Pwani. Kaya 1,000 Lindi na Pwani zafikiwa na huduma ya gesi asili majumbani
Kaya 1,000 katika mikoa ya Lindi na Pwani zimeanza kunufaika na mradi wa usambazaji wa gesi asilia majumbani baada ya kufikishiwa huduma hiyo.
Hayo yameelezwa leo, Machi 8, 2026 na Mhandisi Mwandamizi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Anthony Karomba, wakati wa ziara ya kutembelea miradi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) iliyowashirikisha wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari.
Amesema mradi huo ulioanza Machi mwaka jana na kukamilika Januari mwaka huu, umefadhiliwa na REA na umewanufaisha kaya 530 za Kisemvule mkoani Pwani, kaya 470 mkoani Lindi pamoja na taasisi moja.
Amesema mfumo wa matumizi ya huduma hiyo ni wa malipo kabla (prepaid), kama ilivyo Luku. Wananchi wamefungiwa mita, hivyo hununua tokeni na kuingiza kwenye mita kisha kuanza kutumia.
“Unit moja ni Sh1,000. Mfano, familia ya watu sita wanaweza kutumia unit moja kupika milo mitatu kwa siku,” amesema.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi REA, Mhandisi Emanuel Yesaya amesema mamlaka hiyo imefadhili mradi huo kwa Sh6.8 bilioni, lengo likiwa ni kusaidia wananchi kupata huduma kwa urahisi na kuboresha afya zao kwa kutumia nishati salama.
Mhandisi Yesaya amesena hivi karibuni Shule ya Msingi Kisemvule itaingizwa katika mradi huo kwa kuwekewa jiko linalotumia mfumo huo wa gesi.
Amesema katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha 2026/2027 wanatarajia kuwezesha utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo utakaogharimu Sh7 bilioni.
Mkazi wa Kisemvule, Mariam Rashidi akipika kwa kutumia gesi asilia aliyounganishwa nyumbani kwake kupitia mradi wa usambazaji gesi asilia majumbani.
Pia amesema kwa sasa sheria ya kuanzishwa kwa wakala huo ipo katika mchakato wa kufanyiwa mapitio ili kupanua wigo wa majukumu yao kutokana na uhitaji mkubwa wa huduma hizo kwa wananchi.
Baadhi ya wanufaika wa mradi huo wameeleza unafuu wa gharama na urahisi wa kutumia gesi hiyo.
Mariam Rashid, mkazi wa Kisemvule amesema tangu aanze kutumia gesi hiyo ameacha matumizi ya mkaa, na gesi inapokwisha anaweza kununua muda wowote.
“Naweza kununua gesi ya Sh1,000 ambayo natumia kwa siku tatu. Sihangaiki kama zamani.
“Wakati watu wa REA walipokuja kuhamasisha mradi, baadhi ya wananchi walikataa kwa kuhofia nyumba zao zitalipuka, lakini sasa wanakuja kwangu niwape mawasiliano ya watu wa REA ili nao wawekewe.”
Kaimu meneja usaodizi wa kiufundi wa Wakala wa Nishati Vijijini (Rea), Mhandisi Emanuel Yesaya akionesha mita ya gesi aliyofungiwa mwananchi nyumbani kwake
Amesema anapata unafuu hasa wakati huu wa mwezi wa Ramadhani kwani hatumii gharama kubwa kupika futari na daku.
“Zamani nilikuwa natumia vipimo vinne vya mkaa kwa siku ambavyo kila kimoja ni Sh1,000. Hata nilipokuwa natumia gesi za mitungi nilikuwa na wasiwasi wa kuisha ghafla,” amesema Mariam mwenye kaya ya watu watano.
Naye Mariam Sekena, mkazi wa Kisemvule amesema tangu aanze kutumia gesi hiyo miezi miwili iliyopita ameona nafuu kubwa katika matumizi ya nishati ya kupikia.
Mwenyekiti wa kitongoji cha Kitangwi kilichopo Kata ya Vikindu, Hussein Shemndolwa amesema bado wananchi wengi wanahitaji kufikiwa na huduma hiyo kwani kitongoji hicho kina kaya zaidi ya 12,000.
Meneja Mipango miradi na utafiti wa Rea, Mhandisi Jensen Mahavile akitoa maelezo kuhusu mradi wa usambazaji gesi asilia majumbani, leo Maxhi 8, 2026 wakati wa ziara ya kutrmbea miradi inayotelelezwa na Rea, eneo la Kisemvule.
“REA iendelee kufadhili miradi ya aina hii ili wananchi wengi zaidi wanufaike kwa kuwa ni huduma nafuu na rahisi,” amesema.