Ruangwa. Wazazi na walezi wametakiwa kuwalea watoto katika maadili yanayoendana na dini zao badala ya kuwaachia simu za mkononi na televisheni kuamua malezi yao.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika katika Kijiji cha Mbekenyera, wilayani Ruangwa leo Jumapili, Machi 8, 2026.
Amesema kuwa malezi bora ni yale yanayowafundisha watoto tabia njema, maadili mema na mafunzo ya kidini, si kuwapa uhuru wa kutazama au kufanya chochote wanachopenda kupitia simu au TV.
“Watoto wanapoachwa bila mwongozo, wanaweza kuangalia au kujifunza chochote bila kizuizi. Hivyo, wazazi na walezi wanatakiwa kuwa walinzi wa malezi bora kwa watoto wao,” amesema.
Mkuu wa mkoa amesisitiza kuwa malezi mema ni msingi wa jamii yenye maadili na utamaduni unaoheshimika, na kwamba kila mtoto anastahili kupata mwongozo wa kimaadili kutoka kwa wazazi wake, badala ya kuachwa kwa urahisi mbele ya teknolojia.
Aidha, amewataka wazazi kushirikiana na jamii na mashirika ya kijamii kuhakikisha malezi yanayofundisha watoto heshima.
“Baba na mama tunawajibu wa kulea watoto wetu na familia yetu kwa watoto wote wa kike na kiume, na tujitahidi kuacha malezi ya kizungu kwa kuwaachia simu wachezee au kuangalia TV wao wenyewe,” amesema Telack.
Aidha, amesema changamoto kubwa inayowakabili wanawake bado ni vitendo vya unyanyasaji majumbani, pamoja na dhuluma na uonevu wa kijamii.
Amesisitiza kuwa Serikali ya mkoa itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na vitendo hivyo, ikiwamo unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto.
“Naamini tumepata ujumbe kwamba kinachowaumiza wanawake wengi ni unyanyasaji majumbani.
“Dhuluma na uonevu tutaufanyia kazi haraka sana, na tayari tumeanza kushughulikia masuala ya unyanyasaji wa kijinsia hata kwa watoto wakiwemo wa kiume,” amesema Telack.
Mkazi wa kijiji hicho, Hadija Mohamed amesema wazazi wengi wamekuwa wakijisahau katika suala la malezi, muda mwingi mzazi amekuwa akiwa anapoteza muda kwenye mitandao lakini sio kumuangalia mtoto.
“Aliyozungumza mkuu wa mkoa yapo sahihi sisi wazazi tumekuwa hatuwajali watoto wetu muda mwingi tumekuwa bize mitandaoni, si wakukagua madaftari ya mtoto anaporudi shule, kukaa naye kuzungumza naye, hilo sasa hivi hatuna wazazi, ndiyo maana watoto wetu wanaharibikiwa sana,” amesema Mohamed.