Itilima. Wakati Katibu Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenan Kihongosi akitaka Kituo cha Afya Mwamapalala kuanza kutoa huduma Juni mwaka huu, wananchi wameeleza namna kitakavyowapunguzia adha ya kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 30 kufuata huduma za afya.
Wamesema kukamilika kwake itakuwa ni mkombozi kwa wagonjwa hasa wajawazito na wazee ambao kwa muda mrefu wanakabiliwa na changamoto ya kufika katika vituo vya afya vya mbali na kijiji chao, kilichopo Wilaya ya Itilima.
Kihongosi yuko mkoani Simiyu tangu Machi 7, 2026, akikagua miradi ya maendeleo ambayo Serikali imepeleka fedha, kufuatilia uhai wa chama na kusikiliza changamoto za wananchi, akianzia Maswa.
Leo Machi 8, 2026, Kihongosi amekagua mradi wa Kituo cha Afya katika kijiji cha Mwamapalala ambacho Serikali ilitoa Sh 50 milioni za ujenzi.
Amesema chama kimeridhika kwa asilimia 100 na maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho akitoa wito kuhakikisha ifikapo Juni, 2026 kianze kutoa huduma ili wananchi waanze kutibiwa.
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Kenan Kihongosi akikagua ujenzi wa kituo cha afya Mwamapalala, wilayani Itilima.
“Nimekagua kituo hiki thamani ya fedha imeonekana, kazi kubwa na nzuri imefanyika, chama kimeridhika kwa asilimia 100.
“Wito wangu kwenu (wananchi), niwaombe mshikamane, msiposhikamana hamtaleta maendeleo, msikubali kubaguliwa au kubaguana kwa itikadi za vyama vya siasa, chama pekee ambacho kinawaletea maendeleo ni CCM,” amesema.
Awali, wakizungumza na Mwananchi, baadhi ya wananchi wamesema hulazimika kwenda kwenye Kituo cha Afya Zagayu kilichopo Kijiji cha Kabale ambacho kipo kilomita zaidi ya 30 au kile ya Misheni ambacho pia kipo mbali.
“Kwa kutembea unatumia saa moja au zaidi kulingana na mwendo wako, lakini kutembea saa nzima njiani ukiwa na mgonjwa ni changamoto,” amesema Nestory Makongo.
Mwananchi mwingine, Martha Petro amesema kukamilika kwa kituo hicho kutawasaidia hasa wajawazito kupata huduma kwa wakati.
“Tunalazimika kwenda Zagayu, ni mbali wenye uwezo wanapanda bodaboda Sh2,000, wasio na uwezo wanatembea au kutumia baiskeli,” amesema.
Amesema Kituo cha Mwamapalala kitakapoanza kutoa huduma kitawarahisishia upatikanaji wa matibabu na kupunguza hatari kwa wagonjwa waliokuwa wakichelewa kufika hospitalini.
“Hakutakuwa na gharama za bodaboda kufika kutibiwa, kwa wajawazito itaturahisishia zaidi, kwani unapoumwa uchungu ni rahisi kufika kituo cha afya,” amesema.
Akisoma taarifa ya mradi, Mfawidhi wa Zahanati ya Ukololo, Bahati Andrea amesema hadi sasa ujenzi uko kwenye asilimia 70.
Amesema ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje na matundu manne ya vyoo yapo kwenye hatua ya ukamilishaji sanjari na eneo la kuchomea taka na la kutupia kondo la nyuma.
“Hadi kufikia Juni, 2026 ujenzi utakuwa umekamilika na huduma zitaanza kutolewa mwezi huo huo,” amesema.
Amesema mradi huo uliibuliwa na wananchi tangu mwaka 2022 na kutenga eneo la ekari 17.5 kujenga kituo cha afya, lengo likiwa kusogeza huduma za afya hususani kwa mama na mtoto na wazee.
“Katika mradi huu, wananchi walichangia zaidi ya Sh 2.3milioni kwa ajili ya madini ujenzi na kulipa mlinzi; na Serikali Kuu ilitoa Sh250 milioni na hadi sasa pesa iliyotumika ni Sh214 milioni,” amesema.
Muonekano wa jengoa kituo cha afya Mwamapalala, wilayani Itilima.
Mbali na mradi wa ujenzi wa zahanati wilayani Itilima, Kihongosi amekagua shughuli za kilimo katika shamba la pamba lililopo Kijiji cha Nkololo, Kata ya Mwamapalala.
Pia, ametembelea shina la chama katika Tawi la Nkoma B na kukagua shule mpya ya msingi ya Mwankola iliyojengwa Kijiji cha Lagangabilili kabla ya kufanya mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Center Mnarani, kijijini humo.