Moshi. Wakati takwimu zikionesha kuwa asilimia 14.4 ya wanawake nchini wanaugua saratani ya matiti, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini KCMC, imesema baadhi yao hufika wakiwa katika hatua ya tatu na nne ya ugonjwa hali ambayo inapelekea wastani wa wanawake wanne kukatwa matiti kila wiki.
Hayo yamesemwa leo Jumapili Machi 8. 2026 na Ofisa Uhusiano wa hospitali ya hiyo, Gabriel Chisseo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na ugonjwa huo.
Amesema kwa siku katika idara hiyo wanaona watu 40 hadi 100 wakiwemo watoto, vijana, watu wazima na wazee.
“Niseme tu, Shirika la Msamaria Mwema limekuwa likilipia watoto wenye miaka 0-18 bure na tumekuwa tukisamehe Sh9 bilioni kwa mwaka kwa ajili ya matibabu ya saratani kwa watoto, lakini kuna vijana, tezi dume, saratani za damu, shingo ya mlango wa kizazi.
“Hapa kwetu saratani ya shingo ya kizazi ndio inayoongoza ikifuatiwa na saratani ya matiti na tumekuwa tukikata wanawake wanne matiti kila wiki,” amesema Chisseo.
Aidha, amesema baadhi ya wanawake wanaofika katika hospitali hiyo wanakuwa katika hatua za tatu na nne za ugonjwa hali ambayo inakuwa ngumu kwa mgonjwa kupata huduma stahiki.
“Tumejikita sana kutoa elimu ya saratani ya mlango wa kizazi pamoja ya matiti kwa watu wa Kanda ya Kaskazini na hizi takwimu unaweza kuziona ni chache, lakini ni nyingi sana na ukiangalia ni rika zote zina hii changamoto ya saratani,” amesema Chisseo.
Aidha, amesema hospitali hiyo kupitia taasisi yake ya utafiti(KCRI) inaendelea na utafiti wa kina na kuja na majibu kuhusiana na tatizo, hilo ili kama ni elimu itolewe kwa kina.
Hivi karibuni, mtafiti na mwanafunzi wa shahada ya uzamivu kutoka Chuo Kikuu cha KCMC, Elizabeth Msoka amesema asilimia 70 ya wagonjwa wanaofika katika hospitali hiyo wanafika wakiwa katika hatua ya tatu na nne ya ugonjwa jambo ambalo linahatarisha matibabu na kupelekea asilimia ndogo ya mgonjwa kupona.
“Tunachokiona hapa kwetu KCMC wagonjwa wengi wanaokuja na saratani wanakuja katika hatua ya kuchelewa ambapo ni hatua ya nne na ya tatu, mwaka 2021 na 2022 asilimia zaidi ya 70 ya wagonjwa waliokuja kupatiwa matibabu walikuja katika hatua ya nne na ya tatu ya ugonjwa jambo ambalo linahatarisha matibabu ya mgonjwa kutokana na kuchelewa,” amesema.
Aidha, amesema endapo mgonjwa akiwahi kupata matibabu ugonjwa huo unatibika na kuwaasa wanajamii kuwa na desturi ya kupima mara kwa mara ili kujiepusha na ugonjwa huo.