RC Burian: Tutoe taarifa za ukatili wa kijinsia, wanawake wachangamkie mikopo ya halmashauri

Tanga. Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian, ametoa wito kwa wananchi kushirikiana kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia huku akihamasisha wanawake kutumia fursa za mikopo inayotolewa na halmashauri ili kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika leo Machi 8, 2026 katika Uwanja wa Shule ya Msingi Boma, Halmashauri ya Mji wa Korogwe mkoani Tanga, Dk Burian amesema jamii ina wajibu wa kuhakikisha wanawake na wasichana wanapata haki, usawa na fursa za maendeleo.

Amesema maadhimisho hayo yanafanyika wakati dunia ikiendelea kusisitiza haki na usawa kwa wanawake na wasichana ili kufikia maendeleo jumuishi.

“Tunasherehekea siku hii tukijitafakari tulipo na tunakoelekea. Ni kweli tumepiga hatua katika kuwawezesha wanawake, lakini bado tunahitaji kuongeza juhudi zaidi katika kupambana na changamoto zinazowakabili,” amesema Burian.

Amefafanua kuwa kauli mbiu ya mwaka huu ya maadhimisho hayo inasisitiza haki na usawa kwa wanawake na wasichana kama msingi muhimu wa kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Burian amesema wanawake si kundi dhaifu bali ni nguvu kubwa ya maendeleo katika jamii na Taifa kwa ujumla.

“Katika maandiko matakatifu, Zaburi 68:11 inatukumbusha kwamba wanawake si dhaifu bali ni jeshi la maarifa, ujasiri na matumaini. Hivyo ni wajibu wetu kuhakikisha wanapewa nafasi stahiki katika maendeleo,” amesema.

Akizungumzia suala la ukatili wa kijinsia, Dk Burian amesema takwimu bado zinaonesha changamoto hiyo ipo katika jamii na hivyo, zinahitajika hatua za pamoja kutoka kwa wananchi na taasisi mbalimbali.

Amesema kwa mujibu wa taarifa za mfumo wa taarifa za afya (DHIS-2),   katika kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka 2025/2026 Mkoa wa Tanga uliripoti jumla ya waathirika 1,737 wa ukatili wa kijinsia.

Amesema kati ya waathirika hao, wanaume walikuwa 412 huku wanawake wakiwa 1,325 waliokumbwa na vitendo mbalimbali ikiwemo ubakaji, ulawiti, ukatili wa kimwili na kihisia.

“Takwimu hizi si nzuri. Ni lazima kila mmoja wetu achukue hatua kupambana na ukatili wa kijinsia kwa kutoa taarifa mapema ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria,” amesema Dk Burian.

Amesema Serikali imeendelea kuweka mifumo ya kusaidia waathirika ikiwemo kuanzishwa kwa madawati ya jinsia katika vituo vya polisi pamoja na vituo maalumu vya huduma kwa manusura wa ukatili.

Burian pia amempongeza Rais  Samia Suluhu Hassan kwa juhudi za kuboresha huduma za afya nchini ikiwemo ujenzi wa vituo vinavyotoa huduma za upasuaji.

Amesema uwepo wa huduma hizo katika vituo vya afya umechangia kupunguza changamoto kwa wajawazito waliokuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu.

“Huduma hizi zimepunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya mama na mtoto. Wanawake sasa wanapata huduma karibu na maeneo yao,” amesema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, William Mwakilema, amesema wanawake ni nguzo muhimu katika maendeleo ya familia na jamii.

“Mwanamke akipewa nafasi anaweza. Wanawake wamekuwa mstari wa mbele katika malezi ya watoto na usimamizi wa maendeleo ya familia,” amesema Mwakilema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Ally Mkavinga, amesema maadhimisho hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kutambua nafasi ya wanawake katika maendeleo ya taifa.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Korogwe, Zahara Msangi, amesema kufanyika kwa maadhimisho ya kimkoa katika halmashauri hiyo ni fursa muhimu kwa wananchi kujifunza na kuhamasika zaidi katika masuala ya maendeleo ya wanawake.

Naye Katibu wa Mkoa wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) na mwakilishi wa vyama vya siasa mkoani Tanga, Zainab Ashraff, maadhimisho hayo si ya sherehe pekee bali ni siku ya kujitathmini kuhusu hatua zilizopigwa katika kufikia usawa wa kijinsia.

“Ni jukumu letu sote kuhakikisha wanawake wanapata fursa bora za kiuchumi na ulinzi madhubuti dhidi ya vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia,” amesema.

Aidha, Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) Mkoa wa Tanga, Al-Shaymaa Kwegir, amewahamasisha wanawake kujitokeza kwa wingi kuomba mikopo ya halmashauri ili kuimarisha shughuli zao za kiuchumi.

Baadhi ya wanawake walioshiriki kwenye maadhimisho hayo akiwemo Sofia Juma  wamesema ipo haja ya jamii kuungana kupinga vitendo vya ukatili ambavyo wamekuwa wakifanyiwa wanawake na watoto ili kuhakikisha vitendo hivyo kinapungua kama sio kuisha kabisha.