Kambi ya figo Arusha kunufaisha wananchi 500 Kanda ya Kaskazini

Arusha. Katika kuadhimisha Siku ya Figo Duniani, Hospitali ya Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) imeandaa kambi maalumu ya uchunguzi wa magonjwa ya figo, mfumo wa mkojo, pamoja na mishipa ya damu kwa wananchi wa Arusha na mikoa jirani.

Huduma hizo zinazotarajiwa kufikiwa na zaidi ya wananchi 500 kuanzia Machi 9 hadi Machi 13, 2026, pia zitajumuisha tathmini ya matatizo ya nguvu za kiume na kutoa ushauri wa kitaalamu wa namna ya kuyapunguza.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha, Mkurugenzi wa Tiba wa Ushirikiano wa Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI) na ALMC, Dk Saleh Mwinchete, amesema kambi hiyo inalenga kuwapa wananchi fursa ya kufahamu hali ya afya zao, hususan uwepo wa magonjwa ya figo, matatizo ya njia ya mkojo, pamoja na changamoto zinazohusiana na mishipa ya damu.

Dk Mwinchete pia amesisitiza kuwa kambi hiyo itakuwa ni nafasi bora kwa wananchi kupata uchunguzi wa awali, ushauri wa kitaalamu na wale watakaobainika kuwa na changamoto, watapatiwa maelekezo na matibabu yanayofaa ili kuboresha afya zao kwa ujumla.

“Lengo la ugunduzi wa mapema ni ili  waweze kupata matibabu mapema na kuepukana na madhara yanayosababishwa na kuchelewa vipimo.”

Dk Mwinchete amesema lengo la tathmini ya matatizo ya nguvu za kiume ni kutoa fursa kwa wananchi kupata uchunguzi mapema, kwani matatizo mengi yanatokana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza au kuathirika kwa njia ya mkojo.

“Kila mshiriki atapata uchunguzi wa awali, ushauri wa kitaalamu, na wale watakaobainika kuwa na changamoto watapatiwa matibabu pamoja na maelekezo ya kimsingi ya kuishi kwa afya bora,” amesema.

Amesema kambi hiyo itakuwa na madaktari bingwa na bobezi wapatao 10 kutoka hospitali za Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI) pamoja na ALMC, wataotoa huduma za uchunguzi na ushauri kwa wagonjwa wa magonjwa ya figo, moyo, mishipa ya damu na mfumo wa mkojo.

Dk Mwinchete amesema kuhusu huduma za mishipa ya damu, wagonjwa watapatiwa uchunguzi wa kitaalamu, ushauri wa kitaalamu, na kwa wale wenye uhitaji maalumu, itatolewa huduma ya kuweka njia ya kudumu ya kusafisha damu (Permanent Dialysis Catheter), huduma inayosaidia wagonjwa wenye matatizo makubwa ya figo.

Mkurugenzi wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema kambi hiyo inalenga kusogeza huduma za afya karibu na wananchi, kuwahamasisha kufanya uchunguzi mapema, na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kujali afya ya figo, moyo, mishipa ya damu na mfumo wa mkojo.

“Tunafanya hivi kwa sababu watu wengi hufika hospitalini wakiwa tayari wamechelewa na magonjwa yako katika hatua za mwisho, hivyo kuwa ngumu na gharama kupata tiba.

“Tunawasihi wananchi wajitokeze kwa wingi kutumia fursa hii ya uchunguzi na ushauri wa bure, kwani uchunguzi wa mapema unaweza kusaidia kugundua magonjwa kabla hayajawa makubwa,” amesema.