuwasaidia wagonjwa kurejea katika maisha ya kawaida.