WACHEZAJI wanaocheza timu za Ligi Kuu Bara, wameanza vyema katika Michuano ya Kombe la Shirikisho (FA), baada ya kufunga ‘Hat-Trick’ tatu hadi sasa, ikiwa ni idadi kubwa kwa nyota hao tofauti na msimu uliopita wa 2024-2025, walipofunga moja.
Msimu huu wa 2025-2026, ‘Hat-Trick’, tano zimeshafungwa ikiwa ni hatua ya 32 bora na tatu ni za mastaa wa Ligi Kuu, ambao ni Yassin Mgaza wa Dodoma Jiji aliyeifungia timu hiyo kwenye ushindi wa mabao 3-1, dhidi ya Kilimanjaro Wonders.
Nyota mwingine anayeicheza Ligi Kuu aliyefunga ni Paul Peter wa JKT Tanzania na mshambuliaji huyo alifunga mabao manne, wakati kikosi hicho cha maafande kiliposhinda mabao 7-0, dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu mwaka 1982, Pan Africans.
Mchezaji mkongwe wa Namungo, Jacob Masawe amekuwa wa tatu hadi sasa kufunga pia ‘Hat-Trick’, na nyota huyo alifunga mabao matatu, wakati kikosi hicho cha ‘Wauaji wa Kusini’, kilipoifunga Kagera Sugar inayoshiriki Championship mabao 4-1.
Katika ‘Hat-Trick’ mbili kati ya hizo tano zilizofungwa ni za nyota wanaocheza Championship, ambao ni Omary Ramadhan wa Transit Camp na mchezaji huyo aliifungia timu hiyo ya maafande, ilipoichapa Chama la Wana ya Njombe kwa mabao 4-0.
Mwingine kutoka Ligi ya Championship aliyefunga ‘Hat-Trick’ ni Fredy Masota wa TMA FC na nyota huyo alifunga wakati kikosi hicho kilipoichapa Newala FC ya Mtwara kwa mabao 7-0, katika mechi iliyopigwa jijini, Arusha, Februari 19, 2026.
Msimu uliopita, jumla ya ‘Hat-Trick’ nne zilifungwa huku wachezaji wa Ligi ya Championship wakitawala zaidi kwa kufunga tatu kati ya hizo, huku moja pekee ikifungwa na aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mburkina Faso, Stephane Aziz KI.
Katika msimu wa 2024-2025, Aziz KI anayeichezea kwa sasa Al-Ittihad SC ya Libya, aliifungia Yanga ‘Hat-Trick’, wakati kikosi hicho kikiifunga Stand United ‘Chama la Wana’, mabao 8-1, kwenye mechi ya hatua ya robo fainali, Aprili 15, 2025.
Nyota watatu waliofunga wanaocheza Ligi ya Championship, walikuwa ni Kassim Shaibu ‘Mayele’ anayeichezea kwa sasa Mtibwa Sugar na aliifungia TMA ya Arusha, wakati kikosi hicho kikishinda mabao 5-1, dhidi ya Leopards FC, Desemba 5, 2024.
Elias Maguri anayeichezea msimu huu Dodoma Jiji, aliingia pia katika kumbukumbu za nyota waliofunga ‘Hat-Trick’ na nyota huyo aliifungia Biashara United, kwenye ushindi wa kikosi hicho wa mabao 5-0, dhidi ya TRA FC, Desemba 7, 2024.
Mfungaji bora wa Ligi ya Championship msimu wa 2024-2025, Raizin Hafidh, aliyefunga mabao 18, akiwa na kikosi cha Mtibwa Sugar anayocheza hadi sasa, aliifungia ‘Hat-Trick’, wakati wa ushindi wa mabao 5-3, dhidi ya Town Stars, Machi 3, 2025.
Hadi sasa tayari wachezaji watatu wa Ligi Kuu Bara wameshafunga ‘Hat-Trick’, ikiwa ni idadi kubwa zaidi tofauti na msimu uliopita, huku nyota wanaocheza Ligi ya Championship wakianza vizuri, licha ya timu nyingi hadi sasa kuaga mashindano.