Tehran. Tume ya kuchagua kiongozi mkuu mpya wa Iran imetangaza Jumapili kuwa imefikia uamuzi, ingawa jina la kiongozi huyo halijawekwa hadharani.
Uteuzi huu unakuja baada ya kifo cha aliyekuwa Kiongozi Mkuu, Ayatollah Ali Khamenei aliyefariki dunia katika shambulio la pamoja la Marekani na Israel Februari 28, 2026.
Mohsen Heydari, mmoja wa wanachama wa tume anayewakilisha Mkoa wa Khuzestan, alisema kupitia Shirika la Habari la ISNA kuwa: “Mgombea anayefaa zaidi, aliyepitishwa na wingi wa baraza la wataalamu, tayari ameteuliwa.”
Aidha, mwanachama mwingine, Mohammad Mehdi Mirbagheri amethibitisha kupitia video iliyoripotiwa na Shirika la Habari la Fars kwamba:
“Uamuzi thabiti unaoakisi maoni ya wengi tayari umefikiwa.”
Taarifa za awali zilimtaja Mojtaba Khamenei ambaye ni mtoto wa pili wa aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei (86), kwamba ameteuliwa kuwa mrithi wa baba yake.
Kwa mujibu wa taarifa, uteuzi huo ulitajwa ni mstari mpya wa kisiasa wa Tehran huku Mashariki ya Kati ikiendelea kushuhudia mapigano na mashambulio makali yanayoathiri miji na miundombinu ya Iran.
Mojtaba (56), anajulikana kwa uhusiano wake wa karibu na Kikosi cha Mapinduzi ya Iran (IRGC) na pia anamiliki mali nyingi kupitia mtandao wa kampuni zisizo na shughuli halisi.
Ingawa hajawahi kushika wadhifa wa kisiasa wa juu, Mojtaba alisoma kwenye shule za kidini katika mji mtukufu wa Shiite, Qom chini ya viongozi wa kidini wenye msimamo mkali.
Amezaliwa mwaka 1969 katika mji mtukufu wa Mashhad, Mojtaba wakati anakua baba yake alikuwa kiongozi wa upinzani dhidi ya Shah wa Iran.
Mke wake, Zahra Adel, na mama yake, Mansoureh Khojasteh Bagherzadeh, walipoteza maisha yao katika mashambulio ya Jumamosi, hatua iliyozidisha hali ya taharuki nchini.
Kabla ya kifo cha Khamenei, Rais wa Iran mwenye msimamo mkali, Ebrahim Raisi, alikuwa mmoja wa wagombea waliopendekezwa kuwa mrithi wake, lakini alifariki dunia katika ajali ya helikopta iliyotokea Mei 2024.
Bunge la wanachama 88, lenye jukumu la kuteua, kusimamia na hata kumfuta kazi Kiongozi Mkuu, lilikutana Qom kuamua mrithi mpya.
Hata hivyo, mashambulio ya Israel na Marekani yaliharibu jengo hilo, huku taarifa za vifo zikibaki hazijathibitishwa.
Wakati huo huo, taarifa ya Jeshi la Israel imetangaza wazi kuwa, litawalenga wote watakaochaguliwa kumrithi Khamenei.
Katika ujumbe uliochapishwa kwenye X (awali Twitter), Jeshi la Israel limesema litahakikisha kuwa hakuna mtu anayejaribu kumchagua mrithi atakayepita bila kuchukuliwa hatua.